Ziara ya Trump inafanyika wakati vita vinaendelea Ukraine na Mashariki ya Kati, mataifa makubwa yakikabiliana na ushuru wa Marekani, na hii leo Uingereza ina matumaini kuwa maonesho ya kifalme yaweza kumvutia Trump na kumuweka upande wao.
Trump amekuwa akivutiwa na familia ya kifalme kwa muda mrefu na atapokelewa kwa msafara wa gari la kifahari akiwa na Mfalme Charles III pamoja na karamu kubwa ya kitaifa katika Kasri la Windsor.
Kiongozi wa chama cha Labour, Kier Starmer, si mshirika wa kawaida wa kisiasa wa Trump mwenye mrengo mkali wa kulia, lakini amekuwa akijitahidi kumvutia tangu alipochaguliwa tena kuwa Rais mwezi Januari.
Starmer alimpa mwaliko rasmi kutoka kwa mfalme katika Ikulu ya White House mwezi Februari. Trump alikubali mwaliko na kumwambia Starmer kuwa Mfalme Charles, ambaye kwa sasa anapata matibabu ya saratani ni “mtu mzuri sana.”
Olivia O’sullivan mchambuzi wa siasa za Uingereza anasema “Sawa, ulikuwa mwaliko muhimu kwa Uingereza, si kawaida kutoa mwaliko wa ziara ya pili ya kitaifa kwa mkuu wa taifa. Lakini Uingereza inatamani kuhakikisha kuwa inaweza kupata jambo la kimkakati na lenye maana kutoka kwenye ziara hii.”
“Serikali ya Uingereza inakabiliwa na changamoto ngumu kwa sababu Marekani kwa muda mrefu imekuwa mshirika wake mkuu wa usalama, lakini siasa zake zinazidi kuwa ngumu. Hivyo kama viongozi wengine wa Ulaya, Starmer anapaswa kubaini jinsi ya kumshughulikia Trump binafsi na mtazamo wake kwa washirika na wasiokuwa washirika, ambayo inaweza kuwa hali tete na ya kubadilika.” aliongeza O’sullivan
Kesi ya Epstein
Hata hivyo, sakata la mhalifu wa kingono Jeffrey Epstein na vita vya kisiasa kuhusu uhuru wa kujieleza vinaweza kuleta hali ya sintofahamu wakati Trump atakapokutana na Waziri Mkuu wa Uingereza aliye katika wakati mgumu.
Starmer amekuwa akikabiliwa na maswali kuhusu uamuzi wake wa kumteua Peter Mandelson kama balozi wa Uingereza nchini Marekani, licha ya urafiki wake wa muda mrefu na Epstein.
Trump naye pia anakabiliwa na maswali mazito kuhusu uhusiano wake na mhalifu huyo wa kingono, ambaye pia urafiki wake na ndugu mdogo wa Charles, Andrew, uliwaweka familia ya kifalme katika hali ya aibu.
Uwekezaji wa Marekani
Katika mkutano wao, viongozi hao wawili wanatarajiwa kusaini mikataba ya thamani ya pauni bilioni 10 , ikiwemo ule wa kuharakisha miradi mipya ya nyuklia pamoja na kile maafisa wa Uingereza walichokiita “ushirikiano wa kiteknolojia wa hali ya juu duniani”.
Kabla ya ziara hii, kampuni ya Google ilitangaza kuwa itawekeza pauni bilioni 5 nchini Uingereza katika kipindi cha miaka miwili ijayo, huku kampuni za kifedha za Marekani kama PayPal na Citi Group zikitangaza uwekezaji wa pauni bilioni 1.25.
Trump, ambaye mama yake alizaliwa Scotland, atakuwa rais wa kwanza wa Marekani kupata ziara ya pili ya kitaifa, baada ya ile ya mwaka 2019 alipokutana na Malkia Elizabeth II.