.

    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC, Nairobi

Leo tunaangazia simulizi ya Catherine Mugure anayetuelezea changamoto za maisha alizokumbana nazo kutoka kwa mwenza wake..

Simulizi ya Catherine inaanzia alipokuwa chuo kikuu baada ya kukutana na mchumba wake. Alipata ujauzito jambo ambalo lilimlazimu kusitisha masomo yake.

Lakini kwa sababu wazazi wake walikuwa wakali hali ambayo ni kawaida kabisa kwa mzazi ambaye anamtakia binti yake mema, Catherine hakuwa na namna nyingine zaidi ya kwenda kuishi kwa mchumba wake ambaye sasa walikuwa wamekata shauri na kuanza maisha kama mke na mume.

Kwa Catherine, mchumba wake alikuwa rafiki yake wa karibu, kufa kuzikana. Alikuwa na uhakika kwamba ndiye anayemtaka kuwa naye maishani.

Lakini kuna jambo ambalo mchumba wa Catherine alilichukia sana.

“Alikuwa akisema yeye hangependa kuwa na bikira na wakati huo nilikuwa hivyo lakini kwa sababu ya maneno yake, sikuwahi kumwambia,” Catherine anasema.

Msichana huyo hakuwahi kujua kwanini mchumba wake hakupenda mtu ambaye ni bikira na yeye naye hakutaka kuharibu uhusiano wake.

Ilipofika siku ya kuzaliwa kwake, Catherine anasema aliamua kujitoa yeye mwenyewe kwa mchumba wake.

“Tukio hilo lilinifanya nikapoteza fahari yangu na pia nikapata ujauzito.

“Licha ya kwamba tulikosana vibaya baada ya mume wangu kugundua kuwa mimi ni bikira, mwaka huo huwa ninauchukulia kama nuksi, hatukuwa na budi zaidi ya kuanza kuishi pamoja kwa sababu tulikuwa tunatajaria mtoto,” Catherine anasema.

Alijifungua salama wasalmin wakati ulipowadia lakini mume wake hakuja wakati anajifungua na pia alianza tabia zisizoeleweka.

“Alikuwa akilewa sana na kuja nyumbani kuchelewa. Kila tulipozungumza kuhusu suala hili, mume wangu alikuwa akisema nilimdanganya,” Catherine anakumbuka.

Ila ugomvi ukazidi na Catherine, kwa mara ya kwanza kabisa akaamua kutoroka kwake nyumbani, mtoto alipokuwa na takriban miezi sita.

Catherine alipata mtoto akiwa na umri wa miaka 21 na wakati wanakosana, mume wake alikuwa akimuambia, siku akiamua kuondoka asijaribu kwenda na mtoto wake kwa sababu atakufa.

Maisha yalikuwa kama kawaida, mumewe asijue kumbe Catherine alikuwa ameamua kutoroka.

Alimuomba mume wake ruhusa ya kwenda nyumbani na akamkubalia lakini cha kwanza alichomuuliza ni kuwa, utaniachia mtoto? Na hivi ndivyo alivyomjibu.

“Ukitaka nikuachie, nitakuachia lakini nataka kwenda kuzungumza na baba yangu ili anirudishe chuo kikuu,” Catherine anasema.

Hiyo ndio sababu aliotoa ya kutaka kwenda kwao lakini moyoni mwake alijua fika kwamba, anatoroka. Mume akatoka na kumsindikiza mkewe aliyemruhusu kumbeba mtoto wake.

Mwanamke huyo anasema, alipofika nyumbani mama yake alishutuka kumuona anaingia kwao akiwa na begi la nguo.

Ila alipoulizwa alisema ameenda kufua kwa sababu kwake maji yamepotea kwa muda.

“Asubuhi niliingia kuoga na kuanza kujitayarisha kabla ya kuondoka. Niliacha barua ambayo pia nilikuwa nimeiwacha kule kwa mume wangu bila yeye kujua. Kisha nikawacha maji yakimwagika bafuni ili watu wajue kuwa bado ninafua”

“Nilitoka nikiwa nimemuacha mtoto wangu amelala kitandani”

“Waliposoma barua na kuanza kunitafuta, nilikuwa nimezima simu. Walinitafuta hadi kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti kwa sababu kwenye barua nilikuwa nimeandika, nikiendelea kukaa na mtoto nitamuua au nijiiue,” Catherine anasema.

Nilipomuuliza Catherine kama alimaaniisha alichosema, “Msongo wa mawazo, ukiwa na msongo wa mawazo hakuna ambacho huwezi kufanya,” alisema.

“Nilizima simu kwa miezi mitatu,” Catherine anaendelea kuzungumza huku akilia.

Na kipindi hicho, alikwenda kwa rafiki yake ambaya alimpa makazi kwa muda na akasahau kabisa kwamba alikuwa na mtoto.

Kadiri alivyokuwa anaendelea kupoteza mawazo ndivyo alivyojipanga upya atakavyoanza tena safari ya maisha, akiwa peke yake.

