
Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa wanajeshi wanne wa utawala wa kizayuni wa Israel wameangamizwa na wengine wanane wamejeruhiwa katika mripuko wa bomu lililotegwa ardhini kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Vyombo vya habari vya Kiebrania navyo pia vimeripoti kuwa watu kadhaa waliuawa na kujeruhiwa katika tukio baya sana la kuvizia kusini mwa Ghaza.
Duru nyingine za habari zimebainisha kuwa, bomu liliripuka kwenye njia liliyopita gari aina ya Hummer jeep huko Rafah kusini mwa Ghaza na kujeruhi watu kadhaa ambao wako katika hali mbaya.
Wakati huohuo vyanzo vya Palestina vimeripoti kuwa makombora ya jeshi la utawala ghasibu wa Israel yameshambulia mashariki mwa mji wa Rafah, na wakati huo huo ndege za kivita zimepaa baada ya operesheni ya Muqawama wa Palestina dhidi ya wanajeshi wa Kizayuni katika eneo hilo.
Katika upande mwingine, Jeshi la kizayuni limewaua shahidi Wapalestina wasiopungua 79 katika eneo lote la Ukanda wa Ghaza tangu kulipopambazuka leo, wakiwemo makumi katika Mji wa Ghaza, ambapo mashambulizi makubwa yanaendelea licha ya vitisho vya uwekaji vikwazo vinavyotolewa kimataifa dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza vimeshaua watu wasiopungua 65,141 katika eneo hilo na kujeruhi 165,925 tangu Oktoba 2023 huku maelfu zaidi wakiaminika kuwa wamefunikwa na vifusi…/