Chanzo cha picha, Getty Images/EPA
-
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, BBC Swahili
Wachezaji walio na umri mdogo ambao wanapata msaada mkubwa wa mahitaji yao mengi wana uwezo mkubwa wa kufaulu katika mchezo huo, linasema Chama cha Wachezaji Kandanda wa Kulipwa.
Akizungumza baada ya mechi za kwanza za Ligi kuu ya soka Uingereza (Premier League) za vijana wenye vipaji vya Uingereza Max Dowman na Rio Ngumoha wikendi iliyopita, mtendaji mkuu wa PFA Maheta Molango alisema kuwa “utulivu ndio chanzo cha mafanikio”.
Ili kupata kujua walifikaje hapa na walikokulia tuangazie wachezaji walio na umri mdogo kucheza katika ligi kuu ya Uingereza msimu huu…
1. Ethan Nwaneri (miaka 15 miezi 5 siku 28)
Chanzo cha picha, Getty Images
Ethan Nwaneri alichipuka na kuweka jina lake kwenye historia ya Ligi Kuu ya kandanda Uingerezaa akiwa na umri wa miaka 15 na siku 181, alipoingia uwanjani mara ya kwanza na kuichezea Arsenal dhidi ya Brentford mnamo Septemba 2022 na kumfanya kuwa mchezaji aliye na umri mdogo kabisa kuwahi kucheza katika ligi kuu ya Uingereza.
Nwaneri ndiye mchezaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi Arsenal kucheza mchezo wa hatua ya muondoano ya Ligi ya Mabingwa ulaya, baada ya Cesc Fabregas dhidi ya Bayern Munich Machi 2005 (17y 309d).
Pia ni mchezaji wa tatu wa Uingereza kuanza mchezo wa hatua ya muondoano ya UCL akiwa chini ya umri wa miaka 18, baada ya Jude Bellingham na Phil Foden.
Kiungo huyo wa kati mwenye umri wa miaka 18 ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi wa Arsenal kufunga bao la raundi ya muondoano ya UCL na wa tatu kwa jumla katika mashindano hayo baada ya Bojan Aprili 2008 (17y 217d) na Jude Bellingham Aprili 2021 (17y 289d).
Alipokea nafasi ya kushiriki baada ya Bukayo Saka kuumia. Mchezaji huyu aliyezaliwa Machi tarehe 21 2007, amecheza mechi 37 katika mashindano yote, akifunga mabao 9 na kutoa assist 2 msimu uliopita.
“Yeye kamwe [hana wasiwasi], ni mtulivu na anajiamini katika uwezo wake,” alisema kocha wa Gunners Mikel Arteta baada ya Nwaneri kufunga bao katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Girona mnamo Januari. “Katika umri wa miaka 17, kufunga bao muhimu sana katika Ligi ya Mabingwa si jambo la kawaida.”
Wiki tatu zilizopita kiungo wa kati mshambulizi Nwaneri alitia saini mkataba mpya wa miaka mitano na Arsenali ili kuwazuia Chelsea na Manchester City kumnyakua kiungo huyo wa England.
“Inamaanisha kila kitu kwangu, nina furaha sana kuifanikisha. Hapa ndipo ninapojisikia niko nyumbani, na ambapo nitaenda kuendeleza ubora zaidi,” alisema Nwaneri.
2. Max Dowman (miaka 15 miezi 7 siku 24)
Chanzo cha picha, Getty Images
Max Dowman ana umri wa kutosha kucheza Ligi Kuu lakini hajaruhusiwa kuwa katika chumba kimoja na wenzake wa kikosi wakati wakubadilisha nguo.
Winga huyu alionyesha kwa nini ni kipaji cha haiba ya juu nchini mwake alipocheza mara ya kwanza katika Ligi Kuu ya EPL akiwa na miaka 15 na siku 235 Jumamosi iliyopita dhidi ya Leeds United.
