Juhudi hizi za Marekani zinajiri baada ya wikiendi iliyoshuhudia machafuko mapya yaliyosababisha vifo vya wanajeshi wawili wa Israel na watu takriban 45 upande wa Gaza. Hata hivyo, licha ya pande zote mbili kurudia ahadi ya kuheshimu makubaliano hayo, mashambulizi mapya yanayoendelea yameibua shaka kuhusu uwezo wa Marekani kudumisha kasi na shinikizo la kidiplomasia katika juhudi za kurejesha utulivu.
Utawala wa rais Donald Trump wa Marekani umeongeza maradufu juhudi zake za kudumisha mkataba huo dhaifu wa usitishaji mapigano huko Gaza, kwa kumtuma nchini Israel Makamu wa Rais JD Vance anayetarajiwa kuwasili hii leo. Ziara ya Vance inajiri baada ya Mjumbe maalum wa Trump Steve Witkoff na mshauri na mkwe wake Jared Kushner kukutana na Netanyahu siku ya Jumatatu kujadili hali halisi inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.
Licha ya matukio ya vurugu ya mwishoni mwa juma, Israel na Hamas zimesema ziko tayari kuendelea kuheshimu makubaliano hayo ambapo Trump alionya kuwa anatoa nafasi kwa Hamas “kutuliza hali” la sivyo “itaangamizwa”. Trump ameongeza kuwa Hamas kwa sasa ni dhaifu mno hasa kutokana na kwamba mtetezi wake wa kikanda Iran haina uwezekano wa kuingilia kati kuisaidia kutokana na mashambulizi ya mwaka huu yaliyofanywa na Marekani na Israel.
Tahadhari hiyo imetolewa wakati wanamgambo wa Hamas walikabidhi mateka mwingine chini ya makubaliano hayo. Hamas imerejesha miili 12 ya mateka kati ya 28 ambayo iliahidi kuirejesha lakini imesema inahitaji muda zaidi pamoja na usaidizi wa kiufundi ili kuipata miili ya mateka iliyosalia.
Wito wa Umoja wa Mataifa kwa pande zote
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametoa wito kwa pande zote kuheshimu makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa rasmi Oktoba 10, 2025:
” Tunaridhishwa na hatua ya pande zote kuthibitisha ahadi zao za kutekeleza usitishaji vita huko Gaza na kupongeza juhudi thabiti za wapatanishi. Hata hivyo, bado tuna wasiwasi kuhusu vitendo vyote vya ghasia huko Gaza na mashambulizi yaliyoripotiwa jana. Tunaziomba pande zote kuheshimu ahadi zao zote za kuhakikisha ulinzi wa raia na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha upya uhasama na kudhoofisha operesheni za kibinadamu,” alisema Dujarric.
Mwishoni mwa juma, makubaliano hayo ya kusitisha vita Gaza yalikuwa hatarini kuvunjika wakati wanajeshi wawili wa Israel walipouawa kusini mwa Gaza, na Israel ikafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Hamas siku ya Jumapili kwa kutumia tani 153 za mabomu, hii ikiwa ni kulingana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na ambapo Wapalestina 45 waliuawa.
//AP, DPA, RTR, AFP