#HABARI: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua mradi wa kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani (Children in Street Situation (CiSS) utaotekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza wenye lengo la kupunguza kuwapatia elimu, ujuzi na stadi mbalimbali kwa watoto waliokuwa wanaishi mtaani.
Waziri Dkt. Gwajima amezindua Mradi huo jijini Dar es Salaam huku akisema kuwa Serikali imechukua msimamo thabiti kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeachwa nyuma na kwamba kila mtoto, bila kujali asili au mazingira yake, anafurahia haki ya kulindwa, kutunzwa na kupata fursa ya kufikia uwezo wake kamili.
Ameongeza kuwa watoto wanaoishi katika mazingira ya mitaani wanawakilisha mojawapo ya makundi yaliyo hatarini zaidi katika jamii zetu. Kila siku wanakabiliwa na hatari zinazoweza kuathiri usalama, afya, elimu, na ustawi wao kwa ujumla hivyo mradi huo utasaidia juhudi za Serikali katika kuwanusuru watoto wanaoishi katika hayo mazingira.
“Ninapongeza Shirika la SOS Children’s Villages International na washirika wake kwa maono na kujitolea walikoonesha kupitia mradi wa CiSS. Tangu kuanzishwa kwake nchini Ethiopia mwaka 2022 na kupanuliwa hadi Tanzania na Rwanda mwaka 2023, mradi huu umeonesha jinsi uokoaji, ukarabati, urejeshaji kwa familia na ujumuishaji unaofanywa kwa uratibu unavyoweza kuleta matumaini mapya kwa watoto waliopoteza utoto wao kutokana na maisha ya mitaani.” amesema Waziri Dkt. Gwajima
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania