[ad_1]
Chanzo cha picha, BBC Sport
Ninahisi kama najirudia kila ninapozungumzia matatizo ya Manchester United lakini mambo yale yale yanaendelea kutokea.
Wanafanya makosa yale yale, na hata si vigumu kuzuia.
Nimetazama kila dakika ya mechi nne za Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu na bila shaka kuna maeneo ya maboresho, ambayo inaonekana kuwa jambo la kushangaza kusema baada ya kupoteza mchezo wa 3-0.
Nimeangazia masuala ya mfumo wa Ruben Amorim wa 3-4-2-1 tangu alipoanza kuinoa Old Trafford msimu uliopita, na mimi si shabiki wa sura hiyo, lakini wameufanyia kazi na unaweza kuona.
Wanaonekana kuwa wagumu zaidi kama timu sasa, wakati wanashambulia au kulinda lango. Wanakuwa katika umbo zuri kabisa na umbali kati ya wachezaji ni mdogo zaidi, hatua ambayo huwafanya kuwa vigumu kuwachezea.
Bahati mbaya kwa Amorim, maboresho waliyoyafanya huko yamepuuzwa kutokana na makosa ya kipumbavu ambayo wanayafanya na kusababisha kufungwa mabao ambayo yanawapotezea pointi.
Ninapoangalia baadhi ya mabao ambayo wameruhusu msimu huu, likiwemo bao la kwanza la Phil Foden kwa City kwenye Uwanja wa Etihad siku ya Jumapili, wanazingatia masuala ya uteuzi, na wachezaji kutumika katika nafasi wasiofaa, badala ya mfumo wenyewe.
Chanzo cha picha, Getty Images
‘Bao la rahisi la Foden ndio lililoweka tofauti’
Kipindi cha kwanza dhidi ya City, United walifanya vyema. Walishinda mipira dhidi ya mabeki wa City mara nne au tano mbele na wangeweza kufunga mabao.
Mojawapo ya matatizo ya 3-4-2-1 ya Amorim ni viungo wawili wanaoshikilia nafasi ya kati wanaweza kuzidiwa lakini hilo halikufanyika kwenye Uwanja wa Etihad kwa sababu Bryan Mbeumo na Amad Diallo, ambao walikuwa wakicheza kila upande wa Benjamin Sesko, walishuka ili kusaidia safu ya ulinzi
Timu ilifunga mashimo katikati hatua ambayo ilimsaidia Bruno Fernandes na Manuel Ugarte katika safu ya kati, ndio maana hakukuwa na mapungufu makubwa.
Mara nyingi safu ya ulinzi na safu ya kati ziliwasiliana na kushirikiana vyema badala ya safu ya ulinzi kushuka kama walivyofanya msimu uliopita kwa sababu ya kukosa kasi au kujiamini.
City haikufanikiwa kuwavuruga United ili kuwasambaratisha, na sivyo walivyofunga bao lao la kwanza pia.
Kilichotokea ni kwamba Fernandes, ambaye bila shaka ni mmoja wa wachezaji bora zaidi katika nambari 10 duniani, anacheza nafasi ya kiungo ya kati kama nambari nane wakati uwezo wake sio kuweka ulinzi bali kushambulia .
Hatua ya Foden ya kuchukua mpira na kurudi nyuma nao kulimfanya Fernandes kupotea.
Chanzo cha picha, BBC Sport
Ndio, unaweza kubishana kwamba Luke Shaw angefanya vyema zaidi wakati mpira ulikuwa kwenye eneo la goli lakini Foden yuko huru kufikia hatua hiyo, kwa sababu Fernandes alipotea
Kama nilivyoangazia kwenye Mechi ya Siku, anatazama mpira wakati krosi inapofika katika lango. Sidhani ni mvivu, kwa sababu amerudi kwenye nafasi yake.
Hajazoea kuona washambuliaji na kuona hatari.
Chanzo cha picha, EPA
Hiyo ni mara ya pili Fernandes amesababishia United kufungwa goli msimu huu, kwa sababu pia alishindwa kumfuatilia Emile Smith Rowe kwa bao la kusawazisha la Fulham wakati United walipodondosha pointi kwenye Uwanja wa Craven Cottage mwezi Agosti.
