Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
-
- Author, Angela Henshall
- Nafasi, BBC World Service
Suleyman Hammudan amezoea kuishi katika jiji lenye joto kali mno.
Anajihusisha na mauzo ya teknolojia ya habari (IT) huko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ambapo joto hupanda na kufikia zaidi ya nyuzi joto 45°C (113°F) kuanzia mwezi Juni hadi Septemba.
“Ukitembea nje wakati wa mchana, unahisi kana kwamba uko jangwani. Joto pamoja na unyevunyevu vinakuweka katika hali ya kukosa pumzi kabisa,” anasema.
“Kwa kawaida hufanya kazi nyumbani. Nikilazimika kutoka nje, huwa ni saa moja jioni jua linapotua lakini bado kuna joto, lakini si kali kiasi cha kushindwa kuvumilika.”
Wakati wa msimu wa kiangazi, ni nadra kuwaona watu wakitembea mitaani.
“Kwa hivyo, kwenda kazini kwangu huwa ni kutoka nyumbani hadi garini kisha ofisini,” anaongeza.
“Kila mahali kuna kiyoyozi hasa maduka makubwa ya jumla ambako watu hupendelea kukaa kwa muda mrefu. Maduka haya ya kibiashara yanakuwa kama nyumbani pa pili!”
Kama ilivyo kwa wengi wetu, Suleyman amelazimika kuzoea hali mpya ya maisha ya kila siku, inayokumbwa na joto ambalo awali halikuwahi kufikirika.
Wanasayansi wanachunguza kile kinachotokea ndani ya mwili wa binadamu unapokumbwa mara kwa mara na joto la juu.
Je, kuna athari za muda mrefu? Je, linaweza kubadilisha kabisa jinsi mwili wako unavyozeeka?
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Southern California (USC) ulichunguza athari za joto kwa maelfu ya raia wa Marekani waliokuwa wakiishi katika majimbo yenye hali tofauti za hewa, ambapo joto la kila siku lilipanda zaidi ya 32°C (90°F).
Kwa kutumia vipimo vya damu, watafiti walipima umri wa kibaolojia wa washiriki 3,600 ukilinganishwa na umri wao halisi, na kuyalinganisha matokeo hayo na taarifa za viwango vya joto (heat index).
Mwandishi wa utafiti huo, Dkt. Eunyoung Choi, mtafiti wa baada ya udaktari, alisema kuwa athari zilizobainika zilikuwa za kushangaza.
Watu waliokuwa wakikumbwa mara kwa mara na joto kali walionekana kuzeeka haraka zaidi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Je, kuna athari ya kudumu kwenye mwili wako?
Wanasayansi walikuwa tayari wanajua kuwa joto linaweza kuathiri kazi za ubongo, mfumo wa moyo na mishipa, pamoja na uwezo wa figo kufanya kazi.
Hata hivyo, matokeo ya USC yanaonyesha kuwa kukabiliwa kwa muda mrefu na joto kali kunasababisha mabadiliko ya kikemikali katikamsimbojeni yaani DNA hasa kupitia mchakato wa kuwasha au kuzima jeni.
“Kadri joto la mwili linavyopanda, lipidi (mafuta yanayozunguka seli) huanza kupoteza muundo wake wa kawaida kwa wakati halisi. Seli huanza ‘kuchambuka’ hali kama ile inayotokea unapopika yai na ganda lake kuvunjika,”
Anasema Jeff Goodell, mwandishi wa kitabu kinachoitwa The Heat Will Kill You First: Life and Death on a Scorched Planet.
Chanzo cha picha, Getty Images
Kasi ya kuzeeka kwa seli
Kila mtu anafahamu kuwa baadhi ya watu huzeeka haraka zaidi kuliko wengine.
Dkt. Choi anasema kuwa hali ya seli kudhibiti shughuli za jeni bila kubadilisha msimbojeni unavyofuatana ni mojawapo ya njia za kisasa za kupima uzee wa kibaolojia yaani, kiwango halisi cha uchakavu wa mwili katika kiwango cha seli.
“DNA ya mtu haibadiliki tangu kuzaliwa, lakini kuzima au kuwashwa kwa jeni hufanya kazi kama swichi ya kuwasha au kuzima vinasaba fulani yaani, kudhibiti namna ambavyo vinasaba vinafanya kazi,” anaeleza Dkt. Choi.
Vipimo vya damu hutumika kuchunguza mabadiliko haya kwenye kuzima na kuwasha msimbojeni (DNAm).
“Fikiria DNA kama ramani ya mwili wako, na methylation ni kama kibodi ya kudhibiti sehemu zipi za ramani hiyo zitumike,” anaongeza.
“Jambo muhimu hapa ni kuwa sasa tunajua kuwa mazingira yetu ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo, uchafuzi wa hewa, na sasa joto kali yana uwezo wa kubadili swichi hizo.”
Dkt. Choi anasema matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa ukiishi kwa eneo lina joto kwa muda mrefu huleta madhara makubwa sawa na tabia hatarishi kama vile uvutaji sigara au ubugiaji pombe kupita kiasi.
Ingawa kasi ya kuzeeka inaweza kuonekana kuwa ndogo miezi michache hapa na pale matokeo yake hujilimbikiza kwa muda.
Hata ongezeko dogo la uzee wa kibaolojia kila mwaka linaweza kuongeza miaka kadhaa ya kuzeeka mapema.
Matokeo? Huenda mtu akaanza kupata magonjwa ya uzee mapema zaidi, kama vile kisukari, shida za akili (kama kichaa), na magonjwa ya moyo.
“Tunaliangalia hili kama onyo la awali linalowapa madaktari muda murua wa kuingilia kati na kutoa matibabu mapema,” anasema Dkt. Choi.
Vipi kuhusu mvi na makunyanzi?
Kwahivyo, ukiishi mahali kuna joto kali kuna badilisha muonekano wa mwili wako?
Suleyman anaamini mwili wake umeanza kuzeeka haraka zaidi akiwa Dubai amegundua kuongezeka kwa mikunjo na mistari usoni.
“Kiangazi kilichopita nililazimika kumuona daktari baada ya kuchomeka vibaya sana na jua. Ngozi yangu iliharibika na hadi leo bado naona makovu,” anasema.
Ameanza kufanya utafiti kuhusu mafuta ya kujikinga na jua jambo ambalo halikuwa sehemu ya maisha yake alipokuwa akiishi London.
“Sasa ninaelewa kwa nini watu hutembea na miavuli mchana. Unapofika nyumbani, unahisi kabisa madhara ya kupigwa na jua kwa muda mrefu.”
Kupigwa kwa muda mrefu na mwanga wa ultraviolet (UV) kutoka jua huongeza mikunjo na uharibifu wa ngozi hali inayokufanya uonekane mzee zaidi.
Ingawa haijathibitishwa wazi kama jua pia huharakisha kukua kwa mvi baadhi ya wataalamu wa ngozi wanasema miale ya UV inaweza kuvuruga kazi ya seli zinazotoa rangi ya nywele (melanocytes).
Joto na unyevu pia huchochea magonjwa ya mfumo wa neva kama kifafa, kiharusi, uvimbe wa ubongo, ugonjwa wa mishipa ya fahamu (multiple sclerosis), na kipandauso.
Hali hizi huathiri uwezo wa kufanya mazoezi na kudhibiti uzito, hivyo kuongeza hatari ya matatizo mengine ya kiafya.
Chanzo cha picha, Getty Images
Nani anahitaji ulinzi zaidi kutokana na joto kali?
Katika utafiti mwingine mdogo uliofanyika Ujerumani mwaka 2023, Dkt. Wenli Ni, mtafiti wa afya ya mazingira kutoka Harvard T.H. Chan School of Public Health, alihusisha joto la juu na uzee wa haraka wa seli.
