Chanzo cha picha, Ana Lolenzana
Washindi wa tuzo ya Micheline Masala y Maiz wana matumaini ya kueneza mtindo wao kote Mexico na duniani kote.
Wakati Norma Listman na Saqib Keval, ambao ni wamiliki na wapishi katika mojawapo ya migahawa maarufu ya Mexico City, Masala y Maiz, waliposhinda nyota yao ya kwanza ya Michelin, walikuwa New York City kwenye tafrija ya mpishi mwenzao.
“Timu yetu ilikuwa ikitupigia simu, na hatukuwa tukipokea simu,” anaelezea Listman huku akicheka. “Halafu mmoja wa mameneja wetu mkuu zaidi, ambaye kwa kawaida huwa hapigi simu isipokuwa kama kuna kitu kibaya akapiga simu. Ikabainika kuwa tulikuwa moja kwa moja kwenye jukwaa [kwenye tuzo za Michelin].”
Wanandoa, wanaojulikana kwa kuanzisha mgahawa wa kipekee “Kula Unachotaka, Lipa Unachoweza”, wana shauku ya kusaidia jamii zaidi kuliko kupata sifa za kifahari.
Kutumia wakati kusherehekea mpishi mwenza ayewavutia badala ya kuhudhuria sherehe ya tuzo kwa heshima yake ilikuwa muhimu zaidi kwa Listman na Keval.
Chanzo cha picha, Ana Rolenzana
Chukua, kwa mfano, mtindo wa kulipa kile unachoweza ambao umeifanya Masala y Maiz kuwa maarufu sana. Mara kadhaa kwa mwaka, wahudhuriaji wa mikahawa hupewa menyu ya sahihi ya vyakula vya Mexico, vyakula vya Kiafrika na vya Kihindi vilivyochanganywa pamoja na bahasha ambayo wanaweza kuacha malipo yoyote waliyo nayo au ambayo wanaona kuwa yanakubalika.
Hakuna bili wala kuomba wawekewe nafasi kwenye mgahawa , wageni lazima wajipange ili kupata uzoefu wa kwanza na wa huduma ya kwanza.
Lakini kuna sharti moja: wanaokula chakula lazima waandike ni kiasi gani walichokiacha kimekusudiwa kwa ajili ya malipo ya wafanyikazi badala ya mkahawa wenyewe.
Lengo kuhakikisha kwamba kila mtu katika jiji hilo, bila kujali hali yake ya kiuchumi, anaweza kufurahia sahani zilizoandaliwa hapa: Camarones pa’pelar , sahani ya shrimp iliyopikwa kwa vanilla, ndimu na samli, na Kuku Poussin , kuku mdogo wa kukaanga kwa jibini, huandaliwa kwa njia inayofanana kwa ukubwa na ubora, lakini bila lebo ya bei iliyoambatanishwa.
Wanandoa hao wanasema hawapotezi pesa katika biashara yao. Wageni wengi hutoa kitu, hata ikiwa ni sanaa asili tu kwa wafanyikazi, huku wengine wakiwalipa hata zaidi , wanasema, wakati mwingine kama mara tatu ya gharama ya kawaida.
Kwa wamiliki, ni hatua ya kuhuzunisha sana katika jiji linalotatizika na masuala ya uboreshaji na utalii wa kupindukia . “Kuna tofauti nyingi za kitabaka, kuna tofauti nyingi za kiuchumi katika jiji,” anasema Listman. “Kuna watu ambao wanapata pesa nyingi na kuna wafanyakazi mbali mbali tofauti . Hii itapunguza mgawanyiko huo wa tabaka na mgawanyiko huo wa kiuchumi na kufanya migahawa kufikiwa na kila mtu – angalau kwa siku moja.”
Chanzo cha picha, Ana Lorenzana
Ijapokuwa sherehe haikuwa kuhusu kikombe chao cha chai, Listman na Keval walitambua jinsi nyota ya Michelin inavyoweza kuifaidi jamii yao, na hivyo kukuza ufahamu wa wazo hili zaidi ya watarajiwa wao wa chakula na mikahawa mingine kote Mexico City.
Mwaka huu, kwa mara ya kwanza, walaji wa Mexico City watashiriki katika migahawa 20 ya ziada ya Mexico City ya “Kula Unachotaka, Lipa Unachoweza Siku” mnamo tarehe 27 Agosti kulingana na mtindo wa Masala y Maiz. Tukio hilo litakuwa la kwanza kati ya kile ambacho Keval anatumai kuwa kitakuwa ni utamaduni kote ulimwenguni.
“Tumekuwa na watu kutoka Chile waliofika, kutoka Colombia, kutoka sehemu zingine za Mexico, kutoka Peru ambao wanataka kujiunga,” aliambia BBC. “Na sioni kwa nini hii haiwezi kuwa kama ‘lipa unachoweza kimataifa.’
Mwaka huu, biashara zinazoshiriki ni kuanzia viwanda vidogo vya kuoka mikate vinavyomilikiwa na familia viitwavyo panaderías kama vile Panadería Valle Luna huko Colonia Juarez, hadi Expendio de Maíz , sehemu nyingine ya jiji yenye nyota ya Michelin, ambayo hutoa vyakula vya asili vya Kimexico .
Kuna zaidi ya mikahawa 20 kwa jumla inayoshiriki katika hafla hiyo, ambayo Listman na Keval wanatarajia itafanyika mwaka ujao.
“Tulihamasishwa kimsingi na ujenzi wa jamii,” alisema Ximena Igartúa, wa Baa ya Loup katika Wilaya ya Cuauhtémoc, ambayo inashiriki katika hafla hiyo. “Ni ujumbe wa pamoja wa umoja na mshikamano, na mwaliko wa kujaribu kuvunja mawazo tuliyojiwekea. Pia ni njia ya kuwarudishia shukrani wateja wetu kwa kila kitu tunachopokea.”
Chanzo cha picha, Ana Rolenzana
Keval anatumai tukio hilo linaweza kuibua mtindo mkubwa zaidi ulimwenguni, ndoto ambayo inaweza kuwa tayari iko njiani kutimia. Tayari kuna mipango mingine ya kulipa unachoweza ambayo inapatikana mahali pengine, kama vile Mkahawa wa Annalakshmi huko Singapore au Rethink Cafe huko Brooklyn, NY, mbali na mpango wa Mexico City.
Kuhusu wamiliki wa Masala y Maiz, matumaini ni kwamba migahawa zaidi na watu zaidi wataweza kunufaika na mlo mzuri kwa bei yoyote.
“Kazi ya mgahawa ni ngumu sana na mapato yake yanapungua sana. Mbali na ugumu wake, fursa ya kufikia ndoto yako ni finyu sana ,” Keval anasema. “[Lakini] hili ni jambo linaloweza kufanyika.”
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi