Chanzo cha picha, AFP
-
- Author, Yusuph Mazimu
- Nafasi,
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa sasa ni uwanja wa mateso, hofu, na umwagaji damu unaoendelea bila kikomo.
Katika mazingira ya mizozo ya muda mrefu, vikundi vya waasi wenye silaha kama ADF (Allied Democratic Forces) na M23, vinahusishwa moja kwa moja na mauaji ya halaiki, hasa dhidi ya Wakristo.
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Bunge la Ulaya (3 Aprili 2025), wakristo wamekuwa wakilengwa kwa makusudi kwa kushambuliwa, kuuawa, kutekwa na makanisa yao kuvunjwa au kuchomwa moto.
Usiku wa Jumapili ya Julai 27, 2025, wakristo 43 waliokusanyika katika ibada ya usiku katika kanisa katoliki lililoko Komanda, mkoa wa Ituri Mashariki mwa DRC. Wakiwa katika maombi ya amani, waumini hao waliuawa kikatili kwa risasi, mapanga na kuchomwa moto na waasi wa kundi la ADF linalohusishwa na ISIS.
Kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO) na mashirika ya kimataifa kama Al Jazeera, DW na Vatican News, tukio hilo lilithibitishwa kuwa ni shambulio la kuwalenga wakristo waliokuwa kwenye misa ya usiku.
ISIL (ISIS) walikiri kuhusika kupitia mtandao wao wa Telegram, wakisema walitekeleza “mauaji ya ibada” na kuchoma maduka na nyumba kadhaa zilizokuwa karibu na kanisa hilo.
“Walivamia ghafla usiku na kuanza kuwachinja watu kanisani,” alisema Christophe Munyanderu, mwanaharakati wa haki za binadamu aliyeshuhudia tukio hilo.
“Waumini waliokuwa wamelala ndani ya kanisa hawakuwa na pa kukimbilia.”
‘Utiriri’ wa Mashambulizi dhidi ya wakristo Makanisani
Tukio la Komanda sio la kwanza. Julai 11, 2025, kulifanyika mashambulizi ya ADF katika eneo la Irumu, karibu na mpaka wa Uganda, yaliwaua watu 66, wengi wao wakiwa Wakristo waliokuwa kanisani wakisali.
Machi 2025, zaidi ya waumini 70 walikutwa wameuawa ndani ya kanisa la Kipentekoste karibu na mji wa Lubero, Kivu Kaskazini, wakiwa wamefungwa mikono, baadhi wakikatwa vichwa. Shirika la Aid to the Church in Need (ACN) lilithibitisha na kusema tukio hilo lilitekelezwa na ADF.
Januari 2024, ADF walivamia Kanisa la Kipentekoste huko Beni na kuua watu 8 waliokuwa katika ibada. Mei 2024, Wakristo 14 waliuawa kwa kukataa kubadili dini katika eneo la North Kivu; wengine 11 wakateketezwa Ituri.
Mbali na ADF, kundi la M23 nalo linachangia hali ya sintofahamu na mauaji. Bunge la Ulaya limeitaja Rwanda kuwa mdhamini wa kundi la M23, ambalo hivi karibuni liliikalia kijeshi miji yenye utajiri wa madini kama Walikale. Hali hii imepunguza nguvu za oparesheni ya pamoja ya kijeshi (Operation Shujaa) kati ya DRC na Uganda inayolenga kupambana na ADF.
ADF yanyooshewa vidole kwa vita ya kidini Mashariki mwa DRC
Chanzo cha picha, AL JAZEERA
ADF, kundi la waasi lenye chimbuko kutoka Uganda, limekuwa likihusishwa na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia kwa zaidi ya miaka 20. Kwa mujibu wa Kanisa Katoliki la DRC, na pia ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ya Mei 2024, ADF imejikita hata katika magereza ya Kinshasa kwa ajili ya kusambaza itikadi kali, kuwashawishi au kuwalazimisha vijana kujiunga kwa kutumia hongo au vitisho.
Kwa mujibu wa azimio la Bunge la Ulaya la tarehe 3 Aprili 2025, ADF imebadilika kutoka kundi la waasi wa Uganda kuwa kikundi cha kigaidi chenye itikadi kali ya kidini, kinachotumia dini kama silaha. Tangu 2019, kiongozi wa ADF aliapa utiifu kwa ISIS na kundi hilo likawa tawi rasmi la ISIS Central Africa Province (ISCAP).
Lengo lao halipo tu kwenye ardhi ya DRC, bali pia ni kuanzisha dola la Kiislamu kali Mashariki mwa Afrika, wakitumia mateso, mauaji na propaganda za kidini kuvuruga maelewano ya kijamii na kueneza chuki ya kidini. ADF wamekuwa wakilenga Wakristo kwa makusudi, hasa wanapokuwa katika ibada.
Tangu kiongozi wao atangaze utiifu kwa ISIS mwaka 2019, kundi hili limejiimarisha kama tawi la IS Central Africa Province (ISCAP) na limekuwa likilenga Wakristo kwa misingi ya kidini. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya 6,000 waliuawa huko Beni kati ya 2013 na 2021, huku zaidi ya 2,000 wakipoteza maisha huko Bunia mwaka 2020 pekee wengi wao wakiwa Wakristo.
Jumuiya ya Kimataifa inasema nini kuhusu mauaji haya?
Chanzo cha picha, Getty Images
Haya si mashambulizi ya kivita ya kawaida, bali ni juhudi ya kisayansi ya kuwatokomeza watu kwa misingi ya imani yao. Dunia hailazimiki tu kukemea bali kuchukua hatua.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV alituma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa Komanda na kufanya maombi na sala maalumu kwa ajili yao. Papa amesikitishwa na mauaji hayo huku akiyalaani.
Baraza la Maaskofu wa DRC (CENCO) lilionya kuhusu “mpango wa muda mrefu wa kuislimisha kanda hiyo” kwa nguvu na hila.
Bunge la Ulaya kwa upande wake lilitaka uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kuwekewa vikwazo kwa wahusika, na kuundwa kwa Mahakama maalum ya kimataifa kwa ajili ya uhalifu wa kivita na mauaji ya kidini nchini DRC.
Wakati ADF wanaendesha mashambulizi kwa misingi ya kidini, kundi la M23 lenye uhusiano na Serikali ya Rwanda linadaiwa kuchochea mzozo zaidi kwa kulenga raia na kuzuia oparesheni za pamoja dhidi ya ADF. Bunge la Ulaya lilitaja Rwanda kama mfadhili wa M23, na kutoa wito kwa Rwanda kuondoa wanajeshi wake kutoka ardhi ya DRC.