Katika mechi hiyo alizalisha penalti ambayo imempa nyota zaidi.
Ujasiri wake umemfanya Max Dowman kuthibitisha mapema ni nani atakayemfuata Nwaneri.
Kipaji chake hakitishii mtu aliyezoeana na hali ya Arsenal kwa miaka ya hivi karibuni.
Dowman amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Arsenal tangu akiwa na miaka 14.
Kutokana na nyota yake inayong’aa Arsenal imeweka mikakati dhabiti kumuepusha na majeraha na kimlinda.
Changamoto hizo ni pamoja na mahali ambako hubadilisha nguo, anaruhusiwa kubadilishia jezi zake katika chumba tofauti kando na wenzake kabla ya mazoezi na siku za mchezo, ingawa anaweza kujiunga nao wakati wa mazungumzo ya timu.
Kocha Mikel Arteta na klabu wamekuwa makini sana kuelekeza maendeleo ya Dowman.
Baada ya kuingia uwanjani mara ya kwanza dhidi ya Leeds, Arteta alisema wamekuwa wakikusanya taarifa za jinsi anavyoweza kujituma katika hali kama ya kukaa benchi, kushiriki mazoezini na hata kutojumuishwa kwenye kikosi siku fulani.
Seti ya usalama pia imeimarishwa.
Mlinzi mmoja maalum ameteuliwa kumfuata kila mahali anapoenda, ikiwa ni pamoja na uwanjani pale Emirates.
Aidha, changamoto yake kubwa ni kumaliza shule wakati mafunzo ya mpira yanaendelea kwa pamoja.
Wachezaji wana vyumba tofauti katika hoteli siku za ugenini, kwa hivyo kusafiri sio shida.
3. Jeremy Monga (miaka 15 miezi 8 siku 28)
Chanzo cha picha, Getty Images
Jeremy ambaye anasomea chuo cha Rotcliffe alizaliwa tarehe 10 mwezi Julai 2009.
Monga alianza uchezaji wake na Coventry City, kabla ya kujiunga na akademia ya Leicester City akiwa na umri wa miaka minane kucheza katika kiwango cha chini ya miaka 9.
Jeremy Monga ni mchezaji mdogo zaidi kucheza mwanzo wa mechi katika historia ya Leicester City.
Mechi ya kwanza ya Jeremy Monga ilikuwa katika dimba la Carabao dhidi ya Huddersfield akiwa na umri wa miaka 16 na siku 34, na kuvunja rekodi ya Peter Shilton ambaye alikuwa na umri wa miaka 16 na siku 228, aliyekuwa mlinda mlango wa Foxes na timu ya taifa ya England kwa miaka 59.
Katika mechi hiyo dhidi ya Huddersfield, alikamilisha dakika 60 za kucheza, akapigwa kadi njano dakika ya 14, na alikabiliwa na masimango kutoka kwa mashabiki lakini alijitwaza kwa tabia yake ya ujasiri.
Kocha wa Leicester, Marti Cifuentes, alithibitisha kama hivi:
“Nimeridhika sana kwa Jeremy kuanza mechi na kutimiza rekodi hii ni muhimu sana kwake. Jukumu langu kubwa ni kuhakikisha kuwa sio tu kuchezeshwa kwa mara ya kwanza bali pia kuhakikisha wana ufanisi”.
Wiki chache tu baadaye, alivunja rekodi nyingine akawa mchezaji mwenye umri mdogo kabisa kuifungia Leicester City goli katika mechi ya Championship dhidi ya Preston akiwa na umri wa miaka 16 na siku 37.
Hii imevunja rekodi ya Jude Bellingham (umri 16, siku 63) iliyodumu tangu 2019.
4. Willian Estêvão (miaka 18, siku 120)
Chanzo cha picha, Getty Images
Willian Estêvão (miaka 18, miaka 120) sasa ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Premier League kusaidia bao la Chelsea katika ushindi wa 5-1 ugenini dhidi ya West Ham.
La kufurahisha zaidi yeye ni muimbaji .
Estevao Willian alitakiwa kufanyiwa utambulisho hatua kwa hatua Stamford Bridge, lakini mazingira yameongeza kasi ya mchakato mzima kwa kiasi kikubwa.
Mashabiki walionywa kwa muda mrefu kabla ya kuwasili kwamba angehitaji muda ili kuzoea maisha ya England na Ligi Kuu.
Lakini majaribio yoyote ya kufifisha matarajio yameharibiwa kutokana na kuanza kwake kwa maisha huko London Magharibi.
Aling’aa katika mechi mbili za kirafiki, kisha alipata nafasi ya kujumuishwa kikosini kufuatia jeraha la Cole Palmer kabla ya mechi ya Ijumaa dhidi ya West Ham kung’oa nanga.
Alicheza dakiki 77 na kuchochea kuilaza wananyundo. Lakini sio tu hayo Estevao ana mengi ya kupigiwa mfano kuanzia ukomavu wake na kuwa mtulivu uwanjani akichezea timu yake mpya kama alivyokuwa akipeperusha bendera ya timu yake ya utotoni ya Brasileirao.
Jaribio la meneja wa Chelsea Enzo Maresca kumshusha chini winga huyo kidogo kwa kutumia mahojiano yake baada ya mchezo kuashiria makosa ya Estevao ambayo yaligeuzwa kuwa goli la kwanza la West Ham yanaeleweka – lakini ilionekana kuwa bure.
Tayari ni zaidi ya nyota anayechipukia, na zaidi tatizo la meneja litakuwa jinsi ya kuepuka simu zinazoongezeka za kumwanzisha kila wiki; badala ya jinsi bora ya kumfanyia mazoezi ili ajumuishwe kwenye timu polepole na kwa usalama.
Estevao ni mwanachama wa kinachojulikana kama “geracao do bilhao” – kizazi cha wachezaji ambao pia wanajumuisha Endrick anayetumikia Real Madrid na nyota mpya wa West Ham Luis Guilherme.
Wote watatu wamekuwa wakiteka anga ya ulingo wa spoti tangu wakiwa watoto Estevao mwenyewe alikuwa na umri wa miaka 10 pekee mara ya kwanza Palmeiras ilipojaribu kumvutia kwenye akademia yao, lakini walishindwa kufikia ofa iliyoripotiwa kuwa mara 10 zaidi kutoka kwa Cruzeiro.
Kisha akawa mwanasoka mwenye umri mdogo zaidi wa Brazil kutia saini mkataba na Nike, akiwazidi Neymar (13) na Rodrygo (11), na akapewa jina la ‘Messinho’ (Messi mdogo) kwa uwezo wake wa kubadilisha mwelekeo na kuwapiga chenga wapinzani huku akikimbia na mpira kwa kasi.
Haikuwashangaza sana wale waliokuwa wakimfuatilia wakati gazeti la Uhispania AS liliposema wakati wa Kombe la Dunia la U-17 2023 kwamba “Brazil ina fikra mpya”.
Licha ya kufanana na Lionel Messi, Estevao amesema hataki kuitwa ‘Messinho’ tena.
Sio tu mguu wake wa kushoto ambao huwaacha wengine wakivutiwa, lakini pia mawazo ambayo tayari anayo. Sampaio anakumbuka kipindi kilichoonyesha hilo.
Winga wa kulia ambaye pia anaweza kucheza kama nambari 10, Estevao amekuwa akichukuliwa tofauti kwenye klabu.
Kuna hisia nchini Brazil kwamba mvulana huyo kutoka mashambani mwa Sao Paulo anaweza kuwa kitu kingine, aina ya mchezaji anayekuja mara moja kwa muongo mmoja na anaonekana kupangwa kufika kileleni.
“Estevao ndiye mchezaji bora aliyetokea katika soka ya Brazil tangu Neymar. Unamtazama na unampenda,” mkuu wa akademia ya Palmeiras, Joao Paulo Sampaio, aliambia BBC Sport.
5. Harvey Daniel James Elliot (miaka 16 mwezi mmoja)
Chanzo cha picha, Getty Images
Harvey Daniel James Elliott ambaye ni Muingereza ni kiungo mshambuliaji au winga wa kulia wa klabu ya Ligi ya EPL ya Liverpool.
Uchezaji wa Harvey Elliott kwa vijana wa chini ya miaka 21 wa England hautashangaza kabisa kwa yeyote anayehusishwa na Klabu ya soka ya Liverpool.
Kila mtu anajua kipaji alichonacho kijana huyo mwenye umri wa miaka 22, tatizo kubwa la ‘almasi wa wekundu ni kupata nafasi ndani ya mifumo ya wasimamizi wawili waliopita.
Imekuwa hadithi ya bahati mbaya, ingawa nina uhakika Elliott mwenyewe hatawahi kuielezea kama hivyo.
Kwa haki, kupitia macho yake, anaweza kusema kwamba ameweza kukua na kuchangia timu anayoshabikia, na amepata heshima ya nyumbani tangu alipoanza kucheza tena Septemba 2019 na pia kuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia la chipukizi.
Bila kujali, usajili wa rekodi ya klabu kwa Florian Wirtz unahisi kama kikwazo kingine kwa Elliott, ambaye alianza mechi sita tu chini ya Arne Slot mnamo 2024-25.
Iwapo meneja wa Reds na kiungo wa kati watakaa chini msimu huu wa joto kutafakari mkakati wa kuondoka au atasalia kupigania nafasi yake bado haijajulikana.
Chochote kinachotokea, hakuna shaka Elliott anastahili kujikuta ambapo kipaji chake kinaweza kuonekana mara kwa mara.
Wachezaji bora waliowahi kucheza wakiwa na umri mdogo
Kuna majina ya wachezaji wengine tajika kwenye orodha ya wachezaji 20 bora walio na umri mdogo zaidi kuwahi kucheza katika Ligi kuu ya soka Uingereza.
Aliyekuwa na ufanisi mkubwa zaidi ni Wayne Rooney, ambaye alikuwa na miaka 16 na siku 297 alipoichezea Everton kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2002.
Miaka miwili baadaye alijiunga na Manchester United, ambapo alishinda mataji 16 na kuwa mfungaji bora katika historia ya timu hiyo akifunga mabao 253 katika mechi 559.
Rooney aliichezea timu ya taifa ya England mara 120, mara nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote mwengine ambaye si mlinda lango, na akaifungia three lions mabao 53 akiwa wa pili bora nyuma ya Harry Kane.
Jack Wilshere lalikuwa na umri wa miaka 16 na siku 256 alipoiwakilisha Arsenal kwa mara ya kwanza 2008, aliichezea mara 197 na kushinda kombe la FA mara mbili.
Kiungo huyo wa kati ambaye aliichezea timu ya taifa ya England mara 34 aliwahi pia kuchezea West Ham, Bolton, Bournemouth na klabu ya Denmark AGF Aarhus.
Alistaafu kucheza soka akiwa na miaka 30 mnamo mwaka 2023.
James Milner amecheza mechi takriban 900 tangu aanze kuichezea Leeds mwaka 2003 akiwa na miaka 16 na siku 310.
kiungo huyo wa kati aidha amechezea Newcastle, Aston Villa, Manchester City na Liverpool, na kushinda mataji 12, ikiwemo Ligi kuu Uingereza mara tatu na KLabu bingwa Ulaya.
Alijiunga na Brighton mwaka 2023 na kuwa mchezaji wa kwanza katika historia kucheza misimu 23 ambapo amehusika katika siku ya kwanza ya msimu hadi 2024-25.