Washington imekataa siku ya Ijumaa, Agosti 29, kutoa viza kwa wajumbe wa ujumbe wa Palestina uliopangwa kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba. Mkutano ambao Ufaransa inatarajiwa kutetea kutambuliwa kwa taifa la Palestina. Israel imepongeza uamuzi huo, huku mamlaka ya Palestina ikiitaka Marekani kubatilisha uamuzi wake. Uamuzi ambao baadhi wanachukulia “kinyume na sheria za kimataifa.”

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Utawala wa Marekani umehalalisha hatua yake ya kukataa kutoa viza kwa ujumbe wa Palestina ikitaja misingi ya “usalama wa taifa”, na kuishutumu Mamlaka ya Palestina na Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kwa “kushindwa kutimiza ahadi zao na kuhatarisha matarajio ya amani.”

Wizara ya Mambo ya Nje imewashutumu Wapalestina kwa kutumia mfumo wa haki kwa malengo yasiyo halali kwa kwasilisha malalamiko yao kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutatua mizozo yao na Israel. Mamlaka ya Palestina lazima ikomeshe “majaribio ya kukwepa mazungumzo kupitia vita vya kisheria vya kimataifa” na “juhudi za kupata utambuzi wa upande mmoja wa taifa la Palestina,” imesema taarifa hiyo. Huu ulikuwa ujumbe wa uungwaji mkono, kwa mara nyingine tena, kwa Israel, ambayo inaendelea kutekeleza mashambulizi ya mabomu katika Ukanda wa Gaza.

Uamuzi ulio “kinyume na sheria za kimataifa”

Gideon Saar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, ameushukuru utawala wa Trump kwenye mitandao ya kijamii kwa “hatua hii ya ujasiri” na “kuunga mkono Israel kwa mara nyingine.” Mamlaka ya Palestina, kwa upande wake, imeelezea “masikitiko yake makubwa na kushangazwa” na uamuzi huu, ambao “unakinzana na sheria za kimataifa,” na kuitaka Washington “kuubadilisha”.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric mesema ni “muhimu” kwa mataifa yote na waangalizi wa kudumu, wakiwemo Wapalestina, wawakilishwe katika mkutano uliopangwa kufanyika siku moja kabla ya Mkutano Mkuu kuanza. “Tunatumai kuwa hili litatatuliwa.”

Hali ambayo haijawahi kutokea

Marekani, ambayo ni mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, haitakiwi kuwanyima viza wajumbe wanaosafiri huko. Walakini, hii imetokea huko nyuma. Mnamo mwaka 1988, Yasser Arafat, kiongozi wa kihistoria wa PLO, alinyimwa viza ya kuingia Marekani. Kisha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao maalum huko Geneva, ambapo lilitambua tangazo la uhuru wa Palestina.

Mnamo mwaka wa 2013, rais wa zamani wa Sudan Omar Al Bashir alitangazwa kuwa mtu asiyefaa huko New York. Wakati huo, alikuwa chini ya hati ya kukamatwa kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, pamoja na mambo mengine, kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kama Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alivyo leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *