Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Sean Kearns
- Nafasi, BBC Sport
Soka ya Uingereza iko hatarini kupoteza kizazi cha makocha wenye asili ya Kiafrika, Kiasia au mchanganyiko wa asili mbalimbali, kwa mujibu wa shirika la kupinga ubaguzi la Kick It Out.
Kutimuliwa kwa Nuno Espirito Santo na klabu ya Nottingham Forest wiki hii kunamaanisha kuwa kwa sasa hakuna tena meneja mwenya asili ya kiafrika anayesimamia klabu yoyote katika Ligi Kuu ya Uingereza.
Mara ya mwisho Ligi Kuu ya Uingereza kuwa bila meneja mwenye asili ya kiafrika ilikuwa kati ya mwezi Machi na Agosti 2023, baada ya kuondoka kwa Patrick Vieira kutoka Crystal Palace na kabla ya Vincent Kompany kupandisha Burnley daraja hadi ligi hiyo.
“Hili ni suala ambalo limekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja, na wapo wachezaji wa zamani waliokata tamaa ya kuwa makocha au mameneja,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kick It Out, Samuel Okafor.
“Tunatambua kwamba vipaji kutoka jamii mbalimbali vinapatikana, na klabu zinapaswa kuwa wazi na waadilifu katika taratibu zao za ajira.
“Hatuwezi kuruhusu kizazi kingine kipotee kwa sababu ya ukosefu wa hatua za pamoja na zilizoratibiwa.”
Mpango wa Football United wa Kick It Out, uliozinduliwa mapema mwezi huu, unalenga kushughulikia ukosefu wa uwakilishi katika nafasi za uongozi ndani ya klabu za soka, kwani hazionyeshi taswira ya jamii zinazozizunguka.
Ripoti ya mwaka 2022 kutoka Black Footballers Partnership ilibaini kuwa asilimia 43 ya wachezaji wa Ligi Kuu ya Uingereza walikuwa weusi lakini ni asilimia 4.4 tu ya nafasi za ukocha kwa wachezaji wa zamani zilijazwa na waombaji wa asili ya Kiafrika.
Katika nafasi za juu kama vile uongozi wa utendaji na umiliki wa klabu, takwimu hiyo hushuka zaidi hadi asilimia 1.6.
Aliyekuwa meneja wa Chelsea, Ruud Gullit, alikuwa meneja wa kwanza mweusi kuiongoza klabu ya Ligi Kuu alipoteuliwa kuwa mchezaji-meneja wa Chelsea mwaka 1996.
Kiungo wa zamani wa England, Paul Ince, alikuwa Mwingereza mweusi wa kwanza kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa klabu ya Ligi Kuu alipokabidhiwa majukumu ya kuinoa Blackburn mwaka 2008.
Ashvir Singh Johal hivi karibuni alikua meneja wa kwanza Msikh katika soka ya kulipwa nchini Uingereza baada ya kuteuliwa na klabu ya Morecambe.
Chama cha Soka (FA) kilizindua mpango wa Football Leadership Diversity Code mwaka 2020, kwa lengo la kuongeza uwakilishi wa watu wa jamii mbalimbali katika nafasi za uongozi wa juu, uendeshaji wa timu na ukocha kwenye klabu za soka kote nchini.
Zaidi ya klabu 50 ikiwemo 19 kutoka Ligi Kuu ya Uingereza zilisaini mpango huo.
Hata hivyo, baada ya klabu nyingi kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa, FA ilianzisha Kanuni N mwaka 2023, inayozitaka klabu zote kuchapisha taarifa za utofauti wa wafanyakazi wao mara mbili kwa mwaka, zikijumuisha vigezo kama vile umri, jinsia, mwelekeo wa kingono, utambulisho wa kijinsia, ulemavu, na kabila.
Ingawa FA imeanzisha programu kadhaa kama vile England Elite Coach Programme ili kuleta utofauti katika ajira za ukocha, bado ina ushawishi mdogo katika mchakato wa moja kwa moja wa ajira ndani ya klabu.
Ligi Kuu ya Uingereza ilianzisha mpango wa No Room For Racism Action Plan mwaka 2021, ambao unalenga kuongeza nafasi kwa watu wenye asili ya Kiafrika, Kiasia na jamii nyingine za walio wachache.
Mpango huo unafadhili programu mbili kuu za ujumuishaji wa makocha, Professional Player to Coach Scheme na Coach Inclusion and Diversity Scheme, ambazo husaidia makocha kutoka makundi yenye uwakilishi mdogo kupata nafasi za kazi.
Zaidi ya makocha 80 wameshiriki katika programu hizo, huku 75 kati yao wakiajiriwa katika nafasi za muda wote tangu programu hizo kuanzishwa miaka minne iliyopita.