Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ameeleza hasira yake kufuatia shambulio kubwa zaidi la Urusi mjini Kyiv tangu Julai, ambapo watu 23 akiwemo watoto wanne waliuawa na ofisi ya ujumbe wa EU pamoja na majengo jirani kuharibiwa.
Maafisa wa Ukraine wamesema makombora ya Urusi yaliharibu jengo la ghorofa tano katika wilaya ya Darnytskyi, na wengi wa waliokufa walikuwa humo.
Wengine kadhaa walijeruhiwa, wakiwemo watoto.
Von der Leyen alisema makombora mawili yalipiga karibu na ujumbe wa EU umbali wa mita 50 pekee ndani ya sekunde 20, jambo alilolaani vikali.
Ofisi ya Baraza la Uingereza pia iliharibiwa.
Jeshi la Ukraine liliripoti kuwa Urusi ilitumia karibu ndege zisizo na rubani 600 na zaidi ya makombora 30 ya masafa marefu katika shambulio hilo, likiwa kubwa zaidi mwezi huu.
Shambulio hilo lilitokea majira ya saa 9 alfajiri, likisababisha jengo la makazi kuporomoka. Vikosi vya uokoaji vilionekana wakiondoa kifusi na kutafuta manusura. Maafisa wamesema watoto waliouawa walikuwa na umri wa miaka 2, 14 na 17.