
Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegseth, amewaamuru mamia ya majenerali na maadmeri wa Pentagon walioko kila pembe ya dunia kuripoti kwenye kambi ya Marine Corps iliyoko Quantico, Virginia, wiki ijayo, hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa na ambayo imezua wasiwasi katika safu za juu za jeshi la nchi hiyo.
Pentagon imethibitisha mkutano huo lakini haijatoa maelezo yoyote.
Msemaji wake mkuu Sean Parnell alieleza katika taarifa aliyotoa siku ya Alkhamisi: “Waziri wa Vita atawahutubia viongozi waandamizi wa jeshi mapema wiki ijayo”.
Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye mwezi uliopita alibadilisha jina la Pentagon kutoka Wizara ya Ulinzi na kuwa “Wizara ya Vita,” ametoa maanani wasiwasi uliojitokeza kuhusiana na hatua hiyo ya Hegseth na kuuelezea mkutano huo kuwa ni mkusanyiko wa pamoja wa “kirafiki”.
Trump amewaeleza waandishi wa habari katika Ikulu ya White House: “inapendeza wakati majenerali na watu wakuu wanapotaka kuja Marekani kuwa pamoja na anayeitwa sasa Waziri wa Vita,” na kuongeza kuwa makamanda hao watatembelea pia maeneo ya zana za kivita na kuzungumzia silaha mpya zaidi zilizopo.
Pamoja na hayo, maafisa wa kijeshi wamesema, wakati ni utaratibu wa kawaida kwa Wakuu wa Vikosi na makamanda wa vitani kukutana mara mbili kwa mwaka huko Washington, kuitwa tena mamia ya maafisa – wakiwemo wakuu wanaotoka kwenye maeneo yenye mizozo ya kijeshi – ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa…/