Chanzo cha picha, Reuters
Huku kukiwa na misukosuko ya kisiasa nchini Syria, waandishi katika magazeti ya kimataifa wanazidi kujadili upinzani wa ndani wa Syria kuhusu mazungumzo na Israel na ripoti za vyombo vya habari kuhusu mikutano ya siri inayolenga kujadili uwezekano wa makubaliano ya usalama chini ya usimamizi wa Washington.
Tunaanza ziara yetu katika gazeti la Emirati, The National, kwa makala ya mwandishi Raghida Dergham, ambapo anauliza, “Kwa nini Syria ina haki ya kuzungumza na Israel?”
Mwandishi anasema uongozi mpya wa Syria, baada ya “kuifukuza Iran na Hezbollah katika nchi hiyo,” unaongoza mabadiliko katika uhusiano wake wa kikanda, hasa uhusiano wake na Israel.
Dargham anaeleza kwamba Syria, ambayo hapo awali ilikuwa “nguzo ya mradi wa upanuzi wa Iran,” sasa inatafuta kujiweka upya kikanda na kimataifa. Mabadiliko haya, anasema, yanafanyika kwa usaidizi wa nchi za Ghuba na ufadhili wa Marekani, chini ya uongozi mpya wa Syria unaowakilishwa na rais wa mpito Ahmed al-Sharaa.
Mwandishi anaeleza kuwa kuna ripoti za uwezekano wa makubaliano ya usalama chini ya Marekani kati ya Syria na Israel mwezi Septemba 25, katika hotuba inayotarajiwa ya Sharaa katika Umoja wa Mataifa.
Licha ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria kukanusha, Shirika rasmi la Habari la Syria liliripoti mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje Asaad Sheibani na ujumbe wa Israel kujadili masuala yanayohusiana na kupunguza mvutano, Israel kutoingia Syria na kufuatilia usitishaji vita katika Mkoa wa As-Suwayda.
Dargham anaeleza kuwa nia tu ya Damascus kuzungumza na Israel, licha ya “uvamizi wa kijeshi wa Israel” huko Gaza, inaashiria maendeleo ya uongozi mpya, ambao unaweka maslahi ya Syria juu ya ajenda yoyote ya kiitikadi au tamaa ya uongozi.
Anasema “serikali ya Syria bado haijawa na udhibiti kamili, na kuna hofu ya kupanuka kwa makundi yenye itikadi kali. Kwa hiyo, kauli ya Sharaa ya kukataa kugawanyika na wito wake wa kuunganishwa tena kwa Syria bila kutumia ghasia, lazima itafsiriwe katika hatua za kivitendo.”
Mwandishi anaongeza kuwa mjumbe wa Marekani Tom Barrack alihusika moja kwa moja katika kuendeleza maelewano kati ya Syria na Israel na kushughulikia mivutano ya kimadhehebu huko Sweida.
Anabainisha kuwa jukumu hili la Marekani linaratibiwa na Uturuki na mataifa ya Ghuba, kwa lengo la kuiweka Syria katika utulivu na kuvutia uwekezaji.
Dargham anaamini “Washington na madola makubwa ya Kiarabu yanapendezwa na kupungua kwa ushawishi wa Iran katika eneo la Levant, na wanaichukulia Syria leo kuwa msingi wa mkakati wao wa kukabiliana na Tehran.”
Mwandishi anahusisha hili na kile kinachotokea Lebanon, hasa ikiwa mpango wa kuwapokonya silaha Hezbollah utatimia. Anaonya kwamba “msisitizo wa Hezbollah kutaka kubaki silaha unatishia kutatiza majaribio yote ya suluhu na kuongezeka mvutano zaidi.”
Dargham anahitimisha makala yake kwa kusema, kuishutumu Damascus kwa uhaini kwa sababu tu ya kutaka maelewano na Israeli ni makosa. Inatafuta tu kurejesha eneo lake kutoka udhibiti wa Israel.
“Uhusiano wa Syria na Israel ni mzigo mkubwa kwa Ahmad al-Sharaa”
Chanzo cha picha, Reuters
Gazeti la Turkey Today, mwandishi Ömer Özkizilcik ameandika makala yenye kichwa “Pendekezo Jipya juu ya Sweida laleta Mtanziko kwa Serikali ya Syria.” Anajadili hali nchini Syria huku kukiwa na mazungumzo juu ya kuundwa kwa uhusiano wa karibu na Israel, akiashiria mpango wa Marekani na Israel unaopendekeza kuundwa kwa ukanda wa kibinadamu kutoka Israel hadi jimbo la Sweida.
Mwandishi anaeleza kuwa Marekani inatumai mpango huu utachangia “kufufua mazungumzo kati ya Syria na Israel,” hasa baada ya ripoti za awali kuashiria maendeleo katika maelewano ya pande mbili, kabla ya juhudi hizo kukatizwa kutokana na “kutoelewana.”
Ozkizilcik anaeleza “kutokuelewana” huko kulifuatiwa na hatua za hatari za Israel, ambazo ziilijumuisha kushambulia Wizara ya Ulinzi ya Syria na uwanja wa ikulu ya rais.
“Mashambulizi hayo yalikuwa tatizo kubwa kwa Ahmad al-Sharaa, ambaye alitumia neno ‘Taifa la Israel’ katika mazungumzo yake ya kisiasa, kauli ambayo haijawahi kushuhudiwa katika mazungumzo rasmi ya Syria,” mwandishi anasema.
Anabainisha kuwa Uturuki, licha ya uadui wake dhidi ya Israel, inamuhimiza al-Sharaa kuelekea kwenye maelewano ya kiusalama na Israel, “lakini mpango huo bado haupo kwenye makubaliano ya ndani, wala ndani ya safu ya Hay’at Tahrir al-Sham, wala ndani ya upinzani mpana wa Syria.”
Ozkizilcik anaeleza kwamba Sharaa, licha ya kukosolewa vikali na hata wafuasi wake wa karibu, hakurudi nyuma katika kuwasiliana na Israel, na amefikiria Syria kujiunga na “Makubaliano ya Ibrahimu” chini ya masharti fulani.
Hata hivyo, Sharaa anajua kwamba njia hii ni ya hatari kubwa, inayoweza kudhoofisha mshikamano na kutoa fursa kwa kile alichokielezea kama “makundi yenye itikadi kali” kutumia hasira za watu kuanzisha vurugu.”
Kulingana na Ozkizilcik, watu wengi wanaamini “Israel haiaminiki na mazungumzo nayo ni bure.” Lakini mwandishi anaeleza msimamo wa Washington, ambao kwa sasa umejikita katika “kujenga uaminifu” kati ya Syria na Israel.
Hata hivyo, lengo hili linaweza kuwa mzigo kwa Sharaa ikiwa litatafasiriwa kama makubaliano ya kusalimu amri. Kulingana na Ozkizilcik, kupoteza kwake uungwaji mkono wa ndani kutadhoofisha mkakati wa Marekani wa kuunga mkono utulivu wa Syria kupitia makubaliano na Israel.