Takaichi alichaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Japan, hatua iliyowekwa historia. Uteuzi wake ulihitimisha miezi kadhaa ya mkwamo wa kisiasa ndani ya chama tawala. Hii ilikuja baada ya mfululizo wa kushindwa kwa uchaguzi uliosababisha kupoteza wingi wa kura bungeni.
Katika hotuba yake ya kwanza ya sera, Takaichu alitangaza kuwa Japan itafikia lengo la kutumia asilimia mbili ya pato la taifa kwa ulinzi ifikapo Machi. Awali, lengo hilo lilikuwa limepangwa kutimizwa mwaka 2027. Uamuzi huu unaashiria msimamo wake wa kuongeza kasi ya ujenzi wa jeshi la nchi hiyo.
“Nitakabiliana na changamoto zinazoikabili dunia”
Bi Takaichi amesema serikali yake itakamilisha mapema marekebisho ya mkakati wa usalama wa taifa. Mpango huo mpya unatarajiwa kuwa tayari kabla ya mwisho wa mwaka 2026. Hapo awali, Japan ilikuwa inafanya mapitio ya mkakati wa usalama takribani kila baada ya miaka kumi.
“Nimeazimia kugeuza wasiwasi wa wananchi kuhusu maisha yao ya sasa na ya baadaye kuwa matumaini, na kujenga uchumi thabiti. Nitaiwezesha Japan kuwa taifa lenye nguvu na ustawi. Nitakabiliana na changamoto zinazoikabili dunia na kurejesha hadhi ya diplomasia ya Japan ili ichangamie tena katikati ya jamii ya kimataifa. Kwa dhamira ya kutokata tamaa kamwe, ninaahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo wa dhati kwa ajili ya taifa letu na watu wake”, alisema Takaichi.
Takaichi alifafanua kuwa mabadiliko haya yanachochewa na mazingira mapya ya usalama duniani. Alitaja uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kama ishara ya hatari mpya. Pia alisema migogoro ya Mashariki ya Kati imeongeza hali ya wasiwasi kimataifa.
Wasiwasi kuhusu usalama wa kikanda
Katika hotuba yake, alionya kuwa mpangilio wa dunia huru na thabiti unatikiswa kwa kasi kubwa. Alisema ushindani wa kisiasa na kijeshi unazidi kuongezeka, hali inayohitaji mataifa kuwa na mikakati mipya ya kujilinda.
Takaichi alielezea wasiwasi wake kuhusu shughuli za kijeshi za majirani wa Japan. Alisema China, Korea Kaskazini na Urusi zinachukua hatua zinazotia hofu kubwa. Serikali yake imeeleza dhamira ya kujibu vitisho hivyo kwa kujenga uwezo wa kujihami zaidi.
Amehimiza Japan kuimarisha misingi ya kujilinda na kuongeza nguvu ya kiulinzi, na kuongeza kuwa nchi hiyo haiwezi kutegemea washirika pekee katika usalama wake. Kwa maoni yake, kujitegemea kijeshi kutaleta uthabiti wa muda mrefu.
Ahadi yake imekuja siku chache kabla ya ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump. Ziara hiyo itahusisha mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu uhusiano wa kijeshi. Trump anatarajiwa kuiomba Japan kuongeza zaidi matumizi yake ya ulinzi.
Takaichi amesema anataka kujenga uhusiano wa kuaminiana na Trump. Ameahidi kuinua ushirikiano wa Japan na Marekani hadi “kiwango kipya.” Mazungumzo yao yanatarajiwa kuimarisha ushirika wa kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema Japan inahitaji wafanyakazi wa kigeni kufidia upungufu wa nguvu kazi unaosababishwa na kuzeeka kwa watu. Hata hivyo, ameonya kuwa ni wale tu wanaoheshimu sheria na taratibu watakaoruhusiwa kufanya kazi nchini humo. Amesisitiza kuwa hatua hiyo si chuki dhidi ya wageni, bali ni kulinda nidhamu na utulivu wa jamii.
