Balozi wa Marekani katika utawala wa kizayuni wa Israel, Mike Huckabee amesema, ‘pamoja na Washington kuwa na washirika na marafiki kadhaa katika eneo la Mashariki ya Kati, “Israel ndiye mshirika wetu pekee wa kweli.”

Alipoulizwa kuhusu mjibizo ambao Marekani inaweza ikatoa ikiwa Israel itachukua hatua za kuupora Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuunganisha na ‘ardhi zake’, Huckabee alijibu: “tunaiheshimu Israel kama taifa lenye mamlaka kamili ya kujitawala”.

Balozi huyo wa Marekani mkereketwa wa utawala wa kizayuni ameendelea kusema: “hatutawaambia Israel ni nini inaweza au haiwezi kufanya, kama ambavyo hatutarajii Israel ituambie sisi tunachoweza au tusichoweza kufanya”.

Huckabee amesema: wakati mwingine wanaweza wasikubaliane na Marekani. Ni haki yao. Wao ni taifa lenye mamlaka kamili ya kujitawala na wana kila sababu ya kusema: hatuafiki. Tunamheshimu mshirika wetu.”

Kadhalika, balozi huyo wa Marekani Israel ambaye ni mtetezi sugu wa Uzayuni amekataa msamiati wa “Ukingo wa Magharibi,” akidai “sio sahihi na haliendani na historia,” na akaongezea kwa kusema: “ni neno la kisasa na ni msamiati usio na maana. Sahihi zaidi kuzungumza juu ya Yudea na Samaria, ambalo ni jina lenye historia ya miaka elfu tatu”.

Huckabee amekwenda mbali zaidi kwa kusema, Marekani “inaichukulia Baitul Muqaddas (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu usio na shaka na usiogawanyika wa taifa la Kiyahudi”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *