Chanzo cha picha, Seenergy.ir
Baada ya vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran, baadhi ya wanasiasa na wataalamu nchini Iran waliibua wasiwasi kuhusu msimamo wa Urusi wakati wa vita hivyo, na ukosoaji huo umeendelea hadi leo.
Katika kadhia ya hivi punde zaidi, Mohammad Sadr, mjumbe wa Baraza la Utambuzi wa Mafanikio na Naibu Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni katika serikali ya Mageuzi hivi karibuni alidai kwamba “Huenda Urusi ikawa imeipatia Israel habari kuhusu mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran,” na katika muktadha huu, aliashiria usahihi wa mashambulizi ya Israel.
Katika matamshi yaliyochapishwa Septemba 1, 2025, kwenye chombo cha habari cha Synergy na video yake kupakiwa kwenye jukwaa la kushirikiana la Aparat, Bw. Sadr alisema: “Kuna mashaka kuhusu jinsi Israeli, katika vita vya hivi majuzi na katika migogoro ya hapo awali, ilivyokuwa na taarifa sahihi kuhusu vituo vyetu vya ulinzi wa anga. Kulingana na uchambuzi wangu, naweza kukuambia kwamba Warusi wameipatia Israeli habari muhimu.”
Alipoulizwa kama madai yake yalikuwa ya uchambuzi tu, Sadr alijibu: “Hii pia inatokana na habari.”
Makubaliano ya kimkakati na Urusi ‘yaligonga mwamba’
Katika mahojiano haya, Bw. Sadr alikosoa makubaliano ya kimkakati kati ya Iran na Urusi, na kuyataja kuwa ni “ulaghai” na kuilaani Moscow kwa kupeleka mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kwa Uturuki, mwanachama wa NATO, na kwa kutotoa mifumo sawa na ndege za kivita za Sukhoi kwa Iran.
“Mkataba wa Kimkakati ” kati ya Iran na Urusi unahusu ushirikiano wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi na ulitiwa saini mapema mwaka huu wakati wa ziara ya Rais wa Iran nchini Urusi.
Bwana Sadr alisema katika mahojiano yake: “Tunapaswa kuwa na uhusiano mzuri sana na Urusi, lakini tusiuamini.”
Sadr ni mwanadiplomasia mkongwe ambaye aliteuliwa katika Baraza la Utambuzi wa Ufanisi mnamo 2017 kwa amri ya Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kufuatia vita vya Israel na Iran mnamo Juni 1404, baadhi ya maafisa wa Iran walikosoa jukumu la Urusi. Idadi kubwa wa maafisa wa kisiasa wa Iran wanasema kwamba Urusi katika vita hivi ililaani tu mashambulizi na kutoa upatanishi, na haikutoa msaada wa vitendo kwa Iran.
Wakati wa vita vya siku 12, Kremlin ilitoa wito wa kupunguzwa kwa mivutano na kutoa upatanishi, huku pia ikisisitiza ushirikiano wake wa kina na Iran.
Ukosoaji wa Moscow nchini Iran haukomei kwenye vita vya hivi majuzi tu. Katika miaka ya nyuma, wakati wa uwepo mkubwa wa Iran nchini Syria, shutuma pia zilitolewa kwamba Urusi, kwa kushindwa kutumia mifumo yake ya ulinzi na uratibu wa kiusalama na Israel, ilikuwa imefungua njia kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya misimamo ya Iran.
Urusi ilikataa shutuma hizi na kuelezea sera yake kama kudumisha usawa kati ya wahusika.
Lawama hizo zinaonyesha kuwa licha ya kuwepo kwa ushirikiano mkubwa kati ya Tehran na Moscow, bado hali ya kutoiamini Urusi inaendelea katika anga ya kisiasa ya Iran.
Vyombo vya habari vya Urusi vilipokea maoni ya Bw. Sadr, vikisisitiza msimamo rasmi wa Moscow wakati wa vita: kulaani mashambulizi ya Israeli kama “yasiyo ya haki” na “haramu” na kujitolea kupatanisha kati ya Tehran na Tel Aviv.
Vladimir Putin alisema wakati huo Iran haikuomba msaada wa kijeshi na kwamba ushirikiano kati ya nchi hizo mbili haumaanishi muungano wa ulinzi.
Baada ya vita vya Iran na Israel, Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Umoja wa Ulaya lilisema katika uchambuzi kwamba huenda Urusi ikanufaika na Iran dhaifu, kwani hali hii inaizuia Tehran kukaribia nchi za Magharibi, ingawa ukosefu wa utulivu wa Iran pia ni hatari kwa Moscow.
Kwa kiwango kikubwa, wataalam wanasisitiza kwamba Urusi inasimamia mgogoro zaidi kupitia diplomasia na inajaribu kusawazisha ushirikiano wa kikanda na maslahi yake ya kimkakati.
Chanzo cha picha, Office of the President of the Islamic Republic of Iran via Getty Images
“Nilisema Israel ndiyo iliyosababisha kifo cha Ibrahim Raisi”
Katika hotuba yake, Bw. Sadr alisisitiza imani yake kwamba Israel ndiyo iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta.
Helikopta iliyokuwa imembeba Ebrahim Raisi ilianguka Mei 20, 1403, wakati ikirejea kutoka kwenye sherehe ya ufunguzi wa bwawa kwenye mpaka wa Jamhuri ya Azabajani.
Bw. Sadr alisema: “Wakati Bw. Raisi aliposhambuliwa, nilisema kwamba Israel ndiyo iliyosababisha kifo chake, ingawa kulikuwa na nadharia tofauti wakati huo.”
Uwezekano kwamba ajali ya helikopta ya Bw. Raisi ilifanywa kimakusudi hapo awali ilitolewa na baadhi ya viongozi na watu wa kisiasa nchini Iran.
Kamran Ghazanfari, mjumbe wa Bunge la Iran alisema mwezi uliopita wa Disemba: “Waungwana ndani hawaoni haja ya kutangaza kwamba Marekani na Israel, kwa ushirikiano na utawala wa Aliyev huko Azerbaijan, zilimuua shahidi rais, na wanahusika na wingu zito ambalo lilihusika tu na helikopta kuu.”
Idadi kubwa ya wanasiasa nchini Iran pia iliibua dhana ya kuhusika kwa Israel katika kuidungua helikopta ya Raisi baada ya operesheni ya Israel ambapo maelfu ya wapiganaji wa Hezbollah nchini Lebanon walilipuliwa na vifaa vya mawasiliano – pager.
Iran imefutilia mbali hitilafu yoyote ya kibinadamu au kushindwa kiufundi katika ajali hiyo ya helikopta, huku ripoti rasmi ikihusisha ajali hiyo na hali mbaya ya hewa.
Madai “ya uwongo na ya uchochezi”
Kauli za Bw. Sadr zilisababisha hisia katika siasa za Iran.
Esmail Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, alizungumzia kuhusu matamshi hayo wakati wa mkutano wake wa kila wiki, akisema kwamba matamshi ya Sadr ni “maoni yake binafsi” na “sio msingi wa ushahidi” na hayaakisi msimamo rasmi wa Iran.
Kuhusu kifo cha Ebrahim Raisi, Baqaei alisema kwamba ripoti rasmi ya serikali inasalia kuwa simulizi halali na kwamba ripoti hiyo inakataa “madai na uvumi” katika suala hili.
Malek Shariati, mwakilishi wa Tehran katika bunge, aliandika katika chapisho la X, lililoelekezwa kwa Ali Larijani, katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa: “Ikiwa dai hili ni la kweli, basi Urusi ijibu kwa uthabiti. Ikiwa ni uwongo, chukua hatua madhubuti dhidi ya spika. Usiruhusu usalama wa taifa kuwa mchezo.”
Ahmad Zeidabadi, mwandishi wa habari na mtoa maoni wa mageuzi, alionya kuwa upotoshaji wa taarifa zenye lengo hudhoofisha imani ya umma.
Gazeti hilo lenye misimamo mikali ya Kayhan pia lilisema kuwa kauli za Sadr “zinadhuru usalama wa taifa na sera ya kigeni” na kumshutumu kwa kutoa madai “ya uwongo na ya uchochezi”.
Kinyume chake, baadhi ya vyombo vya habari vya wanamageuzi na vya wastani vilikosoa jibu la Kayhan, vikielezea kama “uungaji mkono usio na masharti kwa Urusi” na “shambulio kali” kwa Sadr.
Shirika la Habari la Mizan linalohusiana na mahakama lilisema kwamba mwendesha mashtaka wa Tehran amefungua kesi ya kisheria dhidi ya mjumbe wa Baraza la Utambuzi wa Ufanisi, bila kumtaja Sadr.
Shirika la habari lilitangaza kwamba mtu huyo alishtakiwa na kuitwa kwa kutoa taarifa “za uwongo na zisizo na msingi”.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi