Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool wamevunja rekodi ya soka ya Uingereza baada ya kufikia makubaliano na Newcastle United kumsajili mshambuliaji wa Kiswidi, Alexander Isak, kwa ada ya £125m. Dili hili linamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya Ligi Kuu England, likivunja rekodi ya usajili wa Florian Wirtz – £116m, iliyodumu muda mfupi, akisajiliwa msimu huu kutokea Bayer Leverkusen.
Isak anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya Jumatatu Septemba 01, 2025 kabla ya kusaini mkataba wa miaka sita Anfield. Liverpool walikuwa wamewasilisha awali ofa ya £110m mapema mwezi huu ambayo ilikataliwa, lakini mara hii wamerejea na dau kubwa zaidi lililowashawishi Newcastle kuachia mchezaji wao bora zaidi wa msimu uliopita.
Uhamisho huu unaashiria kutimia kwa malengo ya Liverpool chini ya kocha Arne Slot, ambaye alihitaji mshambuliaji mwenye kiwango cha juu ili kuendeleza mbio za kulinda taji la ligi. Kwa upande mwingine, Newcastle wanakabiliwa na changamoto za kifedha chini ya sheria za Financial Fair Play (FFP), hivyo dau hili kubwa limewapa nafasi ya kujipanga upya.
Kwa mashabiki wa Liverpool, usajili huu siyo tu taarifa njema , bali pia ni ishara kwamba klabu iko tayari kushindana na vilabu vinavyoongoza Ulaya. Kwa Arsenal ambayo imechapwa na Liverpool 1-0 katika mchezo wa ligi kuu Agosti 31, 2025 au Manchester CIty, hii ni changamoto mpya, kwani sasa wanakabiliana na timu ambayo imeongeza nguvu kubwa kwenye safu ya ushambuliaji.
Isak yupo wapi kwenye orodha hii?
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa ada ya £125m, Alexander Isak sasa anaongoza orodha ya usajili ghali England. Amewapiku Florian Wirtz (£116m), Moises Caicedo – £115m, Enzo Fernández – £106.8m na Declan Rice (£105m), hivyo ameingia rasmi sehemu ya juu Top 5 ya usajili ghali kabisa katika historia ya Uingereza.
Hii inamaanisha Liverpool wamevunja rekodi yao ya ndani pia. Awali, mchezaji ghali zaidi walikuwa wamemsajili ni Darwin Núñez kwa £85m kutoka Benfica mwaka 2022. Usajili wa Isak unaonesha ni kwa kiasi gani thamani ya wachezaji imepanda, huku klabu zenye historia kubwa zikilazimika kutoa fedha nyingi zaidi ili kupata wachezaji wa kiwango cha kimataifa.
Usajili huu pia ni ishara kwa mashabiki na wadau wa EPL: ligi ya England inaendelea kuwa kivutio kikuu cha wachezaji mashuhuri wa dunia.
Usajili 10 ghali zaidi katika historia ya Ligi Kuu England
Alexander Isak – £125m: Newcastle United hadi Liverpool, 2025
Florian Wirtz – £116m: Bayer Leverkusen hadi Liverpool, 2025
Moises Caicedo – £115m: Brighton hadi Chelsea, 2023
Enzo Fernández – £106.8m: Benfica hadi Chelsea, 2023
Declan Rice – £105m: West Ham hadi Arsenal, 2023
Jack Grealish – £100m: Aston Villa hadi Manchester City, 2021
Romelu Lukaku – £97.5m: Inter Milan hadi Chelsea, 2021
Mykhailo Mudryk – £89m: Shakhtar Donetsk hadi Chelsea, 2023
Antony – £86m: Ajax hadi Manchester United, 2022
Harry Maguire – £80m: Leicester City hadi Manchester United, 2019
Kila jina kwenye orodha hii linabeba simulizi kubwa. Fernández alisajiliwa baada ya kung’ara na Argentina kwenye Kombe la Dunia, Rice alihusishwa na klabu nyingi kabla ya Arsenal kumaliza dili, huku Grealish akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kiingereza kusajiliwa kwa £100m. Orodha hii pia inadhihirisha nguvu ya kifedha ya vilabu vya London, Manchester na Merseyside.
Kwa rekodi ya dunia Isak yuko wapi?
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa muktadha wa dunia, bado ada kubwa zaidi ya usajili inashikiliwa na Neymar, ambaye alihamia Paris Saint-Germain akitokea Barcelona kwa takribani £200m mwaka 2017. Usajili huo ulitikisa soka na kufungua ukurasa mpya wa ada kubwa zisizokuwa za kawaida, na hadi sasa haujavunjwa.
Kylian Mbappé naye alijiunga na PSG akitokea Monaco kwa zaidi ya £165m mwaka 2018, wakati Philippe Coutinho alihamia Barcelona kutoka Liverpool kwa karibu £142m mwaka 2018. Orodha hiyo ya juu inakamilishwa na Joao Félix, aliyesajiliwa na Atlético Madrid kutoka Benfica kwa £113m, na Ousmane Dembélé, aliyehamia Barcelona kutoka Borussia Dortmund kwa takribani £112m.
Kwa hivyo, ada ya Isak ya £125m inamweka nafasi ya nne kwenye orodha ya wachezaji ghali zaidi duniani. Anaingia moja kwa moja ndani ya tano bora, akipita majina makubwa kama Félix na Dembélé, na kubaki nyuma ya Neymar, Mbappé na Coutinho pekee. Hii inamaanisha kwamba sasa Isak siyo tu usajili ghali Uingereza, bali pia anakuwa sehemu ya historia ya dunia – mmoja kati ya wachezaji wachache waliofikia kiwango cha ada kinachovuka £120m.