Chanzo cha picha, Prabhat Kumar/BBC
Mwanamke mmoja kutoka India amegunduliwa na ujauzito katika ini lake badala ya mfuko wa uzazi.
Hii ndiyo sababu Sarvesh mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa kijiji cha Dastura katika wilaya ya Bulandshahr huko Uttar Pradesh , amekuwa kitovu cha uangalizi wa madaktari na watafiti wengi wakuu hivi majuzi.
Mbali na raia, wataalam pia wanataka kujua jinsi hili lilivyotendeka na ni ipi hali ya Sarvesh kwa sasa.
Nilifika kijiji cha Dastura ili kupata majibu ya maswali hayo.
Tulipofika nyumbani kwa Sarvesh, alikutwa amelala kwenye kitanda. Mkanda mpana sana ulikuwa umefungwa tumboni mwake na ilikuwa vigumu kwake hata kuugeuka.
Sarvesh aliambia BBC, “Nilikuwa nikitapika sana. Siku zote nilikuwa nimechoka na maumivu. Ilikuwa vigumu kuelewa kilichokuwa kinanipata.”
Anasema hali yake ilipoanza kuzorota, daktari alimtaka aafnayiwa ukaguzi wa kimatibabu.
Lakini ripoti ya ultrasound haikufichua chochote na aliendelea kutumia dawa za maambukizi ya tumbo.
Lakini wakati afya yake iliendelea kuzorota hata baada ya mwezi mmoja wa kunywa dawa, alienda tena kwa uchunguzi wa ultrasound.
Wakati huu, jambo lililojitokeza katika ripoti hiyo lilikuwa nadra sana hata madaktari walikuwa wakipata shida kuamini.
Chanzo cha picha, Prabhat Kumar/BBC
“Kuna mtoto kwenye ini lako”
Dkt. Sania Zehra, ambaye alifanya uchunguzi wa ultrasound, alimwambia Sarvesh kwamba kulikuwa na mtoto kwenye ini lake. Hii ilikuwa hali ya kutatanisha kwa Sarvesh na mumewe Paramveer.
Ili kuthibitisha, alitoka eneo la Bulandshahr hadi Meerut ili kufanyiwa uchunguzi wa ultrasound na MRI kwa mara nyingine tena. Ripoti ilionyesha tena kitu kimoja.
Ilikuwa vigumu kwa Sarvesh kuamini ripoti hii kwa sababu mzunguko wake wa hedhi ulikuwa wa kawaida.
Dkt. KK Gupta, mtaalamu wa radiolojia aliyemfanyia MRI, aliambia BBC kwamba hajawahi kuona kisa kama hicho katika maisha yake ya miaka 20.
Kabla ya kufikia uamuzi wowote, alichunguza ripoti hiyo mara kadhaa na kumuuliza tena na tena mwanamke huyo ikiwa hedhi zake zilikuwa za kawaida au la.
Anasema, “Mwanamke huyo alikuwa na ujauzito wa wiki 12 kwenye tundu la kulia la ini, ambapo mapigo ya moyo yalionekana pia kwa uwazi. Hali hii inaitwa intrahepatic ectopic pregnancy, ambayo ni nadra.
Katika hali hiyo, wanawake huvuja damu nyingi, ambayo huona kuwa ni hedhi ya kawaida na inachukua muda kugundua ujauzito.”
Chanzo cha picha, Prabhat Kumar/BBC
Hakuna chaguo jingine zaidi ya upasuaji
Chanzo cha picha, Prabhat Kumar/BBC
Daktari aliwaambia wanandoa kwamba ikiwa kijusi ni kikubwa, kuna hatari ya ini kupasuka. Katika hali hii, mtoto na mama wote watapoteza maisha. Kwa hiyo, hakuna chaguo jingine isipokuwa upasuaji.
Paramveer anasema kwamba hakuna daktari huko Bulandshahr aliyekuwa tayari kushughulikia kesi hii. Pia alienda Meerut, lakini alikatishwa tamaa.
Madaktari wanasema kuwa hii ilikuwa kesi ngumu na maisha ya mama na mtoto yalikuwa hatarini na kila mtu alishauri waende mjini Delhi.
Sarvesh alisema, “Sisi ni maskini na haikuwezekana kwetu kwenda Delhi na kubeba gharama hiyo. Baada ya kufanya duru kadhaa, tuliamua kwamba tutapata matibabu hapa.”
Hatimaye, timu ya madaktari katika hospitali ya kibinafsi huko Meerut ilikubali kumfanyia upasuaji Sarvesh.
Chanzo cha picha, Prabhat Kumar/BBC
Parul Dahiya, ambaye alikuwa sehemu ya timu ya madaktari, anasema, “Mgonjwa alipokuja kwangu, alikuwa akiteseka kwa muda wa miezi mitatu.
Alikuwa na ripoti za ultrasonography na MRI, ambayo ilionyesha wazi kwamba ilikuwa mimba ya ectopic ya intrahepatic.
Tulizungumza na daktari mkuu wa upasuaji Dkt. Sunil Kanwal kuhusu kesi hii, kwa sababu katika kesi hiyo unahitajika pia baada ya upasuaji.
Kulingana na madaktari, upasuaji huu ulidumu kwa saa moja na nusu.
Dkt. KK Gupta pia alionyesha BBC video ya upasuaji huo na picha za kijusi hicho.
Je, ujauzito wa intrahepatic ni nini?
Kwa kawaida mwanamke huwa mjamzito wakati yai lililotolewa kutoka kwenye ovari linaporutubishwa na manii.
Yai hili lililorutubishwa husogea kuelekea kwenye mfuko wa uzazi kupitia mrija wa fallopian na kisha kiinitete hukua kwenye uterasi yenyewe.
Dkt. Mamta, Profesa wa Taasisi ya Sayansi ya Tiba, BHU, anasema wakati mwingine, badala ya kufika kwenye mfuko wa uzazi, yai lililorutubishwa hubaki kwenye mrija wa fallopian au kushika uso wa kiungo kingine.
Kwa mfano, katika tukio hili yai lilikwama kwenye ini. Ini ina ugavi mzuri wa damu, hivyo hufanyakazi kama ‘ardhi yenye rutuba’ kwa kiinitete katika siku za mwanzo.
Lakini baada ya muda fulani hali ya hatari hutokea kwa mama na mtoto, ambapo hakuna njia nyingine iliyobaki isipokuwa upasuaji.
Ni visa vingapi kama hivyo vilivyoripotiwa nchini India hadi sasa?
Je, ujauzito usio wa kawaida wa intrahepatic hutokea kwa kiasi gani?
Ili kuelewa hili, tulizungumza na Dkt. Monica Anant, Profesa wa Idara ya Uzazi na katika Patna AIIMS.
Kwa mujibu wa Dkt. Monica, kwa wastani asilimia moja ya kesi za mimba ndani ya tumbo huripotiwa duniani kote na katika hili mimba haitokei kwenye uterasi.
Alisema, “Kulingana na makadirio, kesi moja kati ya laki 70 hadi 80 ya ujauzito inaweza kuwa ya intrahepatic.”
Dkt. Monica anasema kabla ya kisa hicho cha sasa, visa 45 vya mimba ndani ya tumbo viliripotiwa kote duniani, kati ya watu hao watatu walitoka India.
Kesi ya kwanza iliripotiwa katika Chuo cha Madaktari cha Lady Hardinge huko Delhi mwaka wa 2012.
Halafu mwaka 2022, kesi ya tatu ilibainika katika Chuo cha Matibabu cha Goa na mwaka wa 2023 huko Patna AIIMS.
Kesi ya Patna AIIMS iligunduliwa na Dkt. Monica Anant na timu yake wenyewe.
Katika kesi hiyo, timu yake ilijaribu kuua yai la mwanamke kwa msaada wa dawa (methotrexate). Kisha wakaendelea kumfuatilia mgonjwa kwa muda wa mwaka mzima.
Baadaye Dkt Monica aliandika ugunduzi wake adimu na akauchapisha katika PubMed kama mimba ya tatu ya intrahepatic ectopic nchini India.
PubMed ni hifadhidata inayoongoza kwa utafiti wa matibabu nchini Marekani.
Dkt. Parul Dahiya na Dkt. KK Gupta wanasema kwamba timu yao pia imeanza kuandika ugunduzi wao.
Hivi karibuni itakamilika na kutumwa kwa uchapishaji katika jarida la matibabu linaloheshimiwa.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla