-
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC, Mbeya
Tahadhari: Makala hii ina maelezo ambayo baadhi wanaweza kuyaona ya kusikitisha!
Baada ya kutekwa akiwa amesimama kando ya moja ya barabara kuu katika jiji la Dar es Salaam, nchini Tanzania, mwanaharakati wa mitandaoni, Edgar Mwakabela, maarufu Sativa anasema aliponea chupuchupu kuuawa.
Anaeleza katika mahojiano na BBC namna gani baada ya kutekwa Juni 23, 2024 watekaji wake walimhoji na kisha kumsafirisha kwa zaidi ya kilometa 1,000 (maili 600), huku akipitishwa mikoa mbalimbali kabla ya kumtupa katika pori lililopo mkoani Katavi, jirani na mpaka wa Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Katika siku nne zilizofuata baada ya kutekwa, Sativa anasema alifungwa pingu, alifunikwa macho na kupigwa kikatili, ikiwemo kupigwa mara kwa mara kichwani, mgongoni na miguuni kwa kutumia ubapa wa panga.
“Kipigo nilichopewa kilinisababisha maumivu makali sana.”
Siku ya tano wakati mateso dhidi yake yakiendelea, alipelekwa katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi yenye wanyamapori hatari, kisha watesi wake wakamsogeza jirani na mto ambao una viumbe hatari. Anaamini ilikuwa dhahiri kuwa watekaji wake hawakuwa na nia ya kumwacha akiwa hai.
Kisha, ikasikika amri ya kutisha kutoka kwenye gari lililokuwa jirani na eneo hilo, “piga chuma!”
Akapigwa risasi, na mara moja ilipenya kwenye kichwa chake. Taya lake lilivunjika.
Watekaji wake wakaondoka, Sativa anaamini waliondoka wakidhani kwamba wamemmaliza.
Mkasa wake ni moja tu ya matukio kadhaa ya utekaji ambayo yameripotiwa Tanzania katika siku za hivi karibuni ambayo yameonekana kuwalenga wakosoaji wa serikali na wanaharakati wa upinzani. Tanzania inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, na matukio hayo kwa mujibu wa wachambuzi yanalenga kuzinyamazisha sauti za ukosoaji.
‘Kwanini unaikosoa serikali?’
Imekuwa kawaida katika siku za hivi karibuni kwa polisi au machapisho ya mitandao ya kijamii kutangaza taarifa za mtu kupotea. Baadhi huwa hawapatikani tena. Wengine hurudi wakiwa na simulizi za kutisha kuhusu ukatili au mateso waliyoyapItIa, lakini kuna wengine hupatikana wakiwa tayari wameuawa.
Mkasa wa Sativa unatoa simulizi adimu kutoka kwa mmoja wa watu walionusurika kufa baada ya kutekwa.
Licha ya kupata majeraha makubwa, aliweza kuzinduka na kisha kujikokota hadi barabarani ambako askari wa wanyamapori waliweza kumuona na kumpa msaada.
Bado anahitaji tiba zaidi ya muda mrefu kutoka kwa wataalamu, na kupona kwake kumeelezewa kuwa ni ‘maajabu’.
Sativa anaamini alikumbwa na madhila hayo baada ya kushiriki katika mgomo wa wafanyabiashara wa soko la kimataifa la Kariakoo mapema 2024. Ushiriki wa Sativa ulikuwa wa mtandaoni, akituma ujumbe kadhaa wa kuikosoa serikali.
Ameiambia BBC kuwa waliomteka, ambao anaamini walikuwa maofisa wa polisi au watu wanaohusiana na vyombo vya dola, walitaka kujua ni nani anayemwezesha kifedha kufanya harakati zake na kwa nini alikuwa akiikosoa serikali.
“Kiuhalisia sikutumwa kuwasemea wafanyabiashara. Nilifanya kwa utashi wangu. Waliamini ninatumwa na ninalipwa, kitu ambacho sicho,” Sativa ameiambia BBC.
Serikali inakanusha kuwa inawalenga wakosoaji na wapinzani.
Polisi hawakujibu maombi ya BBC ya kufanya mahojiano kuhusu suala hili, lakini katika taarifa ya video iliyotolewa mwezi Juni, Msemaji wa polisi, Kamishna Msaidizi David Misime alisema wanafanyia kazi taarifa kuhusu waliopotea na kuchunguza mazingira ya madai hayo.
BBC imezungumza na familia za watu walioripotiwa kupotea na wameeleza majonzi yao kutokana na kuwapoteza wapendwa wao.
Chanzo cha picha, The Citizen
Msanii wa sanaa ya uchoraji, Shedrack Chaula, mwenye umri wa miaka 25, hadi sasa hajulikani alipo.
Hajaonekana wala kusikika kwa zaidi ya mwaka mmoja. Juni 2024 alichapisha video kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa TikTok ambapo alionekana akichoma picha ya Rais Samia Suluhu.
Alikamatwa, kisha akashtakiwa na kuhukumiwa kwa kosa la unyanyasaji wa kimtandao, na kuachiwa baada ya kulipa faini.
Mwezi mmoja baadaye, alitekwa na watu wasiojulikana saa chache baada ya kufungua duka lake la biashara lililopo nje kidogo mwa jiji la Mbeya.
‘Tumefanya kila juhudi kumtafuta, tumechoka’
Baba mzazi wa Shedrack, Yusuf Chaula aliieleza BBC kuwa hawajui kijana huyo atapatikana lini kwani muda unazidi kwenda tangu alipotekwa.
“Hatujui atapatikana lini kwa sababu nao wanasema wanaendelea kuwatafuta na hawajui alipo.Laiti pale alipokuwa amefungwa, ilikuwa inajulikana alipo lakini sasa hivi hata mamlaka wanasema hayupo na hakuna anayemshikilia,” anasema Chaula.
Anasema Agosti, 2024, wanaume watatu waliwasili katika eneo zilipo biashara za msanii huyo, kisha wakateremka kwenye gari lenye vioo vyeusi na kumkamata na kisha kuondoka naye. Anasema watu hao hawakujitambulisha wala kueleza kwa nini au walikuwa wanampeleka wapi.
Chaula anasema, “tumefanya kila juhudi kumtafuta, tumechoka. Tumeenda kila mahali ambapo watu hushikiliwa. Tumeenda magerezani, vituo vya polisi vya ngazi mbalimbali, kuanzia kata, wilaya hadi mkoani. Hatujampata zaidi tunaambiwa wanafuatilia…”
Polisi wamesisitiza kusa uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.
“Kama tungejua yuko wapi, au anashikiliwa wapi, au hata kama tungejua amekufa na kuzikwa mahali fulani, angalau tungekuwa na kaburi la kutembelea,” anasema Chaula, huku akikosa majibu ya mahali alipo kijana wake.
Watu wengine kadhaa pia wameripotiwa kupotea, huku mamlaka zikisema zinafanya uchunguzi.
Juni 2025, wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliripoti kwamba zaidi ya matukio 200 ya watu kupotezwa kwa nguvu yameripotiwa nchini Tanzania tangu mwaka 2019.
Walieleza wasiwasi wao kuhusu mamlaka kuunyamazisha upinzani na wakosoaji, haswa kuelekea uchaguzi, hivyo kuitaka serikali isitishe hali hiyo mara moja.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch, hivi karibuni yaliishutumu serikali kwa kuhusika na ukamataji, ukatili na watu kupotezwa kwa nguvu.
Mamlaka zimekanusha tuhuma hizo.
Rais Samia: Polisi washughulikie watu kupotea
Polisi wamebaini angalau matukio kadhaa ya utekaji tangu mwaka jana, mengine yakiwa yameshapatiwa ufumbuzi. Baadhi ya matukio ni ya nyuma hadi mwaka 2019.
Juni 18, 2025 polisi walitangaza kuwa uchunguzi waliofanya ulibaini sababu za matukio hayo.
Walisema baadhi ya matukio yalihusisha utekaji ulioandaliwa na wahusika wenyewe, huku mengine yakitokana na uhusiano wa kimapenzi uliovunjika, imani za kishirikina na migogoro ya mali.
Msemaji wa Polisi, David Misime alisema, “matukio yote yaliyoripotiwa watu kupotea, uchunguzi bado unaendelea hadi pale ukweli utakapopatikana wa nini kilichowatokea watanzania wenzetu. Kwa upande wa matukio yaliyotokea na kuhusishwa na vitenndo vya utekaji na wahusika wake bado hawajapatikana…
“…jeshi la polisi linatoa wito kwa ndugu, jamaa na marafiki, kuendelea kuwa na utulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi ili kubaini uhalisia wa matukio hayo,” alisema Misime.
Rais Samia, katika hotuba yake ya kuvunja bunge alilitaka jeshi la polisi kukomesha matukio haya, agizo ambalo watanzania wengi wanatumaini litaleta haki, ingawa mustakabali wa waliopotea bado haujuliakani.
Mei 2025 mwanaharakati na mwanasiasa wa upinzani Mpaluka Nyagali maarufu Mdude Chadema alitekwa nyumbani kwake jijini Mbeya katika tukio la kikatili lililoshuhudiwa na mkewe pamoja na mtoto wao mchanga.
Michirizi ya damu ilisalia katika eneo la tukio, kuonesha kuwa shambulio dhidi yake lilikuwa la nguvu na kikatili.
‘Ninaomba mume wangu aachiwe’
Hadi sasa mke wa Mdude, Siji Mbugi, hajapata taarifa yoyote kuhusu alipo mume wake.
Siji aliiambia BBC, “Ilikuwa majira ya saa nane kasoro za usiku, mtoto alishtuka na kulia sana. Nikaamka na kumbembeleza na kumnyonyesha. Nikasikia pikipiki ikipita kisha muda huo huo, gari nalo likafika getini. Nikamwamsha mume wangu na kumwambia kuna watu wanafungua mlango. Muda mfupi walibomoa mlango na kuingia ndani.”
Anasema walitumia nyundo, na baada ya kuingia ndani mmoja alijitambulisha kuwa ni polisi, kisha alimtisha na kumtaka kurudi chumbani huku akimueleza kuwa hana shida naye bali walimtaka Mdude.
“Ninaomba mume wangu aachiwe, naamini anashikiliwa na polisi pamoja na mamlaka. Mdude hajafanya kosa lolote, hajawahi kuiba chochote kutoka kwa mtu yeyote, naomba sana aachiwe. Kama ana kosa basi mpelekeni mahakamani,” anasema Siji.
Julai 9, 2025 Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Mbeya ilitupilia mbali kesi ambayo Siji alikuwa ameIfungua dhidi ya polisi kuhusu kupotea kwa mumewe.
Aliieleza mahakama kuwa watu waliokuwa na silaha na kujitambulisha kama maofisa wa polisi walivamia nyumba yao usiku wa manane na kumshambulia Mdude kabla ya kumchukua na kuondoka naye huku akitokwa na damu nyingi.
Wakati shauri hilo likiendelea, polisi mkoa wa Mbeya walikiri kuwa walikuwa wanachunguza mmoja wa maofisa wao ambao alidaiwa huenda alihusika katika utekaji wa Mdude.
Wanaharakati wamesema kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo ni pigo kubwa katika harakati za kuendelea kutafuta haki nchini Tanzania.
Hakuna watu waliokamatwa au kufunguliwa mashtaka kuhusiana na matukio yanayodaiwa kuhusisha maofisa wa serikali, ingawa polisi wanasema uchunguzi unaendelea.
‘Hakuna mtu anayetoa majibu’
Baadhi ya wanaharakati wa ukanda huu wa Afrika Mashariki pia wameishutumu serikali ya Tanzania kwa kukiuka haki zao.
Boniface Mwangi raia wa Kenya na Agather Atuhaire wa Uganda, walisema walikamatwa na kuteswa baada ya kuwasili nchini Tanzania Mei, 2025.
Mwangi na Atuhaire walipotea kwa siku kadhaa.
Walikamatwa muda mfupi baada ya kuwasili Tanzania kushuhudia kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambaye kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Wote wawili walitelekezwa jirani na mipaka ya nchi zao.
Lakini Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, aliambia BBC kwamba madai hayo yalikuwa ni maoni ya wanaharakati hao na kwamba kama wangekuwepo nchini Tanzania angewahoji kwa kile walichodai.
Baada ya tukio hilo wamefungua kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kuhusu suala hilo.
Mateso waliyopitia yameweka wazi zaidi tatizo la kupotezwa kwa nguvu kwa wakosoaji wa serikali, wanasiasa wa upinzani na watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania.
“Hakuna mtu anayetoa majibu,” anasema Maduhu William, mwanaharakati wa haki za binadamu katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), akiongeza kuwa vyombo vya usalama mara kwa mara huahidi kufanya uchunguzi wa kina lakini jambo hilo huishia hapo bila majibu.
“Mwisho wa siku hatupati mrejesho wa kinachoendelea,” anasema, akitoa mfano wa Ali Kibao, ofisa mwandamizi wa Chadema, ambaye aliuawa mwaka 2024 baada ya kutekwa, kupigwa na kumwagiwa tindikali.
“Hata Rais (Samia) aliagiza vyombo vya usalama nchini Tanzania kufanya uchunguzi wa kina na kuwasilisha ripoti kwake kwa hatua zaidi. Lakini hadi sasa, hakuna kilichosikika,” anasema.
Boniface Mwabukusi, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), anasema watu wengi wanaogopa kujitokeza na kusimulia masaibu yao kwa hofu ya kutekwa au kuumizwa.
Anasema hakuna chombo huru, kisichopendelea upande mmoja, kisichoegemea upande wowote ili kuhakikisha haki inatendeka ipasavyo.
“Ikiwa uko mikononi mwa polisi na ndiyo watuhumiwa na hao hao maofisa wanakuomba utoe maelezo kuhusu utekaji wako, kweli unaweza kuwapa? Huwezi kutoa,” anasema.
Mwabukusi anasema, “Watu wengi huishia kusema wanamwachia Mungu. Wanaogopa, wanasema kama wakiendelea kusema kuhusu suala hili, mambo yatakuwa mabaya zaidi.”