Utafiti wake ulihusisha uchambuzi wa kuwasha na kuzima kwa DNA katika kuhusiana na magonjwa ya uzee kama kisukari na unene.
“Tulibaini kuwa watu wenye kisukari na unene walikuwa wanazeeka haraka zaidi,” anasema.
“Wagonjwa wa kisukari walionekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na joto kali.”
Dk Wenli Ni anaongeza kuwa wakati kazi ya damu inapoonyesha kuzeeka kwa kasi katika seli hii ni alama kuu ya maisha na hatari ya kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari, moyo na mishipa, ugonjwa wa mapafu na ugonjwa wa neva pia.
Kuna mapungufu kwenye tafiti hizi.
Ingawa epijenetiki husaidia kuelewa mchakato wa uzee unaoharakishwa na mazingira, bado haibainishi moja kwa moja mifumo gani ya mwili inayoharibika zaidi ni figo, ubongo au moyo.
Chanzo cha picha, Getty Images
‘They’re going to have to change their lives’
Timu ya Dkt. Choi inapanga kuchunguza hili kwa kina zaidi.
Jeff Goodell alichochewa kuandika kitabu chake baada ya kufanya kazi huko Phoenix siku ambayo joto lilipanda hadi nyuzi joto 46°C (115°F).
Alipojaribu kutembea kuelekea mkutano wake, karibu azirai.
Bwana Goodell alitaka kuelewa ikiwa inawezekana kwamba uzoefu mmoja tu kama huo unaweza kubadilisha kimetaboliki.
Utafiti wa hivi majuzi wa wanyama katika panya ulionyesha hata kukabiliwa mara moja kwa tukio moja la joto kali lilikuwa na athari ya kudumu kwenye kimetaboliki ya panya huyo.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanapoongezeka, idadi ya siku za joto kali nchini Marekani zinaweza kuongezeka kwa siku 20 hadi 30 kote nchini katikati mwa karne, kulingana na Tathmini ya Kitaifa ya Hali ya Hewa ya nchi hiyo.
Majimbo ya kusini mwa Marekani tayari yanakabiliwa na msimu mrefu wa joto na inawasili mapema kila mwaka.
“Katika maeneo kama vile Texas watu hufikiria kuhusu [msimu wa joto] wakati wote,” Bw Goodell anasema.
“Wanajua kutoka majira ya joto mawili yaliyopita kwamba watalazimika kubadilisha maisha yao na kufikiria tofauti kuhusu jinsi wanavyofanya kazi na kuendelea na shughuli za kila siku.”
Bwana Goodell anasema kutokana na hilo tayari kumekuwa na mabadiliko yanayoonekana katika taarifa huku ufahamu wa umma kuhusu hatari za joto kali ukiongezeka.
Kuorodhesha nguvu za mawimbi ya joto kwa nambari zinazofanana na vimbunga kunazingatiwa, ingawa kipimo cha unyevu kinaweza kuhitajika.
“Habari za televisheni zilikuwa zikituonyesha msururu wa magari yakielekea ufukweni wakati wa joto kali,” asema.
Badala yake, watu wameanza kufikiria juu ya kuongezeka kwa joto kwa suala la “nguvu hatari, haswa kwa watu wanaolazimika kufanya kazi nje na watu wanaoishi katika majengo yasiyo na kihami,” anasema.
Kwa Bwana Goodell, mzozo wa hali ya hewa tayari umefungua mgawanyiko mkubwa.
“Tunabadilika katika hali ya vyama viwili: Waliopoa na wanaoungua,” anasema.
“Kwa upande mmoja, kuna maji, kivuli na kiyoyozi. Kwa upande mwingine, kuna jasho, mateso na hata, katika hali mbaya zaidi, kifo.”
Anadhani jambo muhimu zaidi ambalo wakaazi wa Texas wote sasa wanafahamu kuhusu joto “ni kwamba ni joto ni wimbi lenye nguvu na huwashambulia wale walio hatarini kwanza”.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid