Waandishi watano wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya kimataifa wameuawa tarehe 25 Agosti katika mashambulizi ya Israel. Mashambulizi hayo yameikumba hospitali moja kusini mwa Ukanda wa Gaza na kusababisha vifo vya watu 20, kwa mujibu wa Shirika la Ulinzi wa Raia wa Palestina.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa shirika la huduma ya kwanza, Mahmoud Bassal, ametangaza “idadi ya vifo (…) vya watu 20, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari watano na mwanachama wa shirika la Ulinzi wa Raia wa Gaza” baada ya kuripoti mashambulizi mawili ya Israel katika Hospitali ya Nasser huko Khan Younis. Chanzo hicho hapo awali kiliripoti vifo vya watu 15, wakiwemo waandishi wa habari wanne.

Jeshi la Israel limetangaza kuwa limefungua uchunguzi kuhusu mashambulizi yaliyolenga hospitali hiyo, ambayo limekuwa ikilengwa mara kwa mara na Israel tangu kuanza kwa vita hivyo ili kuthibitisha taarifa hizo. Kwa mujibu wa Mahmoud Bassal, shambulio la kwanza limetekelezwa na ndege isiyo na rubani, likifuatiwa na mlipuko wa angani ambao umetokea wakati majeruhi wakihamishwa.

Al Jazeera imetangaza papo hapo kifo cha mmoja wa waandishi wake wa habari, Mohammad Salama, wiki mbili baada ya kupoteza waandishi wa habari wanne na wafanyakazi wawili wa kujitegemea katika shambulio la kuvizia lililotekelezwa na jeshi la Israel, ambalo lilimtuhumu mmoja wao kuwa mwanachama hai wa tawi la kijeshi la Hamas.

Shirika la habari la Canada na Uingereza Reuters limeripoti kuwa mmoja wa waandishi wa habari waliouawa na mmoja wa waliojeruhiwa ni miongoni mwa wafanyakazi wake na kusema “limsikitishwa na hali hiyo.” Kwa upande wake, shirika la habari la Marekani Associated Press (AP) limesema “limeshtushwa” na kifo cha mmoja wa wafanyakazi wake wa kujitegemea ambaye, shirika hilo limeongeza, hakuwa kwenye kazi kwa niaba ya shirika hilo wakati huo. Chama cha Waandishi wa Habari wa Palestina kimewataja wahasiriwa wengine wawili kuwa ni Moaz Abu Taha na Ahmad Abu Aziz.

Kabla ya kutangazwa kwa vifo hivyo, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) na Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF) wamehesabu karibu waandishi wa habari 200 waliouawa tangu kuanza kwa vita huko Gaza, vilivyochochewa na shambulio lisilokuwa na kifani la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

Msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Raia pia ametaja kifo cha mfanyakazi wa matibabu katika shambulio la Agosti 25. Watu kadhaa waliojeruhiwa, wengine wakiwa wametapakaa damu, walipelekwa hospitalini baada ya shambulo hilo, mpiga picha wa AFP kwenye eneo la tukio amebainisha.

“Waandishi wengi sana wameuawa huko Gaza bila ya uhalali hata kidogo”

Hospitali ya Nasser ni mojawapo ya vituo vya afya vinavyofanya kazi kwa sehemu katika Ukanda wa Gaza. Maafisa wa Shirika la Ulinzi wa Raia wamerekodi jumla ya vifo 27 kufikia mapema alasiri kufuatia risasi zilizorushwa na jeshi la Israeli au mashambulio mnamo Agosti 25 katika eneo ndogo la pwani ya Palestina, iliyoharibiwa na karibu miaka miwili ya vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *