#HABARI: Wizara, Taasisi na Mashirika binafsi, zimetakiwa kutekeleza utoaji wa huduma za ustawi wa Jamii kwa vitendo ili kuwa na jamii yenye uwezo wa ustahimilivu na yenye mchango wa kuleta maendeleo kwa mtu, jamii na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa mkoani Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Kilele cha Wiki ya Ustawi wa Jamii kilichofanyika katika Viwanja vya Ustawi wa Jamii Kijitonyama.
Dkt. Jingu amesema uhitaji wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini umeendelea kuongezeka kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kutokana na mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha yakiwemo ya uchumi, siasa, jamii.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, wadau wa maendeleo na mashirika ya hiari inashughulikia changamoto zinazowakabili makundi maalum na jamii kwa ujumla.
“Natoa rai kwa wazazi/walezi na watanzania kwa ujumla kulinda haki na Ustawi wa Jamii kwa watoto wetu ili kuilinda nguvu kazi ya Taifa kwa maisha ya baadae. Kwani ulinzi na usalama wa watoto wetu ni jukumu letu sote.” amesema Dkt. Jingu
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVT