
Shirika la Intelijensia na Usalama la Somalia (NISA) limetangaza kuwa limetekeleza operesheni ya mashambulizi iliyowalenga viongozi wa kundi la kigaidi la Al-Shabab na kuua magaidi 24 akiwemo kiongozi wa kundi hilo aliyekuwa akisakwa kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa NISA, operesheni hiyo ilitekelezwa kwa ushirikiano wa washirika wa usalama wa kimataifa katika mikoa ya Hiran, Galgadud, na Lower Shabelle.
Abdi Hiray, kiongozi wa Al-Shabaab ambaye amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na Shirika la Intelijensia la Somalia, alikuwa miongoni mwa waliouawa katika operesheni hiyo kwenye eneo la Hiran; na magaidi wengine 21 wameuawa katika kijiji cha Tugarey eneo la Lower Shabelle na lile la kati la Galgadud.
NISA imetangaza kuwa, Hiray alihusika na njama na mashambulizi kadhaa yaliyosababisha madhara kwa raia katika jimbo la kusini kati la Hirshabelle.
Taarifa ya shirika hilo imesema: “operesheni hizi ni sehemu za juhudi zinazoendelea kusambaratisha kundi la Khawarij na kuzuia njama zozote mbaya dhidi ya watu wa Somalia”.
‘Khawarij’ ni msamiati ambao serikali ya Somalia huutumia kulitambulisha kundi la kigaidi la Al-Shabab lenye mfungamano na mtandao wa Al-Qaeda.
Tangu mwezi Julai, jeshi la Somalia, kwa msaada wa vikosi vya Umoja wa Afrika, AUSSOM na washirika wengine wa kimataifa, limezidisha operesheni dhidi ya kundi hilo la kigaidi katika mikoa ya kusini na kati ya Somalia.
Kundi la Al-Shabaab, ambalo limekuwa likifanya hujuma za kigaidi dhidi ya serikali ya Somalia kwa zaidi ya miaka 16, mara nyingi linavilenga vikosi vya usalama, maafisa, na raia…/