
Uingereza itaitambua rasmi Palestina kama Dola mwishoni mwa wiki hii baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhitimisha ziara yake ya kiserikali nchini humo. Hayo yamefichuliwa na gazeti la The i Paper likivinukuu vyanzo vya serikali.
Mnamo mwezi Julai, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alitangaza kuwa nchi hiyo itaitambua Palestina kuwa ni dola mnamo mwezi Septemba katika mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York isipokuwa kama Israel itachukua “hatua madhubuti” kushughulikia hali ya kibinadamu huko Ghaza na kukubali kusitisha mapigano.
Ripoti ya The i Paper imesema, sababu ya kuchelewesha kutolewa tangazo hilo hadi baada ya Trump kuondoka Uingereza ni kwa sababu “ingeweza kuzidisha mivutano na Washington, baada ya Trump na waziri wa mambo ya nje Marco Rubio kuonyesha uungaji mkono mkubwa kwa mashambulio ya ardhini ya Israel huko Ghaza”.
Msemaji wa waziri mkuu wa Uingereza amesema utambuzi huo umeratibiwa ili kulinda uwezekano wa kutekelezwa suluhisho la madola-mawili.
“Mamlaka ya kuwa dola ni haki isiyoweza kubatilishwa ya watu wa Palestina, na ni muhimu kabisa katika kulinda uwezekano wa kutekelezwa suluhisho la madola mawili”, ameeleza msemaji huyo.
Mwaka jana, Ireland, Norway na Uhispania zilijiunga na orodha ya nchi 147 ambazo hivi sasa zinaitambua rasmi Palestina kuwa ni dola.
Ufaransa nayo pia imetangaza mipango ya kulitambua dola la Palestina wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, na hivyo kuwa nchi ya kwanza mwanachama wa G7 kufanya hivyo…/