-
- Author, Florian Kaijage
- Nafasi,
Julai 13, 2025 aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchni Cuba, Humphrey Polepole alitangaa kujiuzulu nafasi hiyo na nafasi nyingine za utumishi umma Jumapili akitaja sababu kadhaa za kufikia uamuzi huo ambao haukutarajiwa na wengi.
Sababu kuu alizotaja ni ukiukwaji wa taratibu za chama cha CCM, kupinga matendo ya utekaji wa watu na utendaji wa serikali. Yote hayo aliyafafanua kwa kina siku tano baadaye Ijumaa Julai 18, 2025 wakati wa taarifa mubashara kupitia mtandao wa Facebook.
Na ameendelea kuelezea anachoamini kuwa ‘mambo kwenda mrama’ kwenye chama, alipohojiwa na mwanahabari mkongwe na mwanasheria aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa serikalini, Jenerali Twaha Ulimwengu.
Ushahidi wa uamuzi na tangazo la kujiuzulu kwa Polepole kuwashtua watu wengi ni machapisho kwenye mitandao ya kijamii kuelezea kuwa tangazo lililokuwa kwenye barua ya Polepole kwenda kwa Mwenyekiti wa chama chake na Rais wa nchi Samia Suluhu Hassan halikuwa la kweli, kiasi kwamba Polepole mwenyewe aliamua kuwajibu moja kwa moja mitandaoni kuwa barua ile ilikuwa ni ya kwake.
Kulikuwa pia na jitihada za makusudi mtandaoni kuchapisha taarifa katika mfumo wa habari, kuwa tangazo la Polepole lilikuwa ghushi, kumbe walioliita tangazo ghushi ndiyo walikuwa wameandaa taarifa ghushi, japo walionekana kufanya kazi hiyo kwa haraka, hivyo kukosa utulivu na umakini katika kutekeleza malengo yao ambayo wanayafahamu vema wao wenyewe.
Polepole akaibua mjadala ama gumzo katika uga wa kisiasa na kijamii Tanzania mithili ya moto wa nyika majira ya kiangazi.
Wapo waliombeza, wapo waliomkejeli wapo waliomtukana na hata kumbagaza hadi kuitwa msaliti, kwa sababu tu ya kutofautiana nao katika msimamo, hoja, na fikira kuhusu hali ya kisiasa Tanzania na utendaji wa serikali na chama tawala.
Chanzo cha picha, Daily News
Wakati fulani Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kusema kuwa “watu wawili wakibishana kwelikweli kisha wakakubaliana, ni dhahiri kuwa mmoja wao alikuwa hafikirii vizuri”.
Hii inamaanisha kuwa na misimamo tofauti ni jambo la kawaida tena mara nyingi lenye afya na kusababisha kurekebisha masuala muhimu yanayokwenda kombo. Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliwahi kusema “hoja haipigwi rungu bali inajibiwa kwa hoja nzito zaidi. Waziri Mkuu wa Idia, Indira Gandhi aliyeuawa mwaka 1984 wakati mmoja alisema kwa lugha ya Kiingereza: The power to question is the basis of all human progress, kwamba, nguvu ya kuhoji ni msingi wa maendeleo kwa binadamu wote.
Wakati wa mahojiano maalum na BBC Machi 2022, Rais Samia alisema kwa lugha ya Kiingereza, let them offload kwamba kwa muktadha huo waache watoe ya moyoni. Kauli hiyo ilimpatia sifa hususan miongoni mwa watu wanaopendelea na kuamini katika uhuru wa mawazo na kujieleza, japo kwa vyovyote vile haikuwafurahisha wanaopendela kuminywa kwa uhuru huo. Ni dhahiri wapo wanaojiuliza ni upi mustakabali wa Polepole na si kujiuliza tu bali kutamani mustakabli huo uwe hasi, kama vile yaliyomkuta Mbunge wa Kawe Dar es Salaam pia mchungaji, Josephat Gwajima ambaye alikemea utekaji wa watu kisha kupata msukosuko kanisa lake kufungwa na mwenyekiti wa CCM, Samia kusema Ma-gwajima waachwe nje.
Polepole ana mapungufu yake tena makubwa ikiwemo kutetea masuala tata wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli, wakati huo akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, kama vile utekaji wa watu, watuhumiwa kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu, ‘uporaji’ wa fedha za watu kwenye amana za benki, kesi za uhujumu uchumi, kukandamizi uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2029 na Uchaguzi Mkuu 2020. Lakini anayoyasema sasa yana mashiko na mantiki? Je ni uongo? Mbwa mzembe aliyeshindwa kuwinda hapo awali hata kuzidiwa mbio na sungura, ni sahihi kuendelea kumhukumu kwa makosa ya awali hata anapokamata mnyama mwenye kasi mithili ngili? Bila shaka hapa panahitaji tafakuri ya kina.
Sasa tunapongojea mustakabali wa Polepole, tuangazie baadhi ya vigogo walioonja shubiri baada ya kuonesha mawazo tofauti au kutoridhika na namna ya uendeshaji wa mambo ndani ya serikasli na chamani CCM.
Maalim Seif Sharif Hamad
Chanzo cha picha, EA
Ukipenda waweza kumuita mwamba wa Pemba, pia nembo ya upinzani Zanzibar. Alifariki dunia Februari 17, 2021 baada ya miongo mingi ya kuendesha hoja kinzani ndani ya CCM na baadaye kuwa miongoni mwa waasisi wa chama cha upinzani cha Civic United Frobt (CUF) mwanzoni mwa miaka ya 1990. Alipitia misukosuko mingi. Mwaka 1985 baada ya Ali Hassan Mwinyi kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM wa urais wa Muungano na hatimaye kushinda, kulikuwa na ushindani wa aina yake kati ya Maalim Seif na Idris Abdul Wakil, aliyefariki dunia Machi 15, 2000. Kwa mara ya kwanza CCM ikiongozwa na mwenyekiti Mwalimu Julius Nyerere iliamua Zanzibar ipeleke Dodoma majina zaidi ya moja ya wagombea wa urais. Hii ilitokana na ushindani mkali kati ya Maalim Seif na Wakil, hivyo ikaonekana kupeleleka jina moja ingehatarisha amani na mshikamano wa Zanzibar.
Katika Kura zilizopigwa Halmashauri Kuu ya CCM, Wakil alimshinda Maalim Seif kwa kura chache. Maalim Seif aliamini kulikuwa na mizengwe iliyosababisha kushindwa kwake. ‘Wakubwa’ wa CCM na serikali akiwemo mkubwa wa wote, Mwalimu Nyerere walishauri Rais mpya wa Zanzibar, Wakil (aliyeshinda kwa chini ya asilimia 61 akiwa mgombea pekee na kupigiwa kura za ndiyo au hapana), amteue Maalif Seif kuwa Waziri Kiongozi na Wakil akatekeleza. Hata hivyo, kulikuwa na mazonge mengi serikalini kutokana na Maalim Seif kutokuwa mtiifu ipasavyo kwa Rais Wakil. Haya yameelezwa bayana na mzee Mwinyi katika kitabu chake cha Safari ya Maisha Yangu.
Kutokana na hali hiyo na kile kilichoitwa machafuko ya hali ya hewa kisiwani Pemba, ikiwemo baadhi ya majengo ya serikali na ya CCM kuchomwa moto, mwaka 1988 Kamati Kuu ya CCM ilimfukuza unachama Maalim Seif pamoja na wenzake sita, akiwemo Hamad Rashid Mohamed. Pia Maalim aliwekwa kizuizini kwa takribani miaka mitatu, na alipoachiwa huru aliiibukia kwenye vuguvugu la siasa za vyama vingi na hatimaye mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa kisheria Julai mosi 1992.
Maalim Seif alidai hakuwahi kushindwa uchaguzi kihalalai. Japo kukbukumbu rasmi zinaonesha alishindwa 1995, 2000, (ulipofutwa uchaguzi katika majimbo kadhaa na uliporudiwa CUF wakapiga kilichoitwa ‘kura za Maruhan’), 2005, 2010, 2015 (Uchaguzi uliofutwa na kufanyika wa marudio Machi 2016 uliosusiwa na CUF) na 2020 kupitia ACT Wazalendo baada ya mgogoro mkubwa ndani ya CUF.
Augustine Mrema
Chanzo cha picha, EA
Alivuma mno mwanzoni mwa miaka ya 1990 akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alikuwa na utaratibu binafsi wa kiutendaji uliomuongezea umaarufu, nyota yake ikang’ara mno, hadi Rais Mwinyi kumteua kuwa Naibu Waziri Mkuu wakati huo akiwa mtu pili katika historiua ya Tanzania kushika wadhifa huo usio wa kikatiba baada ya Salim Ahmed Salim.
