Chanzo cha picha, Getty
-
- Author, BBC News Nepali
- Nafasi,
- Author, Emily Atkinson
- Nafasi, BBC News
- Author, Iftikhar Khan
- Nafasi, South Asia Regional Journalism
Waziri Mkuu wa Nepal, KP Sharma Oli, amejiuzulu kufuatia hasira kali ya umma baada ya vifo vya watu 22 waliouawa kwenye makabiliano kati ya polisi na waandamanaji waliokuwa wakipinga ufisadi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi yake, kujiuzulu kwake kumelenga kufungua njia ya kupatikana kwa suluhisho la kikatiba kufuatia maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana, yaliyosababishwa na tuhuma za ufisadi uliokithiri na marufuku ya mitandao ya kijamii ambayo sasa yameondolewa.
Maandamano hayo yaligeuka kuwa ya vurugu siku ya Jumatatu, baada ya maelfu ya waandamanaji wengi wao wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maandishi kuwa ni vijana wa kizazi cha Gen Z, Waliingia barabarani jijini Kathmandu.
Inakadiriwa kuwa watu takriban 200 walijeruhiwa katika makabiliano hayo, ambapo polisi walitumia gesi ya kutoa machozi, magari ya maji ya kuwatawanya waandamanaji, na hata risasi za moto.
Waandamanaji walivamia kuta za jengo la bunge na majengo mengine ya serikali.
Siku ya Jumanne, maandamano yaliendelea kwa kasi, huku waandamanaji wakichoma moto jengo la bunge, makao makuu ya Chama cha Congress cha Nepal, na nyumba ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Sher Bahadur Deuba.
Nyumba za viongozi wengine wa kisiasa pia zilivamiwa na kuharibiwa.
Hiki ndicho tunachojua kuhusu maandamano haya kufikia sasa.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Marufuku ya mitandao ya kijamii ilikuwa nini?
Mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku kwa Waneplali, na taifa hilo lina kiwango cha juu zaidi cha watumiaji wa mitandao barani Asia Kusini.
Maandamano haya yalianza baada ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mitandao 26 ya kijamii, ikiwemo WhatsApp, Instagram na Facebook, kwa kile ilichodai ni kushindwa kwa majukwaa hayo kujisajili na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Nepal kufikia tarehe ya mwisho.
Wakosoaji walitafsiri hatua hiyo kama jaribio la serikali kuzima harakati za kupambana na ufisadi, kwa kunyima wananchi fursa ya kuwasiliana na kujieleza.
Marufuku hiyo ilifutwa rasmi Jumatatu usiku.
Hata hivyo, marufuku hiyo imeelezwa kuwa ni kielelezo tu cha hali ya kukatishwa tamaa kwa muda mrefu na viongozi wa serikali na mfumo wa utawala nchini humo na ndio imechochea maandamano kufikia hapa.
Ni nini kinaendelea kote Nepal?
Maandamano yamesambaa kutoka Kathmandu hadi miji mingine, na siku ya Jumatatu pekee watu 19 waliuawa kwenye makabiliano na polisi.
Waziri wa Mawasiliano, Prithvi Subba, aliiambia BBC kuwa polisi walilazimika kutumia nguvu, ikiwemo maji ya kuwatawanya waandamanaji, virungu, na risasi za mpira ili kudhibiti hali.
Waandamanaji walivamia eneo la bunge, hali iliyowalazimu polisi kuweka amri ya kutotoka nje katika maeneo ya serikali na kuongeza ulinzi mkali.
Jumanne, bunge lilichomwa moto jijini Kathmandu, huku moshi mzito ukifuka hewani.
Majengo ya serikali na nyumba za viongozi wa kisiasa pia zilishambuliwa maeneo mbalimbali ya nchi.
Idadi ya waliouawa imefikia watu 22, huku hospitali za jiji zikielezwa kupokea majeruhi wengi waliopigwa risasi za moto na mpira.Hii ni baada ya wanahabari wa BBC wa Nepal kuuliza madaktari aina ya majeraha wanayoyatibu,
Polisi nao wameripotiwa kupata majeraha, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.
Tazama hapa
Nani anaongoza Nepal kwa sasa?
Jumanne jioni, Mkuu wa Jeshi la Nepal, Jenerali Ashok Raj Sigdel, alitoa taarifa akiwalaumu waandamanaji kwa kutumia machafuko hayo kuharibu na kupora mali ya umma na binafsi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, iwapo hali ya machafuko itaendelea, taasisi zote za usalama ikiwemo Jeshi la Nepal “zitachukua hatua za kudhibiti hali hiyo.”
Wakati huohuo, Jenerali Sigdel alitoa mwito kwa waandamanaji kujitokeza kwenye meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhisho la pamoja kwa mzozo mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miongo mingi.
Hata hivyo, haijafahamika bayana nani anasimamia serikali kwa sasa.
Taarifa ya jeshi haikufafanua iwapo litatumia nguvu zaidi, ingawa askari wake tayari wapo mitaani kudhibiti hali na kuwakamata wanaojihusisha na uporaji na uharibifu.
Pia, haijulikani nani atawakilisha waandamanaji katika mazungumzo, kwani maandamano haya hayajaongozwa na kiongozi au kikundi maalumu.
Yalianza kama harakati huru zilizoanzishwa kupitia mitandao ya kijamii.
Kiongozi pekee wa kisiasa aliyewasilisha uungaji mkono wake kwa waandamanaji ni Meya wa Jiji la Kathmandu, Balen Shah, ambaye amekuwa akihimiza utulivu kupitia mitandao yake ya kijamii.
Chanzo cha picha, Getty Images
Waandamanaji ni akina nani?
Maandamano haya yamechochewa kupitia mitandao ya kijamii na kuongozwa na kizazi kipya cha vijana Gen Z hali isiyowahi kushuhudiwa nchini Nepal.
Ingawa hakuna kiongozi rasmi, vikundi vya vijana vimeibuka kama nguvu ya kuhamasisha na kuratibu harakati kupitia mitandao, huku wakitoa wito wa maandamano na kueneza taarifa mtandaoni.
Wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Kathmandu, Pokhara na Itahari waliombwa kushiriki wakiwa na sare na vitabu mikononi, ishara ya kuonyesha kuwa ni watu walio na elimu wanaotaka mabadiliko.
Video zinazoenezwa mitandaoni zinaonyesha hata watoto wa shule za msingi wakishiriki maandamano haya kwa ari kubwa.
Chanzo cha picha, Getty Images
Matakwa ya waandamanaji ni Yepi?
Waandamanaji wana madai mawili makuu:
- Kufutwa kwa marufuku ya mitandao ya kijamii – jambo ambalo tayari limetekelezwa.
- Kukomeshwa kwa vitendo vya kifisadi miongoni mwa viongozi wa serikali.
Wengi wa waandamanaji ni wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao wanasema marufuku hiyo ilikiuka uhuru wa kujieleza na kuathiri elimu yao kwa kuwazuia kufikia masomo ya mtandaoni.
“Tunataka kuona mwisho wa ufisadi nchini Nepal,” Binu KC aliiambia BBC, mwanafunzi wa miaka 19. “Viongozi huahidi mengi wakati wa uchaguzi lakini hawatimizi. Wao ndio chanzo cha matatizo yetu.” Aliongeza kuwa marufuku ya mitandao ilivuruga elimu yake na uwezo wa kujisomea.
Mtengenezaji maudhui, Subhana Budhathoki, aliongeza kwa hasira: “Gen Z haitarudi nyuma. Hii si tu kuhusu mitandao ya kijamii, ni kuhusu kunyimwa haki ya kutoa maoni, na hatutaruhusu hilo kuendelea.”
Chanzo cha picha, Getty Images
Nini maana ya “NepoKids” na uhusiano wake na maandamano?
Moja ya vipengele vya kipekee vya maandamano haya ni matumizi ya alama za mitandaoni kama #NepoBaby na #NepoKids.
Kauli hizi ziliibuka baada ya video zilizosambaa mtandaoni hasa Tiktok kuonyesha maisha ya anasa ya familia za wanasiasa, zikiwemo safari za kifahari, magari ya bei ghali, na mavazi ya kisasa, yote kwa kutumia mali ya umma.
Waandamanaji wanadai kuwa familia hizo zinaishi maisha ya kifahari bila kustahili, huku vijana wa kawaida wakikabiliwa na ukosefu wa ajira, umasikini na uhamiaji wa kulazimishwa.
Kauli hizo sasa zimegeuka kuwa nembo ya mapambano dhidi ya ukosefu wa usawa wa kijamii.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Nini kinaweza kutokea baadaye?
While the prime minister has stepped down, it’s not clear who will replace him – or what happens next, with seemingly no-one in charge.
Some leaders, including ministers, have reportedly taken refuge with the security forces.
Pamoja na Waziri Mkuu kujiuzulu, bado haijulikani ni nani atachukua nafasi hiyo au ni hatua gani serikali itachukua kurejesha utulivu.
Ripoti zinasema baadhi ya viongozi wa serikali, wakiwemo mawaziri, wamekimbilia kwenye kambi za vikosi vya usalama kwa hofu ya usalama wao.
Waandamanaji wamepuuza amri ya kutotoka nje iliyowekwa Kathmandu na viunga vyake.
Waandamanaji wanatoa wito wa uwajibikaji na mageuzi katika utawala.
Hata hivyo, ikiwa serikali itashindwa kujihusisha kikamilifu, wachambuzi wanaonya kwamba machafuko yanaweza kuongezeka zaidi, hasa wanafunzi na mashirika ya kiraia yanajiunga.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid
