Umoja wa Ulaya Jumapili sasa unazitaka mamlaka nchini Tanzania kujiepusha kuchochea vurugu Pamoja na kutumia nguvu kukabiliana na waandamanaji waliojitokeza siku ya Jumatano kupinga uchaguzi wa nchi hiyo, ambapo rais Samia Suluhu Hassan, alitangazwa mshindi.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Kaja Kallas, taarifa za uhakika kuwa kuna idadi kubwa ya watu waliouawa wakiwemo mamia ya majeruhi zinagusa kila mmoja, akizitaka mamlaka kulinda haki na uhai wa raia wake.

“Ripoti za kuaminika za idadi kubwa ya vifo na majeraha makubwa zinatia wasiwasi mkubwa. EU inazitaka mamlaka kujizuia kwa kiasi kikubwa ili kuhifadhi maisha ya watu,” ameongeza.

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, kimefutilia mbali ushindi mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan siku ya Jumapili.

Hesabu ya mwisho inaonyesha kuwa Chama Cha Mapinduzi, CCM, chama cha rais kimeshinda kwa 98% ya kura.

Chadema, ambacho kilizuiliwa kushiriki uchaguzi kwa kukataa kusaini kanuni za maadili, kimedai matokeo yalighushiwa.

Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, chama hicho kimesema: “Chadema inafutilia mbali vikali kile kinachoitwa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Matokeo haya hayana msingi wowote katika uhalisia, kwani ukweli ni kwamba hakuna uchaguzi wa kweli uliofanyika Tanzania.”

“Maandamano kote nchini yanaonyesha wazi kwamba raia hawakushiriki katika kile kinachoitwa uchaguzi na kwamba wanampinga mtu yeyote aliyetoka katika mchakato huu wa uchaguzi wenye dosari,” taarifa hiyo imeongeza.

Kauli ya umoja wa Ulaya ni kama ile iliyotolewa na Jumuiya ya Madola pamoja na jumuiya za kikanda, ambapo wote wameeleza kuguswa na kinachoendelea kuripotiwa kutoka Tanzania baada ya uchaguzi.

Mgombea urais wa upinzani alizuiliwa kugombea

EU imeongeza: “Kutokuwepo kwa hali ya haki katika kipindi kilichotangulia uchaguzi kulishuhudiwa na ripoti za utekaji nyara, watu kutoweka, na vurugu zinazozuia nafasi ya kiraia na kidemokrasia.

“EU inatoa wito wa kuachiliwa kwa viongozi wote wa kisiasa waliokamatwa, kesi ya uwazi na ya haki kwa wale waliokamatwa pamoja na uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu ripoti zote za utekaji nyara, watu kutoweka, na vurugu.”

Bi. Samia, ambaye alihudumu kama makamu wa rais kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, alichukua urais kufuatia kifo cha John Magufuli.

Siku ya Jumamosi, Hassan alihudhuria hafla katika mji mkuu wa utawala, Dodoma, kupokea cheti chake cha ushindi kutoka kwa mamlaka ya uchaguzi. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 65 aliwapongeza Watanzania kwa kupiga kura nyingi kwa niaba ya mwanamke kama kiongozi wao na akaongeza: “Sasa kwa kuwa uchaguzi umekwisha, ni wakati wa kuunganisha nchi yetu na kutoharibu kile ambacho tumejenga kwa zaidi ya miongo sita.” “Tutachukua hatua zote muhimu na kuhusisha vyombo vyote vya usalama ili kuhakikisha amani nchini.”

Chanzo cha usalama na mwanadiplomasia mmoja jijini Dar es Salaam wote wameliambia shiika la habari la AFP kwamba idadi ya vifo ilifikia “mamia.” Serikali inapinga takwimu hizi.

Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Seif Magango, alisema katika mkutano na waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa huko Geneva siku ya Ijumaa, kupitia mkutano wa video kutoka Kenya, kwamba kulikuwa na ripoti za kuaminika za vifo 10 jijini Dar es Salaam, na pia katika miji ya Shinyanga na Morogoro.

Siku ya Ijumaa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionyesha wasiwasi wake kuhusu hali nchini Tanzania na akazitaka pande zote kuzuia ongezeko zaidi la machafuko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *