-
- Author, Tessa Wong
- Nafasi, BBC
Ilikuwa ni Ijumaa nyingine asubuhi kwenye kisiwa cha Taiwan cha Kinmen, kilomita chache kutoka pwani ya China, wakati king’ora cha mashambulizi ya anga kilipolia.
Katika ofisi ya serikali ya mtaa, watu walizima taa na kujitia chini ya meza. Wengine walikimbilia kwenye maegesho ya magari ya chini ya ardhi. Katika hospitali ya karibu, wafanyakazi walikimbia kuwatibu watu waliokuwa na majeraha na damu.
Lakini damu hiyo ilikuwa ya uwongo, na waliojeruhiwa walikuwa waigizaji wa kujitolea. Walikuwa wakishiriki katika mazoezi ya lazima ya ulinzi wa raia yaliyofanyika kote Taiwan mwezi uliopita.
Ni mazoezi ya kujiandaa na shambulio linaloweza kufanywa na China.
China kwa muda mrefu imeapa kuwa itaiunganisha Taiwan inayojitawala yenyewe na China bara na haijaondoa uwezekano wa kufanikisha hilo kwa matumizi ya nguvu. Ni tishio ambalo Taiwan inazidi kulichukua kwa uzito.
“Tunahitaji mazoezi haya ya ulinzi, naamini kuna tishio kutoka China,” anasema Ben, mtaalamu wa fedha anayefanya kazi Taipei. “Lakini uwezekano wa uvamizi huo ni mdogo. Kama kweli wanataka kutushambulia, wangefanya hivyo tayari.”
Kama Ben, watu wengi nchini Taiwan – 65% kulingana na uchunguzi uliotolewa Mei na Taasisi ya Kitaifa ya Ulinzi na Utafiti wa Kimkakati (INDSR) – wanaamini hakuna uwezekano wa China kuishambulia Taiwan katika miaka mitano ijayo.
Licha ya onyo la Marekani kwamba tishio kwa Taiwan “limekaribia” na Beijing inatayarisha jeshi lake kuwa na uwezo wa kuivamia Taiwan ifikapo 2027.
Maandalizi ya kijeshi
Rais William Lai wa Taiwan, na serikali yake mara nyingi hurudia msemo huu: “Kwa kujitayarisha kwa vita, tunaepuka vita.” Wanasisitiza kuwa hawataki migogoro bali wanatumia haki ya Taiwan kujenga ulinzi wake.
Pamoja na kuanzisha mageuzi makubwa ya kijeshi, pia wanataka kuongeza matumizi ya ulinzi kwa 23% mwaka ujao hadi NT$949.5bn (£23bn; $31bn), itakuwa zaidi ya 3% ya Pato lao la Taifa, kufuatia shinikizo la Marekani kuwekeza zaidi katika ulinzi. Lai ameahidi kuiongeza matumizi hayo hadi 5% ifikapo 2030.
Mbali na hayo pia imepanua mafunzo ya kijeshi ya lazima kwa raia wake, pia imeongeza malipo na manufaa kwa wanajeshi, na kuanzisha mafunzo makali zaidi.
Hatua hizi zinalenga kushughulikia tatizo la uhaba wa wanajeshi na kupandisha ari iliyoshuka – askari hapo awali walilalamikia kuhusu mafunzo duni.
Mazoezi ya kila mwaka ya vita ya Han Kuang, ambayo hufanyika kujibu mashambulizi ya kijeshi ya China, yameboreshwa ili kuchukua nafasi ya mazoezi ya maandishi na kuyafanya ya kweli zaidi.
Mazoezi ya mwaka huu yalidumu muda mrefu zaidi kuwahi kutokea, huku wanajeshi 22,000 wa akiba wakishiriki, takriban 50% zaidi ya mwaka jana. Kando na kujiandaa na vita na mapambano dhidi ya habari za uongo, lengo moja kuu lilikuwa kujiandaa kwa vita vya mijini.
Wanajeshi walifanya mazoezi ya vita katika miji. Huko Taipei, walifanya mazoezi ya kupakia makombora kwenye helikopta za kushambulia, na kubadilisha shule kuwa kituo cha kutengeneza mizinga ya vita.
Kwa siku kadhaa, maeneo makuu ya mijini kote Taiwan, yalichukua zamu kufanya mazoezi dhidi ya uvamizi wa anga. Wakaazi katika wilaya zilizoteuliwa walilazimika kuingia ndani, huku hoteli, maduka na mikahawa ikilazimika kusitisha biashara. Abiria hawakuweza kupanda au kushuka treni na ndege. Mtu yeyote aliyenaswa kukiuka mazoezi, alikuwa hatarini kupigwa faini.
Katika jiji la Taipei, timu za watoa huduma wa dharura na watu waliojitolea walifanya mazoezi ya kuwahamisha watu waliojeruhiwa, kuzima moto, na kuwashusha chini ya majengo ambayo yalikuwa yamepambwa kuonekana kana kwamba yamepigwa na makombora.
