Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Olesya Zhygalyuk
- Nafasi, Idhaa ya Urusi ya BBC
Ili Ukraine iendelee kuwepo kama taifa huru, haitoshi kuipatia msaada wa kawaida.
Inahitaji silaha zenye nguvu, za kisasa na za muda mrefu, zitakazoiwezesha kumaliza vita kwa masharti yake yenyewe, anaandika Dan Sleeth, mshauri mwandamizi wa masuala ya Urusi na Ukraine katika Tony Blair Institute for Global Change, kupitia safu yake ya maoni katika gazeti la Politico.
Kwa mujibu wa Sleeth, Urusi ilishatupilia mbali matarajio ya ushindi wa haraka.
Sasa imejikita kwenye vita ya msuguano, mkakati wa kuisubiri Ukraine ichoke.
Kremlin inaamini muda upo upande wake, na kwamba Ukraine na washirika wake watachoka kabla ya Moscow.
“Mazungumzo ya amani bado yanawezekana, lakini kwa sasa ni nadra,” Sleeth anasema. “Moscow inakataa ombi la Kyiv la kusitisha mapigano kabla ya kuanza mazungumzo.”
Kwa mtazamo wake, Vladimir Putin anaamini Urusi itaweza kuvumilia tu hadi wapinzani wake waanguke kwa uchovu, hata kama haitapata ushindi wa moja kwa moja kwenye uwanja wa mapambano.
Kwa nini mkakati wa Putin unaweza kushindwa
Katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu ya vita kamili, Urusi inadhibiti takriban asilimia 19 ya ardhi ya Ukraine.
Hata hivyo, Sleeth anakumbusha kuwa udhibiti huu umepatikana kwa gharama kubwa, ikiwa ni pamoja na vifo vingi, uharibifu mkubwa wa vifaa, na shinikizo la kiuchumi.
“Uchumi wa Urusi uko chini ya mzigo mkubwa, ukuaji wa uchumi umepungua, mfumuko wa bei na riba vimepanda, huku vikwazo vya kimataifa vikizidi kuiandama,” anaeleza.
Kwa sasa, Putin anajaribu kupima mahitaji ya kijeshi dhidi ya matarajio ya wananchi wake, lakini Sleeth anaonya kuwa hali hii haitadumu kwa muda mrefu.
Uchambuzi unaonesha kuwa ikiwa vita vitaendelea, Urusi itatumia pesa nyingi zaidi katika kuendesha jeshi kuliko inavyotumia katika elimu na afya kwa pamoja.
Chanzo cha picha, Ramil Sitdikov/Sputnik/Kremlin Pool
Hata hivyo, licha ya changamoto hizi za ndani, Kremlin bado inaendeleza vita vya uchovu, ikiamini kuwa rasilimali za Ukraine ni finyu na msaada wa Magharibi hautadumu.
“Kremlin inaamini muda uko upande wake, kwamba Kyiv italazimika kutoa masharti ya amani yenye upendeleo kwa Urusi,” anaandika Sleeth.
Mkakati huu, Sleeth anasema, haujalenga ushindi wa haraka, bali kumchosha adui na utafanikiwa iwapo mataifa ya Magharibi haitabadilisha mkakati wake wa sasa.
Nini Ukraine inahitaji ili kushinda vita?
Sleeth anasema Ukraine na mataifa ya Ulaya wako katika kipindi cha maamuzi muhimu.
Ikiwa msaada utabaki katika kiwango cha sasa, mkakati wa muda mrefu wa Kremlin utafanikiwa.
Lakini, ikiwa mataifa ya Magharibi itaongeza kwa kiwango kikubwa msaada wake, Ukraine inaweza kubadilisha mwelekeo wa vita, kuchukua hatua ya mashambulizi, na kulazimisha Moscow kutathmini upya mikakati yake.
“Magharibi lazima iachane na msaada wa kijuujuu,” anasisitiza Sleeth. “Zinahitajika hatua halisi na madhubuti.”
Sio tu kutuma mifumo maarufu kama ndege za kivita za F-16, bali msaada unapaswa kuwa thabiti, wenye wingi, na unaohusisha aina mbalimbali za silaha.
Sleeth anataja vifaa vinavyohitajika na Ukraine kwa sasa:
1. Magari ya kivita na mizinga kwa ajili ya harakati na mashambulizi ya ardhini;
2. Risasi za mizinga ya 155mm kwa mtiririko wa kudumu;
3. Uzalishaji mkubwa wa droni za kushambulia na za upelelezi;
4. Vifaa vya uhandisi kuvunja ngome za Urusi.
“Bila vifaa hivi, Ukraine itabaki kwenye mtego wa vita vya msuguano na kwa njia hiyo, itashindwa vita ya kustahimili,” anaonya.
Kwa mujibu wa Sleeth, msaada wa kweli kwa Ukraine unapaswa kupangwa kwa miaka, si kwa vipindi vya muda mfupi. Hii ndiyo njia pekee ya kuvunja mkakati wa Putin wa muda mrefu.
Sleeth anasema hali hiyo italazimisha Kremlin kutathmini upya mkakati wake.
Kibarua cha mataifa ya Ulaya: Kuachana na fikra za muda mfupi
Sleeth anasisitiza kuwa viongozi wa Ulaya wanapaswa kupita katika mtihani wao wenyewe kuacha fikra za muda mfupi na kupanga kwa urefu.
Chanzo cha picha, EPA
“Kuisaidia Ukraine katika awamu hii mpya si tu suala la kudhibiti ardhi,” anaandika. “Ni swali la uwepo wa taifa hilo. Ikiwa Ukraine inataka kusalia hai na imara mwaka mmoja kutoka sasa, lazima iwe na uwezo wa kijeshi unaoifanya iamue hatima ya vita yenyewe.”
Kikao cha kilele cha hivi karibuni jijini Washington kilionesha umoja wa bara la Ulaya na dhamira ya kuhakikisha Ukraine inapata amani kwa masharti yake yenyewe.
“Kama msukumo huu utatumiwa ipasavyo,” Sleeth anaandika, “unaweza kuzalisha mkakati wa pamoja, ambapo bara zima la Ulaya litasimama na malengo ya pamoja.”
“Mwaka 1991, Ukraine ilijipatia uhuru. Mwaka 2022, iliutetea. Sasa, mwaka 2025, inahitaji msaada mkubwa zaidi.
Haitakiwi maneno, bali hatua thabiti na kadiri zinavyowahi, ndivyo bora zaidi.”
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid