Chanzo cha picha, Reuters
Riek Machar
amekuwa chini ya kizuizi cha nyumbani tangu Machi
Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amefunguliwa mashtaka ya mauaji, uhaini na
uhalifu dhidi ya binadamu hatua ambayo baadhi ya watu wanahofia inaweza kuzusha
vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Waziri wa Sheria
Joseph Geng Akech alisema mashtaka dhidi ya Machar yanahusiana na shambulio la
mwezi Machi na wanamgambo wanaodaiwa kuhusishwa na makamu wa rais.
Barabara
zinazoelekea kwenye nyumba yake katika mji mkuu, Juba, zimefungwa na vifaru na
wanajeshi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Vikosi vinavyomtii Machar vilipigana vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano dhidi ya vile vinavyomuunga mkono Rais Salva Kiir hadi makubaliano ya amani ya 2018 yanayomaliza mapigano katika nchi hiyo mpya zaidi duniani.
Bwana Machar amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu mwezi Machi, huku Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na nchi jirani zikitoa wito wa utulivu.
Makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yalimaliza mzozo uliosababisha vifo vya takriban watu 400,000, hata hivyo uhusiano kati ya Machar na Kiir umezidi kuwa mbaya huku kukiwa na mivutano ya kikabila na ghasia za hapa na pale.
Wengine saba wameshtakiwa pamoja na Machar, akiwemo Waziri wa Petroli Puot Kang Chol na Naibu Mkuu wa Majeshi Lt Jenerali Gabriel Duop Lam, Waziri wa Sheria Joseph Geng Akech alisema katika taarifa.
Wote ni washirika wa Machar ambao walikamatwa kwa wakati mmoja na yeye na pia wamekuwa kizuizini tangu wakati huo. Washukiwa wengine 13 bado hawajakamatwa, waziri alisema.