Ethiopia imetia saini makubaliano na kampuni ya Dangote kutoka Nigeria ya kujenga kiwanda cha kutengeneza mbolea kitakachogharimu doma Bilioni 2.5, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametangaza leo Alhamisi katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Uwekezaji huu ni sehemu ya juhudi za bilionea wa Nigeria Aliko Dangote kukomesha uagizaji wa mbolea barani Afrika.
Kiwanda hicho ambacho kitajengwa huko Gode, kusini mashariki mwa Ethiopia, kitazalisha tani milioni 3 za mbolea kwa mwaka, Abiy amesema.
Mkataba huo ulitiwa saini na Kampuni ya Ethiopian Investment Holdings (EIH) inayomilikiwa na serikali na kampuni ya Dangote.
Ethiopia itashikilia asilimia 40 ya hisa katika kampuni hiyo, huku kampuni ya Dangote ikiwa na asilimia 60, Mkurugenzi Mkuu wa EIH, Brook Taye amesema katika hafla ya kutia saini mkataba huo mjini Addis Ababa.
Taarifa ya EIH kwenye mtandao wa kijamii wa X imemnukuu bilionea Dangote akisema uwekezaji huo unawakilisha “maono ya pamoja ya kuifanya Afrika kuwa ya viwanda na kufikia usalama wa chakula katika bara zima.”
