
Katika taarifa yenye nguvu isiyo ya kawaida, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeionya Israel siku ya Jumamosi, Agosti 30, dhidi ya kuwahamisha watu wengi kutoka mji wa Gaza. Wakati taifa hilo la Kiyahudi likiimarisha mzingiro wake dhidi ya mji huo kwa ajili ya kujiandaa na kile inachokiita kuwa ni mashambulio makubwa dhidi ya vuguvugu la Hamas la Palestina katika mji huo, shirika hilo la misaada ya kibinadamu limeonya kuwa mpango huo “hauwezekani” na “haueleweki.”
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Haiwezekani kuhamishwa kwa watu wengi katika Jiji la Gaza kunaweza kutekelezwa kwa usalama na heshima katika hali ya sasa,” amesema Mirjana Spoljaric, Mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC). Mpango kama huo “sio tu hauwezekani, lakini pia haueleweki” ikiwa Israel inakusudia kuheshimu kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, amesema.
Siku ya Ijumaa jeshi la Israel lilitangaza rasmi mji wa Gaza kuwa “eneo hatari la mapigano”, kwa ajili ya maandalizi ya mashambulizi yake makubwa yanayokuja. Jeshi halikutoa wito wa watu kuhamishwa kutoka jiji hilo, lakini msemaji wake alisema siku ya Jumatano kwamba kuhamishwa huko kwa watu “hakuwezi kuepukika.” Licha ya kuongezeka kwa shinikizo kutoka nje na ndani ya Israel, serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu inashikilia kuwa ina nia ya kuendeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza, na jeshi limeagizwa kujiandaa kwa mashambulizi ya kila upande katika mji wa Gaza.
Baada ya karibu miezi 23 ya vita ambavyo vimeharibu Ukanda wa Gaza, kuhamishwa kwa watu kutoka Jiji la Gaza “kungesababisha kuhama kwa watu wengi ambao hakuna eneo la Ukanda wa Gaza lingeweza kuchukua,” ameonya Bi. Spoljaric. “Iwapo amri ya kuhama itatolewa, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, Israel lazima ifanye kila iwezalo kuhakikisha kwamba raia wanafurahia hali ya kuridhisha katika suala la makazi, usafi, afya, usalama na upatikanaji wa chakula (…). Masharti haya hayawezi kufikiwa kwa sasa huko Gaza,” ameongeza.
Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, takriban Wapalestina milioni moja wako katika mji wa Gaza. Maelfu ya wakaazi tayari wameukimbia mji huo, ulioko kaskazini mwa eneo hilo, ambako karibu watu milioni moja wanaishi, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.
Sheria za kuhamisha watu kutoka mji wa Gaza kwa mujibu wa sheria za kimataifa haziheshimiwi katika kesi hii, anachanganua François Dubuisson, profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha libre huko Bruxelles na mwanachama wa chama cha Jurdi – wanasheria kwa heshima ya sheria za kimataifa.
Israel yaimarisha operesheni zake za kijeshi
Katika muda wa wiki tatu zilizopita, Israel imeongeza mashambulizi yake ya anga huko Gaza na kuongeza operesheni kwenye viunga vya mji huu, ambao ni mkubwa zaidi katika eneo hilo linalokumbwa na njaa, kulingana na Umoja wa Mataifa. Kwa Bwana Netanyahu na washirika wake wa mrengo mkali wa kulia, lengo ni kukomesha Hamas, vuguvugu la Kiislamu la Palestina lililoanzisha vita mnamo Oktoba 7, 2023, na kuwarudisha mateka wote waliotekwa nyara siku hiyo.
Wakati huo huo operesheni za kijeshi za Israel ziliongezeka zaidi siku ya Jumamosi kwenye viunga vya mji huo.
Shirika la Ulinzi wa Raia la Gaza, shirika la huduma ya kwanza linalofanya kazi chini ya mamlaka ya Hamas tangu vuguvugu hilo liliponyakua mamlaka katika eneo hilo mwaka 2007, limeripoti mashambulizi makali ya Israel katika vitongoji vya Sabra (katikati) na Zeitoun (kusini mashariki) na “ongzeko la ghasia” katika kitongoji cha Sheikh Radwan (kaskazini).
“Takriban watu milioni moja wanaoishi katika eneo la Gaza hawana pa kwenda, hawana hata njia nyingine ya kutumia kuondoka katika mji huo,” Philippe Lazzarini, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNRWA), alisema siku ya Ijumaa. “Iwapo operesheni ya kijeshi itafanyika katikati ya raai (…) itakuwa janga kubwa.”