Alitembelea vituo vya polisi na maeneo tofauti hata nyakati za usiku kuhakiki utendaji wa polisi, alikua mkali kama pilipili kiasi kwamba baadhi ya watu waliokuwa na ukali wa aina hiyo waliitwa Mrema. Alijipatia sifa kemkem kwa kupambana na migogoro mbalimbali ya kijamii kama vile mgogoro wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Arumeru ambako makumi ya watu walikuwa wakijeruhiwa na kutishia amani ya eneo hilo.
Alishughulikia mizozo hadi ngazi ya famili kiasi cha kuwaita ofisini kwake wanafamilia hususan wanaume ‘wakorofi’ waliowanyanyasa wake zao au kutelekeza familia. Aliweka utaratibu wa watu wa kawaida kufika ofisini kwake kuwasilisha kero au malalamiko yao, hakika alivuma.
Mwanzoni mwa mwaka 1995 Mrema aliushangaza umma alipotangaza kujitoa CCM na kujiuzulu uwaziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, nafasi aliyokuwa ameteuliwa Desemba 7, 1994 wakati wa mababadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Mwinyi. Katika Mkutano na Waandishi wa habari alilalamika kuwa aliondolewa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kumnyamazisha na kufifisha jitihada zake za kupambana na rushwa, magendo na utoroshwaji wa rasilimali za Tanzania nje ya nchi kama vile dhahabu.
Baadaye Mrema aligombea urais kupitia chama cha NCCR-Mageuzi lakini alishindwa na mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa aliyepata asilimia 61.82 ya kura huku Mrema akipata asilimia 27.77. Hata hivyo, katika uchaguzi huo wa 1995, NCCR ilipata wabunge wa majimbo zaidi ya 15 ya Tanzania Bara yakiwemo ya Arusha Mjini, Ubungo, Mbeya Mjini, Iringa Mjini, Muleba Kaskazini, Moshi Mjini, Hai, Siha, Vunjo, Urambo, Rorya, Mwibara, Bunda na Musoma Vijijini.
Mzee Mwinyi alitanabaisha katika kitabu chake kuwa alimwamini Mrema kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi, lakini kumbe yeye (Mrema) alikuwa na mipango yake ya kugombea urais.
Mivutano ndani ya NCCR-Mageuzi ilisababisha Mrema kujiondoa na kujiunga na na chama cha Tanzania Labour Party (TLP) alichokiasisi lakini umaarufu wake ulipungua kadiri miaka ilivyosonga na hata alipogombea urais miaka iliyofuata, kura zake zilizidi kupungua kulinganisha na 1995. Alifariki dunia Agosti 21, 2022.
Edward Lowassa
Chanzo cha picha, Nip
Lowassa ni Waziri Mkuu wa Tanzania ambaye ukimuacha Mwalimu Nyerere aliyeshika wadhifa huo baada ya Uhuru wa Tanganyika 1961 hadi 1962, aliyedumu kwa muda mfupi zaidi wa miaka miwili, mwezi mmoja na siku 8, kuanzia Desemba 30, 2005 hadi Februari 7, 2008 alipojiuzulu kutokana na tuhuma za kuhusika katika kashfa ya Richmond. Richmond ni kashfa iliyolikumba Taifa kutokana na Wizara ya Nishati na Madini wakati huo, kamati ya wataalamu na kwa msukumo wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuipa zabuni kampuni ya Richmond ya Houston Texas Marekani mwaka 2006, kufua umeme wa dharura.
Baadaye iliibainika kuwa kampuni hiyo ilikuwa haina uwezo kabisa hata wa kufunga kishikio ya taa (lamp holder), hii ni kwa mujibu Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza na kuongozwa na aliyekuwa mbunge wa Kyela, Dr. Harrison Mwakyembe. Lowassa alilalamika sana kwamba hakutendewa haki kwani Kamati ya Mwakyembe haikumpa nafasi ya kutoa maelezo yake.
Baada ya hapo aliamua kuwa mkimya zaidi maana hata bungeni alikuwa akichangia mara chache. Mwaka 2015 kama ilivyotarajiwa, alitia kuomba CCM imteua kuwa mgombea wake wa urais. Ifahamike kuwa Lowassa kabla ya kuwa Waziri Mkuu, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha kimataifa cha mikutano Arusha (AICC) Waziri wa Ardhi pia Waziri wa Maji. Tofauti na matarajio yake na wafuasi wake waaminifu jina la Lowassa hata halikuwemo miongoni mwa majina ya watia nia 5 waliojadiliwa na Kamati Kuu kiasi kwamba wakati mwenyekiti Jakaya Kikwete akiingia kwenye ukumbi kwa ajili ya kikao cha Halmashauri Kuu, baadhi wajumbe waliimba “tuna imani na Lowassa”.
Hata wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu wakiwemo Dkt. Emmanuel Nchimbi, Adam Kiimbisa na Sophia Simba walitoa kauli ya kupinga utaratibu uliotumika kukata jila na Lowassa. Hasira dhidi ya utaratibu wa uteuzi ulisababisha pia kuondoka kwa watu maarufu kama vile Kingunge Ngombale Mwiru ambaye ni mmoja wa watu waliohudumu kwa muda mrefu ndani ya serikali na chama, tangu enzi za chama cha TANU.
Kwa mfano mwaka mwaka 1973 Kingunge alikuwa mkuu wa mkoa wa Tanga. Uthibitisho upo kwenye jiwe la msingi la uwanja wa Mkwakwani ambao wakati ukizinduliwa mwaka huo, Kingunge alikuwa mgei rasmi.
Baada ya CCM kumtosa huku ikimteua Dkt. John Magufuli kupeperusha bendera, Lowassa aliamua kuitosa CCM na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeloe (Chadema), ambacho kilimteua kuwa mgombea wa urais.
Siasa za uchaguzi 2015 zilichangamka mno huku mikutano ya Lowassa, akiwakilisha pia vyama kadhaa vya upinzi chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ikivutia umati mkubwa na kusababisha shauku kuhusu matokeo ya ushindani mkali kati ya Magufuli na Lowassa.
Mwishowe Magufuli aliibuka mshindi kwa kuwa 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 dhidi ya Lowassa aliyepata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97, kiwango ambachi ni kikubwa zaidi kwa mgombea wa upinzani Tanzania tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Miaka mitatu baadaye Lowassa alirejea CCM na kusema kwa kifupi kuwa alikuwa amerejea nyumbani. Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2023.
Frederick Sumaye
Chanzo cha picha, Mallya
Uchaguzi wa mwaka 2015 pia ulishuhudia Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi wa miaka 10 kati ya Novemba, 1995 na Desemba, 2005 akiliacha jahazi la CCM Agosti 22, 2015 na kuhamia UKAWA na baadaye Chadema akieleza sababu za kufanya hivyo kuwa ni mawazo yake kutopewa nafasi serikalini na ndani ya CCM, hivyo alitaka kuwasaidia wapinzani kushika nchi.
Sumaye Hakuwahi kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya upinzani kwani hakuwa na wadhifa wa kitaifa. Nafasi kubwa rasmi aliyowahi kushika wakati akiwa Chadema ni uenyekiti wa kanda ya Pwani. Alirejea CCM mwanzoni mwa 2020, siku chache tu baada ya kushindwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti wa kanda.
Benard Membe
Chanzo cha picha, ACT
Kachero mwandamizi kitaaluma. Aliwahi kuwa mchambuzi mwandamizi wa Usalama wa Ikulu wakati wa uongozi wa Rais Benjamin Mkapa. Alifanya kazi katika ubalozi wa Tanzania nchini Canada. Kisiasa nafasi ya juu zaidi ilikuwa ni kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, akipanda kutoka Naibu Waziri.
Alijiamini mno kuwa angeteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa urais. Kielelezo ni pale aliposema Bungeni katikati mwa 2015 kuwa anaondoka akiwa Waziri na alitarajia kurejea bungeni akiwa katika wadhifa mwingine. Japo hakutamka moja kwa moja kuhusu wadhifa, wadadisi wa siasa walipata picha kuwa alimaanisha kurejea bungeni akiwa Rais wa nchi. Kwa mantiki hiyo, hakugombea ubunge kutetea kiti chake jimboni. Alipotia nia kugombea urais alifanikiwa kuingia hatua ya tano bora na kuishia hapo. Alifariki dunia Mei 12, 2023