Ajabu ya Fernandes dhidi ya City ilikuwa kwamba baadhi ya vipengele vya uchezaji wake katikati ya uwanja vilikuwa vyema sana.
Sio jambo la kijinga kabisa kumchezesha pale, kwa sababu ya pasi zake kutoka nyuma kwa washambuliaji mbele yake, na ni mchezaji bora kiufundi na jasiri akiwa na mpira.
Tatizo ni nini kinatokea bila yeye. Mchezaji mwenye akili kama yake anapaswa kujifunza kurudi nyuma katika hali ya ulinzi, lakini hilo ni wazi halifanyiki.
Huwezi kucheza katika nafasi hiyo ikiwa makosa hayo yanatokea mara kwa mara hivyobasi ni wakati wa kocha kutambua tatizo hilo na kuingiza wachezaji wanaofanya vyema zaidi.
Nani wa kulaumiwa?
Fernandes sio mchezaji pekee wa United ninayemtazama na nadhani ni kigingi cha mraba kwenye shimo la duara.
Shaw amecheza nafasi ya beki watatu hapo awali na ametumia muda wake mwingi kama beki mahiri wa kushoto na anahisi kama anapewa nafasi ya beki wa kati chini ya Amorim.
Tena unaweza kubishana anatakiwa kuwa na ubora wa kubadilika mara kwa mara, na kwa Jeremy Doku kumpita kirahisi na kusababisha goli la kwanza ilikuwa ni ulinzi mbovu uwe beki wa kushoto au kiungo wa kati, lakini iwapo kuna wachezaji ambao hawafurahii majukumu yao mapya, basi itaathiri timu.
Bao la pili la City, halikusababishwa na mfumo wa United, zaidi ilikuwa mchanganyiko wa mambo – na wingi wa makosa ya watu binafsi.
Ugarte anamkaba Foden lakini kisha anafuata mpira, kama alivyofanya katika hatua ya City iliyosababisha bao lao la kwanza, na kwenda kumzuia Nico O’Reilly, akimuacha Foden kufunga.
Kutoka hapo ilikuwa msururu wa makosa..
Noussair Mazraoui anatoka na Foden lakini hawezi kumzuia anapotoa pasi karibu na kona, Leny Yoro anazungushwa na Doku – mchezaji ambaye anajua ni matata kumkaba – halafu Shaw hana nguvu au kasi ya kutosha kumzuia Erling Haaland.
Hatimaye, mabao mengi yanatokana na makosa fulani lakini wakati wachezaji wanafurahia mfumo, na katika nafasi nzuri ndani yake, hufanya mambo sahihi – na makosa hayawi mengi kama tunavyoona na United.
Nini kinafuata? Kitu kile kile kitaendelea kutokea…
Chanzo cha picha, PA Media
Lazima tukumbuke kwamba mwanzo wa United hadi msimu haukuwa wa kutisha – walipaswa kuishinda Arsenal, waliwafunga Burnley na watahisi walikuwa na nafasi za kutosha katika kipindi cha kwanza dhidi ya Fulham kufanya kazi hiyo pia.
Lakini walipatikana dhidi ya City, na kadri kipindi cha pili kikiendelea wangeweza kufunga mabao zaidi.
Tunajua kwa sasa Amorim hatabadilisha mfumo wowote lakini anajiletea matatizo yake mengi kwa kuchagua wachezaji wasiofaa katika nafasi za mfumo huo .
Bado nadhani Fernandes kama nambari 10, akiwa na viungo wawili wanaomsaidia nyuma yake, ni mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani lakini inaonekana ni vigumu kupata nafasi ya kuionyesha United ubora wake.
Ikiwa United itaendelea kuchezesha wachezaji wale wale katika mfumo uleule – ikiwa ni pamoja na Fernandes katika safu ya kati, jukumu ambalo hajacheza vya kutosha kulielewa – basi mambo yale yale tunayoona labda yataendelea kutokea.
Ni nadra sana wachezaji kubadili fikra zao uwanjani kiasi hicho na huku wakiwa hawana uwiano huo, wataendelea kujipata katika hali mbaya
Danny Murphy alikuwa akizungumza na Chris Bevan wa BBC Sport.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla
[ad_2]
Source link