#HABARI: Mahakama ya Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 10 mwaka huu, kusikiliza maombi ya walalamikaji katika kesi ya mgawanyo wa mali ambayo imefunguliwa na Mwenyekiti Mstaafu wa CHADEMA, Said Issa Mohamed, Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hii inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa CHADEMA na Katibu Mkuu wa Chama hicho na upande wa walalamikaji unawakilishwa na jopo la Mawakili watatu, huku wajibu maombi ambao ni CHADEMA, wakiwalishwa na jopo la mawakili wanne chini ya Dkt. Rugemeleza Nshala.
Kesi hii ya msingi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na mawakili wa pande zote kuainisha hoja zinazobishaniwa lakini hata hivyo imeshindwa kuendelea kutokana na mawakili wa walalamikaji kuwasilisha maombi mahakamani hapo.
Wakili Shaban Marijani, ameieleza Mahakama kuwa katika maombi hayo wanaomba wajibu maombi ambao ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwapatia nyaraka mbalimbali za cha hicho ambazo zitawasaidia katika kesi ya msingi.
Miongoni mwa nyaraka wanazoimba kupatiwa na CHADEMA ni muhtasari wa kikao cha Kamati Kuu kilichoketi kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2014, taarifa ya ukaguzi wa chama hicho, na taarifa ya fedha ya chama kuanzia mwaka 2019 hadi mwaka 2014.
Kwa upande wa mawakili wa wajibu maombi kupitia wakili wake Hekima Mwasipo, wameiomba Mahakama siku saba kwa ajili ya kuwasilisha kiapo kinzani kwa kuwa wana nia ya kupinga maombi hayo huku upande wa walalamikaji wakiomba siku tano kwa ajili ya kujibu.
Hata hivyo, baada ya hayo Jaji Hamidu Mwanga, akakubaliana na maombi hayo ambapo amepanga kusililiza maombi hayo Septemba 10, mwaka huu huku kesi ya msingi ikitegemea kuendelea baada ya uamuzi wa maombi hayo.
Katika kesi ya msingi walalamikaji wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na sheria ya vyama vya siasa na katiba ya chama hicho.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania
#Follow @itvtz @radioonetanzania
@capitaldigitaltanzania