Kisiwa hicho kidogo, ambacho kilishuhudia mapigano makali kati ya vikosi vya China na Taiwan mwishoni mwa miaka ya 1940 na 50, kinachukuliwa kuwa mstari wa mbele wa shambulio lolote la China.
Matumaini ya Taiwan
Lakini kutokana na kuboreshwa kwa uhusiano wa kiuchumi, watu wengi wa kisiwa cha Kinmen wanaona ukaribu wao na China kama neema, na sio tatizo.
Sehemu kubwa ya uchumi wa Kinmen sasa unawahudumia watalii wa China ambao husafiri katika feri kupitia njia nyembamba ya maji kutoka Xiamen, jiji la karibu la China.
Jambo lingine ambalo linawapa moyo WaTaiwani kwa muda mrefu ni kwamba Marekani ina wajibu kisheria kulinda usalama wa Taiwan. Ingawa kura za maoni zinaonyesha uhakikisho huo umepungua wakati wa utawala wa sasa wa Rais Donald Trump, lakini wengine bado wanaamini Marekani itaisaidia Taiwan katika tukio la shambulio – na China inasita kuingia katika mzozo wa moja kwa moja wa kijeshi na Marekani.
Pia kuna imani kwamba jumuiya ya kimataifa itaisaidia Taiwan kutokana na umuhimu wake katika uzalishaji wa chipu kimataifa.
“Baada ya kutoa vitisho vya miongo kadhaa, pia kuna hisia kwamba Beijing inatoa vitisho hewa,” anasema Wen-ti Sung, mtaalamu wa siasa katika Kituo cha Taiwan.
China haijawahi kuthibitisha madai ya Marekani kwamba inatayarisha jeshi lake kuivamia Taiwan ifikapo mwaka 2027. Lakini imekuwa ikiimarisha jeshi lake, hasa jeshi la wanamaji na silaha zake, ambazo zitaonyeshwa katika gwaride la mwezi ujao.
Wataalam wamegawanyika ikiwa China itafanya uvamizi au la. Lakini wengi wanakubali kwamba mivutano hiyo, pamoja na hatua za kijeshi za China, huongeza uwezekano wa makabiliano.
China imeanza kushambulia?
Chanzo cha picha, Ritchie B Tongo / EPA/Shutterstock
Kuna njia nyingi ambazo China inaweza kushambulia. Kando na mashambulizi kwenye fukwe za Taiwan au kurusha makombora, inaweza pia kuweka vizuizi vya anga na baharini, au kukata nyaya za mawasiliano chini ya bahari.
Lakini serikali ya Taiwan, inaamini uvamizi wa hila unaweza kuwa tayari unafanyika; ambapo China inajaribu kushinda mioyo na akili za WaTaiwani wa kawaida kwa matumaini kwamba siku moja watachagua kuungana.
Kwa njia rasmi China imekuwa ikihimiza uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na Taiwan, pamoja na uhusiano wa kitamaduni.
Kwa njia isiyo rasmi, kulingana na wachambuzi na maafisa wa Taiwan, Beijing pia imewekeza katika kampeni za upotoshaji na kuongeza ushawishi.
Utafiti mmoja uliofanywa na Taasisi ya V-Dem ya Chuo Kikuu cha Gothenberg cha Sweden uligundua kuwa kwa miaka mingi, Taiwan imekuwa sehemu inayolengwa zaidi ulimwenguni kwa kampeni za taarifa zilizoanzishwa na serikali ya kigeni.
Mwezi Machi, Lai alionya juu ya kuongezeka kwa ushawishi wa China katika uchumi wa Taiwan, utamaduni, vyombo vya habari, na hata serikali, na kutangaza hatua kadhaa za kuimarisha usalama.
Wanajeshi kadhaa na maafisa wa kijeshi wa Taiwan wamefungwa kwa madai ya kufanya ujasusi kwa niaba ya China. Wanachama wa DPP – ikiwa ni pamoja na msaidizi wa zamani wa Lai – pia wameshtakiwa kwa ujasusi.
Wakati huo huo, watu mashuhuri wa Taiwan wanaoipenda China, washawishi wa mitandao ya kijamii na wana ndoa kutoka China wenye uraia wa Taiwan wamechunguzwa, na wengine kufukuzwa au kulazimishwa kuondoka.
Lai pia ameunga mkono vuguvugu lenye utata linalolenga kuwafukuza wanasiasa wa upinzani wanaochukuliwa kuwa karibu na China.
Kura za maoni zinaonyesha mara kwa mara kwamba watu wengi wa Taiwan wanataka “hali ya sasa ibaki,” kumaanisha kuwa hawataki kuungana na China, wala kutangaza uhuru rasmi.
Lakini Chama cha upinzani chama cha Kuomintang (KMT), kinaishutumu serikali ya chama tawala cha DPP kwa kutumia uvamizi wa China, kuogopesha watu ili kupata uungwaji mkono wa kisiasa.