s

Maelfu ya watu wameandamana kote nchini Mexico kupinga hatua hafifu na dhaifu za serikali katika kukabiliana na tatizo la watu kutowekwa na kupotezwa na kulazimishwa kutoweka kwa nguvu.

Ndugu na marafiki wa watu waliopotea, pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, waliandamana mitaani katika Jiji la Mexico, Guadalajara, Córdoba na miji mingine wakitoa wito wa kupatikana kwa haki na kumtaka Rais Claudia Sheinbaum kusaidia katika kuwatafuta wapendwa wao waliopotea.

Zaidi ya watu 130,000 wameripotiwa kutoweka nchini Mexico tangu mwaka 2007, wakati Rais wa zamani Felipe Calderón alipozindua “vita dhidi ya dawa za kulevya”.

Katika visa vingi, waliopotezwa wamelazimishwa kujiunga na magenge ya dawa za kulevya au kuuawa wanapokataa.

Ingawa magenge ya dawa za kulevya na makundi ya uhalifu yaliyojipanga ndiyo wahusika wakuu, vikosi vya usalama pia vimehusishwa na vifo na kutoweka kwa watu.

Maandamano yaliyofanyika katika majiji, majimbo na Manispaa mbalimbali yalionyesha wazi jinsi tatizo la kutoweka kwa nguvu linavyoathiri familia na jamii kote nchini Mexico.

Kutoka kusini katika majimbo kama Oaxaca hadi kaskazini katika Sonora na Durango, wanaharakati na familia za watu waliopotea walijitokeza kwa maelfu wakiwa na mabango yenye picha za wapendwa wao, wakizitaka mamlaka kuchukua hatua madhubuti zaidi kukomesha tatizo hili.

Umoja wa Mataifa umelitaja jambo hili kama “janga la kibinadamu la kiwango kikubwa sana.”

Mexico sasa inakabiliwa na kiwango cha kutoweka kwa watu kinachozidi rekodi za baadhi ya nchi za Amerika Kusini.

Takribani watu 40,000 walipotea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Guatemala vilivyodumu kwa miaka 36 na kuisha mwaka 1996. Inakadiriwa kuwa 30,000 walipotezwa nchini Argentina chini ya utawala wa kijeshi kati ya mwaka 1976 na 1983.



Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *