Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kutokomeza Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) imesema, serikali ya Nigeria inawajibika kwa ukiukaji mkubwa na wa kimfumo wa haki za wanawake na wasichana katikati ya matukio ya utekaji wa watu wengi

Kupitia taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa OHCHR, kamati hiyo imesisitiza kuwa baada ya kupita miaka 10 wasichana 91 wa Chibok wangali wanashikiliwa mateka au hawajulikani walipo, huku waathirika wa tukio hilo wakiendelea kuteseka kwa msononeko na unyanyapaa bila msaada wa kutosha.

CEDAW imechapisha taarifa yake hiyo kufuatia ziara ya siri ya wiki mbili iliyofanya nchini Nigeria mnamo mwezi Desemba mwaka 2023.

Wakati wa ziara hiyo, ujumbe wa kamati hiyo ya UN ulitembelea mji mkuu Abuja na majimbo mbalimbali ikiwemo Adamawa, Borno, Enugu na Kaduna.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nahla Haidar amesema: “utekaji wa wasichana wa Chibok haukuwa tukio la kipekee, bali ni sehemu ya mlolongo wa utekaji wa watu wengi uliolenga skuli na jamii mbalimbali kaskazini mwa Nigeria, japokuwa lilikuwa tukio la kwanza lililojulikana sana duniani”.

Haidar ameendelea kubainisha kuwa, ingawa mashambulizi kama hayo yalianza mapema, Chibok ndiyo iliyowasha mwamko mkubwa wa kimataifa kuhusu mtindo wa utekaji wa watu wengi uliodumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Kwa mujibu wa afisa huyo wa UN, wanafunzi wa kike wapatao 1,400 wametekwa kutoka skuli mbalimbali tangu tukio la Chibok, ambapo Wasichana hao mara nyingi walichukuliwa kwa kutakiwa kikomboleo, kwa ajili ndoa za kulazimishwa, usafirishaji haramu wa binadamu na kubadilishana na wafungwa.

“Kamati imeona kwamba kushindwa mara kwa mara Serikali kulinda wanafunzi wa kike, wanawake na wasichana wengine dhidi ya utekaji ni ukiukaji wa kimfumo na mkubwa,” amesisitiza Bi Haidar.

CEDAW imehitimisha taarifa yake kwa kusema, serikali ya Nigeria imeshindwa kuzuia mashambulizi yanayolenga skuli na jamii, kulinda wanafunzi wa kike dhidi ya utekaji na kuhakikisha haki yao ya elimu. Pia imebaini kwamba, serikali imeshindwa kuondoa unyanyapaa kwa waathirika wa utekaji, hasa waathirika wa ubakaji na watoto wao…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *