#HABARI: Moto mkubwa ambao chanzo chake hakijajulikana umeibuka na kuteketeza jengo la ghorofa linaloendelea kujengwa katika eneo la Kariakoo, kwenye makutano ya Mitaa ya Aggrey na Sikukuu, majira ya saa sita mchana wa leo Agosti 31, 2025.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa awali waliona moshi mzito ukifanana na vumbi kutoka kwenye jengo hilo, kabla ya moto kuanza kushika na kusambaa kwa haraka.
Wananchi waliokuwa eneo hilo walitoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ambapo magari ya zimamoto na askari wa polisi waliwasili kwa dharura kujaribu kudhibiti moto huo.
Hadi sasa, juhudi za kuuzima moto zinaendelea huku mamlaka husika zikieleza kuwa chanzo cha moto bado hakijafahamika. Hakuna taarifa za majeruhi au vifo zilizothibitishwa mara moja.
Jeshi la Polisi limesema litatoa taarifa kamili mara baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.