Rais Samia na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi

Chanzo cha picha, CCM

Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu zimeanza rasmi leo, kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Hata hivyo, uchaguzi huu unatarajiwa kutokuwa na hamasa ya mshikemshike baada ya chama kikuu cha upinzani kutangaza kutoshiriki, kikidai mfumo wa uchaguzi wa sasa unakinufaisha chama tawala na hautoi usawa wa ushindani.

Kwa mujibu wa INEC, jumla ya vyama 18 vilivyosajiliwa vitashiriki uchaguzi huu, vikiwa na wagombea 17 wa urais.

Hali hiyo inatokana na mgombea wa urais wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, kutoidhinishwa kugombea baada ya Tume kubaini uteuzi wake ulikuwa kinyume cha taratibu.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pia ilimwengua rasmi kufuatia pingamizi lililotolewa na mwanachama wa chama hicho, Monalisa Ndala.
Sababu kuu iliyoelezwa ni kwamba Mpina alipata uanachama wa ACT-Wazalendo mnamo Agosti 5, 2025, nje ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambao ulipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025.

Hali hii imesababisha chama hicho kushindwa kushiriki katika nafasi ya urais mwaka huu.

Hata hivyo chama hicho kimekwenda Mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili na Tume.

Kwa upande wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuzindua rasmi kampeni zake Agosti 28, 2025 katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa CCM na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.

Samia Suluhu Hassan, ataongoza uzinduzi huo akifuatana na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Uzinduzi huo utaashiria mwanzo wa kampeni za CCM kwa nafasi za urais, ubunge na udiwani, huku chama hicho kitakuwa cha kwanza kuzindua kampeni zake tangu INEC ilipotangaza tarehe rasmi ya kuanza kwa kampeni, Agosti 28, 2025.



Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *