#HABARI: Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Frola Sangiwa, ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu ongezeko la usafirishaji haramu wa binadamu, hasa watoto kutoka nchi jirani wanaofika kwa lengo la kufanya kazi za ndani katika Wilaya ya Kahama.
Sangiwa amesema kuwa hali hiyo inachangia kwa kiwango kikubwa mmomonyoko wa maadili ya Kitanzania, kwani Watoto na Vijana hao huingia nchini kwa njia zisizo rasmi, huku wakijifunza lugha za wenyeji kama Kisukuma na Kiha ili kuficha utambulisho wao.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Kahama, Swaiba Chemchem, amesema kuwa kila baada ya kipindi cha miezi mitatu, zaidi ya Watoto 150 wamekuwa wakikamatwa wakiwa wamesafirishwa kutoka nchi jirani kama Rwanda na Burundi kwa nia ya kutumikishwa katika kazi za nyumbani.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo amesema baadhi ya Watoto hao hutumika pia kwenye mashamba ya tumbaku, jambo linalokiuka haki za Mtoto na sheria za kazi nchini.
Katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo, Mkuu wa Programu kutoka Shirika la Wote Sawa (@Wotesawatanzania), Demitila Faustine akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo , Angela Benedicto (@Angela_Benedicto), amesema kuwa shirika hilo limekuwa likipokea watoto wengi kutoka Kahama waliotumikishwa kinyume cha sheria.
Amesema kuwa Shirika hilo linaendesha kampeni ya kutokomeza ajira kwa Watoto, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kazi zenye staha na maslahi bora kwa wafanyakazi wa ndani.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania