
Mvutano unaongezeka kati ya Washington na Caracas baada ya shambulio lingine la Marekani dhidi ya meli ya Venezuela katika Bahari ya Caribbean. Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa jeshi la Marekani limelenga boti inayoshukiwa kusafirisha mihadarati kuelekea Marekani. Watu watatu wameripotiwa kuuawa katika operesheni hiyo iliyofanyika siku ya Jumatatu, Septemba 15. Hili ni shambulio la pili katika muda wa chini ya mwezi mmoja.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Video iliyorushwa kwenye jukwaa la Truth Social inaonyesha meli ikilipuka baharini. Kulingana na Donald Trump, boti iliyolengwa ilikuwa imebeba “mifuko mikubwa ya kokeini na fentanyl.” “Ilikuwa kila mahali katika bahari,” rais wa Marekani amesema.
Shambulio hilo lilifanyika “katika eneo la uwajibikaji la Southcom,” kamandi ya jeshi la Marekani katika Amerika Kusini na Karibiani, Donald Trump amebainisha. Watu watatu waliotajwa kuwa “magaidi wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya” kutoka Venezuela waliuawa, kulingana na rais wa Marekani, ambaye anadai kuwa na “ushahidi” wa kuwepo kwa madawa ya kulevya katika boti hiyo.
Mvutano kati ya Washington na Caracas umeongezeka katika wiki za hivi karibuni baada ya jeshi la Marekani kupeleka meli saba za kivita katika Karibiani na nyingine kwenye Pasifiki. Kipindi hiki cha hivi punde kinakuja baada ya shambulio la kwanza Septemba 2 dhidi ya meli nyingine katika visiwa vya Caribbean, ambapo Marekani imetuma vikosi vya kijeshi, rasmi kwa jina la kupambana na makampuni ya madawa ya kulevya. Operesheni hii ya kwanza iliwaangamiza kumi na moja, kulingana na mamlaka ya Marekani.
Katika mahojiano kwenye Fox News, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ametetea shambulio la kwanza dhidi ya boti hiyo, ambayo ilikuwa katika maji ya kimataifa, na kuibua maswali kuhusu uhalali wake.
Makundi (…) yaliua watu 300,000 katika nchi yetu mwaka jana, hatutaacha hilo litokee tena.
Donald Trump anaahidi kwamba vita dhidi ya makampuni ya biashara vitaongezeka
Caracas inashutumu “uchokozi wa kijeshi”
Marekani inamtuhumu Rais wa Venezuela Nicolás Maduro kwa kuongoza mtandao wa ulanguzi wa dawa za kulevya, Cartel of the Suns – ambao kuwepo kwake bado ni suala la mjadala. Imeongeza maradufu zawadi iliyotolewa kwa kukamatwa kwake hadi Dola Milioni 50.
Kwa kujibu, Nicolas Maduro ameshutumu kile anachokiita “uchokozi unaoendelea wa asili ya kijeshi,” akisema kwamba Venezuela “imepewa mamlaka na sheria za kimataifa kujibu” na kwamba mawasiliano na Washington yamekatishwa. Rais wa Venezuela pia amekanusha shutuma za Marekani kama “uongo,” akisema kuwa kokeini iliyosafirishwa kwenda Marekani kimsingi ilipitishwa kupitia bandari za Pasifiki na Ecuador. Kulingana naye, Marekani inataka “kuleta mabadiliko ya utawala ili kunyakua utajiri mkubwa wa mafuta na gesi wa Venezuela.”
Katika wiki za hivi karibuni, Nicolas Maduro ametoa wito kwa watu kujiandikisha katika wanamgambo, kikosi chenye siasa kali kilichoundwa na Rais wa zamani Hugo Chavez (1999-2013). Pia alitangaza kutumwa kwa wanajeshi 25,000 kwenye mipaka.
Uvumi umeenea kuwa utawala wa Trump unajiandaa kufanya shambulio la moja kwa moja kwenye ardhi ya Venezuela. Alipoulizwa kuhusu uwezekano huo, Donald Trump ametilia shaka hili. “Tutaona kitakachotokea,” amejibu. Lakini uhalali wa mashambulizi haya umesababisha ukosoaji mkali. “Ninachotaka kusema kwa makampuni ya biashara ni kwamba tutasimamisha usafirishaji huu kwa njia ya barabara pia, kama tulivyofanya kwa njia ya baharini. Waliua watu 300,000 katika nchi yetu mwaka jana,” Donald Trump ametetea, akimaanisha vifo vinavyotokana na dawa za kulevya. “Hatutaacha hilo litokee tena.”