Leo ni Alhamisi tarehe 25 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na Septemba 18, 2025.
Miaka 1011 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijria aliaga dunia faqihi mkubwa na mashuhuri wa Kishia Sayyid Murtadha Alam al Huda mwanafunzi mtajika wa Sheikh Mufid akiwa na umri wa miaka 80. Sayyid Murtadha Alam al-Huda, ambaye nasaba yake inafika hadi kwa Imam wa Saba, Imam Musa al Kadhim AS alizaliwa Baghdad, Iraq mwezi Rajab mwaka 355 Hijria. Alianza kuhudhuria darsa na masomo ya Sheikh huyo akiwa pamoja na kaka yake Sayyid Razi.
Miongoni mwa sifa za darsa za Sayyid Murtadha Alam al Huda ni kwamba watu wa itikadi zote waliweza kuhudhuria darsa zake na kunufaika na elimu na mafunzo mbalimbali.

Katika siku kama ya leo miaka 316 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza.
Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.

Katika siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba 1947, Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilianzishwa.
CIA ni miongoni mwa mashirika ya kijasusi ya kutisha sana duniani, na lina jukumu la kukusanya na kuchambua taarifa kuhusu serikali za nchi za kigeni, makampuni na watu binafsi na kuripoti taarifa hizo kwa serikali ya Marekani.
Shirika hili lilichukua nafasi ya Idara ya Huduma za Kimkakati, ambayo iliundwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kuratibu shughuli za kijasusi kati ya matawi mbalimbali ya jeshi la Merekani.
Shirika la CIA, lenye idara na taasisi nyingi na pana, kama wakala wa ujasusi wa serikali ya Marekani, huwasaidia viongozi wa nchi hiyo katika kuingilia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi ya nchi zingine.
Hadi sasa shirika hilo limehusika na mapinduzi ya serikali katika nchi mbalimbali zinazojitawala. Miongoni mwa mapinduzi hayo ni yale ya tarehe 28 Mordad 1332 Hijria Shamsia (19 Agosti 1953) nchini Iran kwa kushirikiana na shirika la ujasusi la Uingereza MI6.
Baada ya tukio la Septemba 11, 2001 lililoharibu majengo pacha (Twin Towers) huko New York, CIA ilipewa jukumu rasmi na la wazi la kuwateka nyara au kuwaua wapinzani wa Marekani duniani kote.

Na siku kama ya leo miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 27 Shahrivar mwaka 1367 Hijria Shamsia, aliaga dunia, Ustadh Muhammad Hussein Shahriyar mshairi mashuhuri wa Kiirani.
Alizaliwa mjini Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran na baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari katika Chuo cha Dar al-Funun mjini Tehran alijiunga na chuo cha tiba. Hata hivyo baada ya miaka michache aliacha masomo na kurejea katika kijiji alichozaliwa.
Ustadh Shahariyar alitoa mashairi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23. Sambamba na kushadidi harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Shahriyar aliungana na wimbi hilo kwa kutumia mashairi yake.
Vilevile alikuwa mashuhuri sana kwa kumpenda Mtume wa Ahlubaiti zake na mapenzi hayo yalidhihiri katika tungo na mashairi yake.
