Waendesha mashtaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamewasilisha maombi kutaka Joseph Kabila ahukumiwe adhabu ya kifo kwa makosa ya uhaini katika kesi inayomkabili mahakamani.
Jenerali Lucien René Likulia aliyemwakilisha mwendesha mashtaka aliitaka Mahakama siku ya Ijumaa, Agosti 22, 2025 pamoja na adhabu ya kifo, imuhukumu Kabila kifungo cha miaka 20 kwa madai ya kufumbia macho uhalifu wa vita na pia kifungo cha miaka 15 kwa kula njama na wahalifu.
Hata hivyo kesi ya Rais huyo wa zamani inaendelea bila ya yeye kuwepo mahakamani. Anakabiliwa na makosa ya uhainii, mauaji na ubakaji na makosa mengine ya uhalifu wa kivita.
Wafuasi wake wanasema kesi hiyo inaendeshwa kwa kutumia nguvu za kisiasa kwa ndio maana rais huyo wa zamani Joseph Kabila aliondolewa kinga ya rais mnamo mwezi Mei, 2025.
Kabila yuko wapi?
Mpaka sasa Kabila hajulikani alipo. Rais wa Kongo Felix Tshisekedi mwaka 2024 alimshutumu Kabila kwa kuwaunga mkono waasi na “kushirikiana nao katika kutayarisha uasi , madai ambayo Kabila ameyakanusha.
Chama cha Kabila cha PPRD, kinachoongozwa na Ferdinand Kambere, waziri wa zamani chini ya Kabila kimesema kufutiwa kinga rais huyo wa zaman ilikuwa ndio mwanzo wa kampenichafu dhidi yake.
Henry-Pacifique Mayala, mtafiti na mratibu wa shirika la Ufuatiliaji wa Usalama la Kivu ameliambia shirika la Habari la AP kwamba madai ya mwendesha mashtaka yanaonekana kuwa “zaidi ya kutafuta alama za ushindi kuliko kutafuta ukweli.”
Joseph Kabila aliyeiongoza Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019 alifunguliwa mashtaka tangu mwezi Julai. Serikali ya Kongo pia imedai kuwa kiongozi huyo wa zamani analiunga mkono kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
M23 ndio wanadhibiti miji miwili muhimu ya eneo la mashariki ya Goma na Bukavu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Bado haijatolewa tarehe rasmi ambapo mahakama itatoa uamuzi wa kesi hiyo.
Kabila alikuwa anaishi uhamishoni tangu mwaka 2023 hadi mwezi April, 2025 alipowasili katika mji wa Goma unaodhibitiwa na waasi baada ya mji huo kutekwa katika na waasi wa M23.
Rais huyo wa zamani alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 29 baada ya baba yake Laurent Kabila kuuwawa na alirefusha uongozi wake kwa kuchelewesha uchaguzi kwa muda wa miaka miwili baada ya muda wake kumalizika mwaka 2017.
Chanzo: AP