Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Leo XIV amesema Wapalestina wanaishi katika “mazingira yasiyokubalika” huku wakihamishwa kwa nguvu katika Mji wa Ghaza, wakati huu wa mashambulizi makubwa yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel.

Papa Leo amesema: “ninaelezea mshikamano wangu wa dhati na watu wa Palestina huko Ghaza ambao wanaendelea kuishi kwa hofu na kuishi katika mazingira yasiyokubalika, wakihamishwa kwa nguvu kwa mara nyingine tena katika ardhi zao”.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki amesisitiza kwamba, anatoa upya ombi lake la kusitishwa mapigano, kuachiliwa mateka, kujadiliwa suluhu ya kidiplomasia, na kuheshimiwa kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu.

Vikosi vya jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel vimeshambulia majengo ya makazi katika Mji wa Ghaza, na kuyageuza vifusi mamia ya majengo ya makazi ya raia. Sambamba na hayo, jeshi hilo linawalazimisha Wapalestina kulihama eneo hilo huku likiendeleza operesheni ya kulivamia na kulikalia kwa mabavu kikamilifu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jeshi la utawala wa kizayuni hadi sasa limeshawaua shahidi Wapalestina wapatao 65,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto huko Ghaza tangu Oktoba 2023. Mashambulio hayo ya mtawalia yamelifanya eneo hilo lisiweze kukalika na kusababisha baa la njaa na mripuko wa magonjwa mbalimbali…/ 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *