Iran imetaja kuwa ya kipuuzi madai ya Marekani kuhusu ustawi wake katika sekta ya makombora, ikielezea mpango huo kuwa wa kujihami dhidi ya mashambulizi ya Marekani na Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, ameashiria matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, hivi karibuni na kusema kuwa kauli zake ni za kipuuzi.

Msemaji huyo amesema kuwa Washington haina haki ya kutoa maoni kuhusu uwezo wa kujihami wa taifa linaloamua kulinda uhuru wake kwa gharama yoyote ile.

Ameongeza kuwa mpango wa makombora ni njia ya Iran “kusimama kidete dhidi ya ulafi, ukatili, na mashambulizi ya madola ya kigeni kama vile Marekani na utawala wa Kizayuni.”

Kauli hiyo inafanana na ile iliyotolewa na Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, ambaye amesema kuwa takwa la Marekani la kutaka vikwazo dhidi ya mpango wa makombora wa Iran“ ni takwa ambalo litakatisha mazungumzo yoyote.”

Wakati wa ziara yake ya Jumatatu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu—yaani Israel—Rubio aliahidi kuendeleza sera ya “mashinikizo ya juu” ya vikwazo dhidi ya Iran, sera ambayo ilianzishwa wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rubio alisema kuwa eti uwezo wa makombora wa Iran ni tishio kwa nchi za Ghuba ya Uajemi na Ulaya.

Katikati ya Juni, Israel ilianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran, ambapo iliwalenga makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi, wanasayansi na raia wa kawaida.

Iran ilijibu kwa kushambulia kwa nguvu, ikivurumisha mawimbi ya makombora ya balistiki na ya hypersonic kwenye maeneo nyeti ya Israel, ikiwemo Tel Aviv, Haifa na miji mingine inayokaliwa kwa mabavu.

Marekani iliingia rasmi vitani kuunga mkono Israel kwa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran. Katika kujibu, Iran ilivurumisha makombora kadhaa yaliyolenga kituo cha jeshi la anga la Marekani cha Al Udeid kilichopo Qatar. Baada ya hapo, na kwa kuhofia kuendelea vita, Marekani ilipendekeza kusitishwa mapigano—ombi ambalo Israel ililikubali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *