Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa
Marekani Donald Trump amesema siku ya Jumatatu kuwa hakujulishwa na
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mapema kuhusu shambulizi la Israel
nchini Qatar wiki iliyopita.
Maoni ya
Trump yanatolewa baada ya ripoti ya Axios kusema kuwa Netanyahu alimfahamisha
rais wa Marekani kuhusu shambulizi hilo muda mfupi kabla ya kutokea.
Utawala wa
Trump umesema uliarifiwa tu baada ya makombora kurushwa angani, na hivyo kumnyima
Trump fursa ya kupinga shambulizi hilo.
Axios
iliripoti, ikiwanukuu maafisa wa Israeli, kwamba Ikulu ya Marekani ilijua
mapema, hata ikiwa muda wa kusitisha shambulizi hilo ulikuwa kidogo.
Israel ilifanya
shambulizi la kujaribu kuwaua viongozi wa kisiasa wa Hamas kwa shambulizi
la anga nchini Qatar siku ya Jumanne, na kuzidisha hatua yake ya kijeshi Mashariki
ya Kati.
Shambulizi
hilo lilishutumiwa pakubwa Mashariki ya Kati na kwingineko kama kitendo ambacho
kinaweza kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo ambalo tayari linakumbana na
changamoto zake.
Awali, Trump
alisema hakuhusika katika uamuzi wa Israel kuivamia Qatar.
Alipoulizwa siku
ya Jumatatu ikiwa Netanyahu alizungumza naye moja kwa moja kumtahadharisha kuwa
Israel itavamia viongozi wa Hamas nchini Qatar, “Hapana, hapana, hawakunijulisha,”
Trump alisema.
Ofisi ya
Netanyahu ilisisitiza baada ya Axios kuripoti kwamba shambulizi hilo lilikuwa
operesheni “huru kabisa” ya Israeli.