Jeshi la Israel limeishambulia Gaza City kutoka ardhini usiku wa kuamkia leo huku vikosi vyake vikitanua operesheni hizo katika ngome ya wanamgambo wa Hamas katikati ya mji huo. Jeshi hilo limesema limeingia katika hatua yake ya mwisho inayonuiwa kulisambaratisha kabisa kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina.
Jeshi limesema linaamini bado maelfu ya wanamgambo wa Hamas wamejificha mjini humo. Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee ameandika katika mtandao wake wa X kwamba Gaza sasa, inachukuliwa kama mahali hatari pa mapambano na kuendelea kukaa huko ni sawa na kujiweka hatarini huku Waziri wa Ulinzi Israel Katz akisema Gaza kwa sasa inawaka moto.
Nalo Shirika la habari la Kipalestina la WAFA limeripoti ndege za kivita za Israel kushambulia Gaza usiku kucha huku vifaru vya kivita vikionekana kuingia katika mji huo ambao ni makaazi kwa maelfu ya Wapalestina. Awali jeshi la Israel liliwataka wakaazi kuondoka mji huo na kukimbilia katika maeneo ya kusini katika eneo la pwani lililozingirwa.
Haya yote yanatokea wakati Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Marco Rubio akielekea Qatar kutokea Israel anakopanga kukutana na wakuu wa taifa hilo la Kiarabu, ambao bado wamekasirishwa na hatua ya Israel kuishambulia ardhi yake na kuwauwa watu sita, akiwemo afisa mmoja wa usalama.
Akizungumza na waandishi habari alipoondoka Israel, Rubio alithibitisha kuanza kwa operesheni hiyo ya ardhini dhidi ya Hamas.
“Kama mnavyojua Waisraeli wameanza kufanya operesheni zao huko, kwa hivyo tunadhani tuna muda mfupi sana wa kufikia makubaliano. Hatuna miezi tena, na labda tuna siku na hata wiki chache, kwa hivyo ni wakati maksusi na muhimu, alisema Marco Rubio.”
Nchi za kiarabu na kiislamu zataka mapitio ushirikiano na Israel
Rubio ameyasema hayo wakati viongozi takriban 60 wa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu waliokutana mjini Doha kwa mkutano wa dharura wa siku mbili kujadili shambulio la Israel nchini humo kutoa wito wa kuangalia upya mahusiano yao ya kidiplomasia na taifa hilo. Walikubaliana kwa pamoja kuchukua hatua za kisheria na kiutendaji kuizuia Israel kuendelea na hujuma dhidi ya Wapalestina.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit, alisema ni muda sasa wa dunia kuvunja ukimya wake kuhusu tabia ya Israel aliyoiita ya kichokozi.
“Miaka miwili ya ukimya juu ya uhalifu na ukatili unaofanyika Gaza inatoa picha kwa viongozi wanyakuzi kwamba chochote kinawezekana na uhalifu unaweza kufanywa bila kuadhibiwa. wameendelea kuharibu nchi moja baada ya nyengine na kuleta vurugu katika eneo zima. Tunatoa ujumbe kwa Jumuiya ya kimataifa kwamba ukimya umetosha kwa taifa hili la Israel lililochoma eneo zima la Mashariki ya Kati, lililosababisha njaa, mauaji na kuwakosesha watu makaazi bila kuwajibishwa.”
Wakati huo huo, ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa imeishutumu Israel moja kwa moja kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza ikimyooshea kidole cha lawama Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Tume huru ya kimataifa ya Umoja huo inayoongozwa na Navi Pillay imesema mauaji hayo yametokea Gaza na yanaendelea. Israel kupitia wizara yake ya mambo ya nje imekanusha ripoti hiyo na kuiita ya uwongo.