Chanzo cha picha, GP
-
- Author, Na Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC Swahili
- X,
Ni msimu wa siasa za uchaguzi katika mataifa ya Afrika Mashariki. Tanzania ikiwa inatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu nayo Uganda ikiifuata nyuma mnamo Januari 12 2026. Kenya bado ina muda, kwani inatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu Agosti 2027.
Na japo Kenya ina miaka miwili kabla ya kuandaa uchaguzi mkuu, vijana kadhaa wamejitokeza na kutangaza rasmi azimio lao la kumrithi Rais William Ruto.
Uchaguzi Mkuu Kenya 2027
Idadi ya watia nia wenye matarajio ya kumuondoa madarakani Rais William Ruto inaongezeka kila uchao nchini Kenya, jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wa siasa wanahisi huenda likaleta changamoto kubwa kwa juhudi za kumng’atua madarakani kupitia kura.
Ruto ambaye atakuwa anawania kiti hicho kwa awamu ya pili atamenyana na vijana wenye umri ulio chini ya miaka 45 ikiwa vijana hao watatimiza kanuni za tume huru ya uchaguzi nchini Kenya IEBC.
Boniface Mwangi
Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyependekeza kutaka kuwania kiti hicho hivi maajuzi ni mwanaharakati na mwandishi wa Habari Boniface Mwangi.
Mwangi atakumbukwa sana hasa nchini Tanzania kwa alivyokamatwa pamoja na mwanaharakati mwenzake Agather Atuhaire wa Uganda , wawili hao walipokuwa nchini humo kuhudhuria kesi ya mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu anayekabiliwa na shtaka la uhaini.
Mwangi ambaye alijipatia umaarufu mkubwa nchini Kenya kwa kunakili kumbukumbu za machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 kupitia picha, amefanya kazi na vyombo kadhaa vya Habari nchini Kenya kama mpiga picha na hata amechapisha kitabu chenye kazi yake katika miaka ambayo alifanya kazi katika vyombo vya Habari nchini Kenya.
Na hii sio mara yake ya kwanza kuwania kiti cha kisiasa, mnamo 2017 aliwania kiti cha eneo bunge la Starehe jijini Nairobi kupitia tiketi ya chama cha Sisi kwa Sisi ambapo alipiga kampeni tofauti ya kuwafuata wapiga kura walipo mitaani kwa miguu au mara nyingine akiwa anaendesha piki piki.
Wakati huo alichangisha pesa za kampeni yake kwa kuwaomba wapiga kura kutoa shilingi kumi za Kenya sawia na senti 77 dola za kimarekani. Alifanikiwa kuchangisha milioni tano chini ya wiki moja, hela ambazo aliahidi kueleza jinsi zilivyotumika kwenye kampeni yake.
Na katika siku ya kuadhimisha miaka 15 tangu kuasisiwa kwa katiba mpya nchini Kenya – Agosti 27 – Mwangi alitangaza ari yake kuwania kiti cha Urais nchini Kenya akisisitiza kwamba taifa liko tayari kwa uongozi wa vijana wenye uadilifu na utakaozingatia sheria za nchi na haki kwa wote.
“Viongozi wetu wameshindwa kuwajibikia majukumu yao na kuwafaa Wakenya katika njia mbali mbali. Tunalipa kodi na bado tunalazimika kulipa mlungula kwa ajili ya kupata huduma muhimu. Kwa hilo, nimesimama mbele yenyu, kutangaza kwamba ni wakati wa taifa letu kurejea mikononi mwetu kama raia.” Alisema katika hafla ya uzinduzi wa kampeni yake.
Mwangi amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali za Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na sasa William Ruto na amekamatwa na kufunguliwa mashtaka kadhaa ya uchochezi mbali na kuandaa maandamano.
Mwezi Juni mwaka 2025 alikamatwa nyumbani kwake , COURAGE BASE katika kaunti ya Machakos ambapo polisi walikagua pia ofisi zake mtaani Kilimani na kupata mabomu ya kutoa machozi na Maganda ya risasi.
Na japo upande wa serikali ulitangaza kwamba angeshtakiwa na Uhaini, ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya ummma ilimshtaki kwa kumiliki silaha kinyume bila ya kuwa na kibali rasmi.
Mwangi ni miongoni mwa kundi la vijana wenye mtazamo wa kwamba ni wakati wa vijana kuchukuwa nafasi yao katika uongozi wa taifa na kujihusisha na yaliyo juu ya meza badala ya kusubiri kualikwa au kupata misaada ya mara kwa mara.
Morara Kebaso
Wengine ambao wametangaza azma yao ni kama vile mwanaharakati Morara kebaso, ambaye alitangaza uamuzi wake wa kuwania kiti cha Urais mwezi Novemba 2027. Kebaso ni mjukuu wa mwanasiasa wa zamani George Kebaso aliyewahi kuwa mbunge katika miaka ya 90 nchini Kenya.
CMP Prezzo
Jackson Ngechu Makini maarufu kama CMB Prezzo ni mwanamuziki mashuhuri nchini Kenya mwenye nyimbo za kufoka kama vila ‘NALETA ACTION’ miongoni mwa mengine mengi.
Makini, amesajili chama chake Chama cha mabadiliko ambacho anasema kimepata motisha kutoka kwa msukumo wa vijana wa GEN Z nchini Kenya walipoandaa maandamano kupinga sera za serikali ya Rais William Ruto.
Peter Salasya
Chanzo cha picha, Salasya facebook
Mbunge wa Mumias Mashariki katika kaunti ya Kakamega nchini Kenya – Peter Kelerwa Salasya ana umri wa miaka 37. Alifanya kampeni yake ya ubunge kwa kutembea vijijini kuwabishia wapiga kura milango yao majumbani mwao na kutumia baiskeli au pikipiki kuuza sera zake.
Na mwezi Aprili 2025 alitangaza nia ya kuwania Urais akijitanagaza kama kiongozi kijana ambaye anakabiliana na uongozi wa wazee ambao haujawafaidi Wakenya.
Babu Owino
Paul Ongili Owino maarufu Babu Owino sio mgeni katika siasa. Aliwahi kuzua utata nchini Uganda alipomkashifu Rais Museveni ambaye alimuonya Rais Ruto kwamba hatokubali, ‘Tabia mbaya’ kusafirishwa hadi Uganda.
Ongili ni mbunge wa eneo bunge la Embakasi East kwa sasa na mwanachama wa ODM ambacho ni chama kinachoongozwa na Raila Odinga.
Alitangaza nia ya kumenyana na Gavana wa sasa wa Nairobi Johnson Sakaja ila kwa sasa anaonekana kuashiria kwamba huenda akataka kumrithi William Ruto.
Atakuwa na kibarua kigumu hasa katika chama chake kupata tiketi ambayo kinara wa chama Raila Odinga pia atakuwa anapigania.
Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025
Kampeni rasmi zimaanza nchini Tanzania, ambapo vyama 17 vimepata idhini ya kuwania viti mbali mbali vya kiasaia kutoka Udiwani hadi Urais.
Wagombea zaidi ya 14 wameidhinishwa kumenyana na Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan ambaye anawania kusalia madarakani baada ya kurithi kiti hicho kufuatia kifo cha John Pombe Magufuli – Rais wa awamu ya tano.
Na kama mataifa Jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki vijana kadhaa wamejitokeza kupigania kiti hicho cha Urais nchini Tanzania.
Salum Mwalimu
Salum ambaye ni katibu Mkuu wa chama cha CHAUMA ameidhinishwa kupigania kiti hicho Oktoba 29.
Yeye ni mzaliwa wa Zanzibar kama Mama Samia Suluhu Hassan . Amehudumu kama mgombea mwenza wa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa 2020. Aliwania kiti cha Ubunge huko Kiwanjani mwaka 2015 na uchaguzi mdogo wa Kinondoni mwaka wa 2018 bila mafanikio.
Chama Cha Wananchi (CUF) kimemsimamisha Gombo Samandito Gombo akiwa na mgombea mwenza Husna Mohamed Abdalla. NCCR- Mageuzi kitawakilishwa na Haji Ambar Khamis pamoja na Dkt. Eveline Wilbard Munisi,
Katika chama cha UDP, mgombea ni Saum Hussein Rashid, mgombea mwenza ni Juma Khamisi Faki. Chama cha TLP amethibitishwa Yustas Mbatina Rwamugira na Amana Suleiman Mzee. Chama cha DP amepitishwa Abdul Juma Mluya akiwa na Sadoun Abrahman Khatib, wakati chama cha TADEA kimemsimamisha Georges Gabriel Bussungu kuwania urais na Ali Makame Issa kama mgombea mwenza.
Chama cha UMD, kitawakilishwa na Mwajuma Noty Mirambo akiwa na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji. UPDP kimmepitisha Twalib Ibrahim Kadege na Abdalla Mohamed Khamis. NRA imemteua Hassan Kisabya Almas kuwania urais na Hamis Ali Hassan mgombea mwenza, huku chama cha MAKINI kikiwa na mgombea urais Coaster Jimmy Kibonde na mgombea mwenza Azza Haji Suleiman.
Chama cha NLD kitawania urais kupitia Doyo Hassan Doyo pamoja na Chausiku Khatib Mohamed kama mgombea mwenza, wakati SAU kimemsimamisha Majalio Paul Kyara kupeperusha bendera ya chama hicho na Satia Mussa Bebwa. CCK kimempitisha David Daud Mwaijojele na mgombea mwenza Masoud Ali Abdala, huku chama cha AAFP kikiwa na Kunje Ngombare Mwiru kama mgombea urais pamoja na Chumu Abdallah Juma, mgombea mwenza.
Uchaguzi Mkuu Uganda 2026
Vyombo vya Habari nchini Uganda vina ripoti idadi mbalimbali za watu waliochukuwa karatasi za kuwania Urais nchini humo mwezi Januari mwakani.
Kwa jumla kuna wagombea kati ya 51 na 114 waliochukuwa fomu hiyo kwa ajili ya kumenyana na Yoweri Kaguta Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miongo minne na anawania awamu ya saba uongozini.
Museveni atakuwa anakabiliana na wapinzani ambao walijaribu awali na kushindwa naye mbali na kundi jipa la vijana wa rika la Gen Z ambao wana uchu wa kufanya mabadiliko katika taifa lao.
Roberto Ssentamu Kyagulani
Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamuziki na mwnaharakati ‘Bobbi Wine atakuwa ana jaribu kwa mara ya pili kumrithi Rais Museveni madarakani. Wine mwenye umri wa miaka 43 amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Museveni n ahata kutumia muziki wake kueneza uanaharakati wake unaopinga uongozi wa kiimla na kutaka haki kutendeka kwa wote.
Kwa mfano wimbo wake Dembe alioutoa mwaka wa 2016 akitaka mabadiliko nchini Uganda kupitia uongozi bora. Ameendeleza injili ya mabadiliko nchini Uganda katika wimbo wake ZUKUKA alioshirikiana na msanii NUBIAN LI .
Lakini ni wimbo wake wa lugha ya Luganda unaofahamika kama FREEDOM ambao ulionekana kuikashifu vikali serikali ya Museveni. Wine amejipata pabaya na mamlaka nchini Uganda .
Amewahi kumamatwa na kukabiliwa na mashtaka ya uhaini mnamo 2018 katika mahakama ya kiraia muda mfupi baada ya kuachiliwa huru na mahakama ya kijeshi.
Wine ambaye alikulia katika mitaa ya mabanda katika eneo ambalo aliliwakilisha bungeni la Kyadondo East alipochaguliwa 2017 kama mbunge wa kujitegeme huru.
Kwa sasa ni kinara wa chama cha NUP ambacho anatarajia kukitumia tena kuwania Urais mwakani akiwa na matumaini makubwa kwamba atafanikiwa.
Bobbi kama anavyofahamika miongoni mwa mashabiki wake amekashifiwa na Mkuu wa Jeshi la Uganda UPDF – Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye amewahi kumtishia maisha ‘Kabobi’ kupitia ujumbe aliouchapishwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
Jenerali alikuwa akimuonya Wine kwamba atamzuia kama alivyofanya dereva wake na kunfanya alien a kujiendea haja kama alivyomfanya Eddi Mutwe ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini tangu 2021.
Wine hatokuwa kijana wa kipekee ambaye anatarajia kuwania Urais nchini humo, kunao vijana wa rika la Gen Z ambao wamejitokeza kuchukuwa karatasi za kujiandikisha kama watia nia.
Voniter Nassanga
Binti huyu mwenye umri wa miaka 20 ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha Kampala International. Anasema kwamba kampeni yake itazingatia haki za kina mama wanaolewa Watoto kama wazazi wa pekee na kujaribu kuinua hadhi yao katika jamii na kuboresha hali yao ya kiuchumi.
Deogratius Akampurira
Kijana huyu mwenye umri wa miaka 24 ni mwanafunzi wa chuo kikuu anayesomea Uanasheria katika chuo cha Uganda Pentecostal na alizaliwa katiak wilaya ya Rukungiri. Amemtaka Rais Museveni kujiuzulu madarakani akimtaja kama kiongozi aliyeshindwa kukabiliana na ufisadi ambao umekithiri Uganda kwa miaka 39.
Ayeza Abigail Victoria
Huyu ni binti mwenye umri wa miaka 22 na mwanafunzi wa chuo kikuu . Na jap oni miongoni mwa watia nia wenye umri mdogo zaidi katika Uchaguzi huo mkuu, amekiri kwamba uamuazi wake haujapokelewa vyema na wazazi wake ambao wanahishi kwamba anajiweka katika hali ya hatari kwa maisha yake. Lakini anasisitiza kwamba ana uchu wa kuleta mabadiliko katika jamii.
Jorine Najemba
Binti huyu mwenye umri wa miaka 20, ni mwanafunzi wa kidato cha sita ambaye anafanya mtihani wake wa mwisho baadaye mwaka huu. Kampeni yake ameielezea kama , ‘Mlango uliowazi na unaotoa nafasi ya raia kuingia ndani ya Uganda mpya inayowajali wote.’
Wengi wa wanaotaka kumrithi Rais Museveni wanasema kwamba uongozi wa Uganda katika siku zijazo umekwamishwa na kizazi cha sasa cha wanasiasa na mfumo wa uongozi uliopo na ni muhimu kwa vijana kuchukuwa nafasi yao katika siasa za nchi na kuhakikisha kwamba uongozi wa taifa hilo unaweka mikononi mwao.