Pia unaweza kusoma:

Na baada ya hiyo miezi mitatu, Catherine alifungua simu yake.

“Mama yangu alikuwa wa kwanza kunipigia. Alianza tu kulia huku akisema angalau ningemwambia kile kinachoendelea”.

Huo ukawa mwanzo wa mawasiliano na familia yake na kutengana na mume wake kwa kipindi cha miaka miwili.

Ingawa Catherine alisonga mbele na maisha, siku moja alikutana naye mjini katika duka moja akiwa anauza simu.

“Nilikuwa ninaita wateja kununua simu, ‘hi darling, hi babie’, njoo nikuuzie simu, ghafla nikamuona aliyekuwa mume wangu na nikashtuka. Kwa sababu sikutarajia na nina imani hata yeye hakutarajia.”

Alimuambie amuuzie simu na kuanzia hapo akawa anampitia kila siku. Wanakwenda kunywa kahawa kabla ya kila mmoja kwenda alipokuwa anaishi.

“Lakini muda si muda, Catherine alijipata akiwa na ujauzito wa mtoto wa pili.”

“Ilikuwa rahisi kurudiana tena naye kwa sababu alikuwa akituhudumia kila kitu.”

Wakaamua kumchukua mtoto aliyekuwa anaishi na bibi yake na kuanza maisha pamoja.

Lakini amini usiamini, hata baada ya wao kupata fursa ya kurejeleana na kuishi kama familia. Bado matatizo yalikuwa yale yale.

Na baada ya kipindi kifupi walianza tena kugombana ila safari hii haikuchukua muda mrefu sana kabla ya kuachana tena kwa mara ya pili.

Machungu niliopitia nikiwa na ujauzito wa tatu

.

Licha ya kwamba walikuwa na changamoto zao kama mtu na mwenza wake. Aliyekuwa mume wake Catherine hakuacha kuwahudumia.

Hili lilimpa fursa ya kutembelea familia hiyo kila alipotaka kufanya hivyo.

Na hivyo ndivyo Catherine alivyojipata na ujauzito wa mtoto wa tatu wa mume huyo huyo.

“Kwa sababu ya kile ambacho nimepitia kwa mtoto wa kwanza na wa pili, nilikuwa nimeamua kuwa sitazaa tena mtoto mwingine na yeye.

“Baada ya kufanya vipimo, nilihakikisha kuwa nimepata mimba nyingine ya tatu.”

Catherine alianza kupata matatizo ya kiafya. Alikuwa na kisukari na shinikizo la damu lakini akilini mwake tayari alikuwa amepanga kuwa ujauzito huo atautoa.

Baada ya kwenda hospitali, taarifa alizopata hakuamini alichokisikia.

“Huu ujauzito huwezi kuutoa, na ukijaribu utakufa. Umebeba mapacha na pia una ugonjwa wa ‘fibrosis’,” daktari alimwambia.

Hapo ndio mambo yalipobadilika kabisa. Licha ya kwamba daktari alimshauri kulea ujauzito na kumfajiri, mume wa Catherine alizua mengine mapya baada ya kuarifiwa kuwa safari hii ni mapacha.

“Mimi kwetu hakuna mapacha na kwenu hakuna mapacha kwa hivyo hawa watoto sio wangu.”

Hilo ndio lililokuwa jibu la mume wake Catherine. Na huo ndio ukawa mwanzo wa matatizo ya mama huyo.

Akikaribia miezi sita, alianza kutoka maji kumbe watoto walikuwa wanatoka. Ikabidi akimbilie hospitali na kufanyiwa upasuaji wa ghafla. Mtoto wake wa kwanza na wa pili, pia alikuwa amefanyiwa upasuaji.

Alipata mapacha wake, lakini kufikia asubuhi, mmoja alikuwa ameaga dunia.

“Niliambiwa niende ‘nursery’ kuangalia watoto, nilipofika hapo nikaona mmoja yuko kwenye meza, tayari ameshafariki dunia. Mwingine alikuwa anaendelea vizuri”.

Mume wake aliwaacha hospitali akiwa ameenda kujifungua.

“Nilikataliwa na mume wangu kwa sababu ya kuzaa mapacha na hajawahi kurejea hadi wa leo,” Catherine anasema.

Safari ya kupona majeraha ya moyo

Baada ya kutoka hospitali, Catherine aliwezaje kusonga mbele na maisha yake?

“Kidogo nirukwe na akili. Karibu hata niwauwe watoto wote watatu. Lakini Mungu amenipa nguvu.”

Pacha aliyesalia, madaktari walikuwa wamesema hatakuwa na muda mrefu wa kuishi kwa sababu aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa moyo lakini sasa hivi ametimiza miaka mitatu.

Catherine anawaomba kina mama wengine, wakisakate tamaa.

“Nguvu yako iko kwenye fikra zako,” Catherine anasema.

Kwa sasa, amesonga mbele na maisha yake huku akiendelea kulea wanawe.



Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *