Huku kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025 zikianza kwa wagombea wa nafasi zote. Wagombea wa nafasi za urais wamejikita kuzinadi ahadi za kitaifa za vyama vyao kwenda wa wafuasi na wapiga kura kwa ujumla.
Katika kueleza ahadi kwa wapiga kura. Kuna wapiga kura wa aina mbili: Wale ambao ni wafuasi wa chama fulani kwa miaka mingi. Aina hii ya wapiga kura mara nyingi hawahitaji hata ahadi, tayari washaamua wao ni wapiga kura wa chama gani.
Kundi la pili, ni wale ambao huwafuatilia wagombea kupitia kampeni zao, husikiliza ahadi za wagombea na kisha hufanya maamuzi kura yao iende kwa mgombea yupi, kulingana na kuvutiwa na ahadi zao.
Makala haya yana lengo la kuzungumzia vyama viwili vikubwa, Chama cha Mapinduzi CCM na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kwa upande wa Tanzania bara. Ahadi zao kwa upande wa Zanzibar, ni mjadala wa wakati mwingine.
ACT Wazalendo, chama cha upinzani chenye ushawishi unaokuwa kwa kasi, bado mgombea wao wa urais bado hajapitishwa hadi wakati wa kuandaa hii makala.
Ahadi kuu za Chaumma
Chanzo cha picha, CHAUMMA
Sula la katiba mpya lipo katika ahadi za Chaumma, endapo itapewa ridhaa na wananchi kuunda serikali, imeahidi kuwasilisha bungeni muswada wa sheria kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kuandika Katiba mpya.
Pia Chaumma inaahidi kuwasilisha bungeni muswada wa kuundwa Tume ya Ukweli na Upatanishi, ili kufanya uchunguzi wa malalamiko mbalimbali ya wananchi, juu ya mauaji, utekaji na kupotea kwa wananchi, migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, kuyataja kwa uchache.
Katika swala la kupambana na umasikini, mkakati wao unaitwa ‘ubwabwa kwa wote,’ utakuwepo ili kuboresha mfumo wa lishe ni kuhakikisha taifa linaondokana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe.
Vilevile, inakusudia kuwasilisha bungeni muswada wa kufuta tozo zote zinazoathiri sekta ya kilimo na ufugaji. Ndani ya miaka mitano ya uongozi wao unaahidi kima cha chini cha mshahara ni Sh800,000 baada ya kodi.
Katika huduma nyingine za kijamii, wameahidi kudhibiti upotevu wa maji unaotokana na ubovu wa miundombinu.
Katika eneo la makazi, watahakikisha wanapunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi na kutoa motisha kwa wauzaji wa vifaa vya ujenzi.
Ahadi Kuu za CCM
Chanzo cha picha, CCM
Mbele ya maelfu ya wanachama na wafuasi wa CCM katika sherehe za ufunguzi wa kampeni za chama hicho, August 28, Kawe, Jijini Dar es salaam, rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM ametoa ahadi kadhaa za kitaifa, katika maeneo mbali mbali.
Katika eneo la afya CCM inaahidi, bima ya afya kwa wote, wagonjwa wa saratani, sukari, figo kugharamiwa na Serikali. Serikali itaajiri wahudumu wa afya wapya 5,000. Pia ni marufuku hospitali yoyote nchini kuzuia miili ya marehemu.
Katika kupunguza tatizo la uhaba wa ajira, CCM inaahidi itaajiri Walimu 7000. Serikali ya CCM itatenga Bilioni 200 ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa Wafanyabishara ndogondogo. Jingine ni uanzishwaji wa programu maalumu za mitaa ya wiwanda Wilayani zenye kulenga kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Kwenye huduma za kijamii CCM imeahidi itajenga gridi ya Taifa ya maji kwa lengo za kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji. Pia kuongeza matumizi ya Nishati safi ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ili kutunza mazingira.
Fupa la muda mrefu, katiba mpya. CCM imeahidi itaendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi, kwa kuunda Tume ya Kuanzisha Mazungumzo ya Maridhiano na Upatanishi na kuandaa mazingira ya kuanza kwa Mchakato wa Katiba Mpya.
Rais Samia maefupisha ahadi za CCM kwa kusema, “kwa ujumla kwa miaka 5 ijayo serikali ya CCM imejipanga kuongeza nguvu kwenye ubora wa huduma zinazotolewa kusimamia haki, amani na utulivu wa kisiasa ili tuweze kukuza uchumi na kuleta maendeleo na ustawi wa Taifa.”
Matumaini ya wananchi
Bila shaka kampeni za uchaguzi mara nyingi hutoa ahadi kedekede, na asilimia kubwa ya ahadi hizo ni nzuri. Ni mara chache sana kukutana ahadi mbaya za wanasiasa wakati wa kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Lakini utekelezwaji wa ahadi ni jambo jingine. Zipo ambazo zitatekelezwa na zipo ambazo zitabaki tu katika makaratasi na kumbukumbu za vyombo vya habari. Bila utekelezwaji wa aina yoyote. Kwa lugha nyingine, ni adimu sana kupata yote katika ahadi za wanasiasa.
Kwa ujumla ahadi zilizotolewa na vyama hivi viwili, zinakusudia kutatua matatizo ya kijamii. Ukosefu wa ajira, huduma za kijamii – na mambo mengine mengi. Lengo kuu ni kuboresha maisha ya Mtanzania.
Jambo jingine kubwa katika ahadi hizi, ni upatikanaji wa katiba mpya. Kwa hakika CCM imeshikilia makali katika suala hili, na ikiwa wataingia tena madarakani, bado wataendelea kuwa waamuzi wa mwisho juu ya katiba mpya.
Kwa vile wametoa ahadi ya kuendelea mchakato huo. Na Chaumma pia imetoa ahadi kuhusu upatikanaji wa katiba mpya. Hili linatoa matumaini kwamba yoyote atakayeingia madarakani, angalau kuna mategemeo ya mchakato wa katiba mpya kuendelea.