Chanzo cha picha, ACT
Hatma ya mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, ipo njia panda baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutangaza kuwa uteuzi wake haujakidhi matakwa ya kikanuni, kufuatia pingamizi lililowasilishwa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.
Katika uamuzi uliotolewa leo, Msajili alibainisha kuwa Mpina hakutimiza vigezo vya uanachama kwa mujibu wa kanuni za chama, akisema kuwa alijiunga ACT-Wazalendo nje ya muda uliopangwa na hivyo hakustahili kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Hata hivyo, uongozi wa ACT-Wazalendo kupitia Katibu Mkuu, Ado Shaibu, umetangaza kutopokea uamuzi huo na kueleza kuwa tayari wameanza mchakato wa kufungua kesi Mahakama Kuu ili kupinga hatua ya Msajili, wakidai imekiuka taratibu na kuingilia mchakato wa ndani wa chama.
“Chama cha ACT Wazalendo kinaweka msimamo kuwa hakitofuata maelekezo ya Msajili wa Vyama vya siasa juu ya suala hili” inasema taarifa ya ACT na kuongeza kuwa katika kesi itakayofungua itaweka zuio dhidi ya utekelezaji wa uamuzi huu hadi kesi ya msingiisikilizwe.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), uteuzi rasmi wa wagombea urais unatarajiwa kufanyika Jumatano August 27, 2025 kuanzia saa 1:30 asubuhi mpaka saa 10 Alasiri, jambo linaloweka mustakabali wa Mpina katika kinyang’anyiro hicho kwenye mizani ya kisheria na kisiasa.
Wataalamu wa sheria wameeleza kuwa hata kama Tume itakubaliana na maamuzi ya Msajili, Mgombea huyo bado ana nafasi ya kwenda Mahakamani kuomba zuio la utekelezaji wa uamuzi wa Msajili pamoja na Tume hadi pale shauri la msingi litakaposikilizwa.