
Serikali ya Yemen imekemea vikali viongozi wa Kiarabu na Kiislamu kwa kushindwa kuchukua hatua za kivitendo katika kuunga mkono Palestina na kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni, ikisisitiza kuwa utawala huo wa kibeberu huelewa tu lugha ya nguvu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imebainisha masikitiko yake kuhusu matokeo ya mkutano wa dharura wa Kiarabu-Kiislamu uliofanyika Qatar, kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya viongozi wa harakati ya Kiislamu ya mapambano ya Palestina, Hamas, waliokuwa wakikutana mjini Doha wiki iliyopita.
Wizara hiyo iliongeza kuwa mkutano huo haukuzingatia kwa kina tishio kwa umma wa Kiislamu ambalo linasababishwa na utawala wa Israel, wala haukuchukua hatua madhubuti za kuilazimisha Israel kuheshimu sheria za kimataifa na kusitisha mashambulizi na mzingiro dhidi ya Gaza.
Aidha, wizara ilibainisha kuwa wananchi katika nchi za Kiarabu na Kiislamu walikuwa wakitarajia kwa hamu hatua kali kutoka kwa mkutano huo, kama vile kukatiza mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara na Israel, kuweka vikwazo vya kina, kushinikiza kuvunja mzingiro wa Gaza, na kuunga mkono mapambano ya Wapalestina na wapiganaji wao jasiri.
Wizara hiyo iliongeza: “Kushindwa kwa mkutano huo kutoa maamuzi ya kivitendo na madhubuti kunazidi kuupa ujasiri utawala wa Kizayuni kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza, na mashambulizi dhidi ya mataifa ya ukanda huu.”
Wizara hiyo pia ilisisitiza kuwa tajriba imeonyesha wazi kuwa utawala wa Israel huelewa tu lugha ya nguvu, na kwamba hatua za kivitendo na misimamo thabiti ni muhimu katika kudai haki.
Zaidi ya hayo, Yemen ilithibitisha tena msimamo wake thabiti wa kuunga mkono Gaza na watu wake, ikiahidi kutumia kila njia na rasilimali zilizopo, na kujitolea kwa hali yoyote ile, hadi uvamizi na mzingiro wa kikatili dhidi ya Gaza utakapokoma.
Mnamo Septemba 9, utawala wa Israel ulishambulia kwa makombora eneo la makazi mjini Doha, ukilenga wanachama wa Hamas waliokuwa wakijadili pendekezo la Marekani kuhusu kusitisha mapigano Gaza. Viongozi wakuu wa Hamas walinusurika, lakini wanachama watano wa harakati hiyo kutoka Gaza na afisa mmoja wa usalama wa Qatar waliuawa.
Jumatatu, mkutano wa dharura wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu ulifanyika katika mji mkuu wa Qatar kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya viongozi wa Hamas mjini Doha. Viongozi hao walithibitisha kuunga mkono kwa dhati suala la Palestina na kulaani vitendo vya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Hata hivyo, mkutano wa Doha ulimalizika kwa maneno makali tu, bila kuchukuliwa hatua madhubuti za kivitendo na mataifa ya Kiislamu dhidi ya utawala dhalimu wa Israel.